
Mwaliko wa Kenya kushiriki mkutano wa kundi la nchi saba tajiri duniani (G7) unaoanza Jumatatu, Juni 15, 2026 katika mji wa Evian nchini Ufaransa, umeiweka nchi hiyo ya Afrika Mashariki katika uangalizi wa kimataifa huku baadhi ya mataifa yenye uchumi mkubwa zaidi duniani yakijadili masuala muhimu yanayoikabili dunia.
Kenya ndiyo nchi pekee ya Afrika iliyoalikwa kushiriki mkutano wa viongozi wa G7 wa mwaka huu utakaofanyika kuanzia Juni 15 hadi 17, 2026, ikiripotiwa kuchukua nafasi ya Afrika Kusini.
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron alimwalika Rais wa Kenya, William Ruto kwa lengo la kuhakikisha mitazamo ya Afrika kuhusu mageuzi ya mfumo wa fedha wa dunia na maendeleo yenye usawa inajumuishwa moja kwa moja katika ajenda ya mkutano huo.
Mkutano huo unafanyika wiki chache baada ya Kenya kuwa mwenyeji mwenza wa mkutano wa Ufaransa na Afrika ulioongozwa na Macron na Ruto, hatua iliyoiweka nchi hiyo katika nafasi muhimu ya kuunganisha masilahi ya Afrika na mataifa ya Magharibi.
Kwa miaka ya hivi karibuni, Kenya imejiunga na Afrika Kusini, Senegal, Algeria, Misri, Tunisia, Comoro, Ethiopia, Tanzania, Ghana, Nigeria na Morocco miongoni mwa nchi za Afrika zilizowahi kualikwa kushiriki mikutano ya G7.
G7 ni jukwaa lisilo rasmi la ushirikiano wa serikali linaloundwa na mataifa yenye uchumi mkubwa na yaliyoendelea kiviwanda zaidi duniani, ambayo ni Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Uingereza na Marekani.
Akizungumza na Daily Nation la nchini humo, Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi amesema mkutano huo ni fursa muhimu kwa Kenya na Afrika kuibua masuala yenye umuhimu mkubwa kwa bara hilo.
“Kuna masuala mengi ya kimataifa yatakayojadiliwa. Mbali na ushirikiano wa nchi mbili, Rais Ruto amekuwa sauti muhimu ya Afrika katika masuala ya bara,” amesema Mudavadi.
Amesema Rais Ruto atapata nafasi ya kuzungumzia athari za migogoro ya kimataifa kwa uchumi wa Afrika, hususan vita vya Mashariki ya Kati.
“Mzozo unaohusisha Marekani, Israel na Iran umevuruga usambazaji wa bidhaa mbalimbali ikiwemo mafuta. Vita hivi vinaathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa Afrika. Hii ni nafasi kwa Rais wetu kueleza kwa G7 kuwa huu si mgogoro wa Mashariki ya Kati pekee, bali una madhara makubwa duniani kote, hasa kwa mataifa ya Afrika,” amesema.
Mudavadi ameongeza kuwa suala la mageuzi ya mfumo wa fedha wa dunia litakuwa miongoni mwa ujumbe muhimu ambao Rais Ruto atasisitiza katika mkutano huo.
Pia, amesema mkutano huo utatoa fursa kwa Kenya kueleza hali yake ya madeni na kujadili namna ya kuyakabili.
“Rais pia atazungumzia masuala ya amani na usalama katika ukanda huu. Mfano ni vita vya Sudan ambavyo vinaonekana kusahaulika katika ajenda za kimataifa,” amesema.
Mtaalamu wa masuala ya kimataifa, Calvince Adhere amesema umuhimu wa G7 unatokana na ukweli kwamba unazikutanisha nchi zenye uchumi mkubwa na zilizoendelea zaidi duniani.
Kwa mujibu wake, Kenya inapaswa kutumia jukwaa hilo kutangaza fursa zake kwa jamii ya kimataifa.
“Kwa mtazamo wangu, Nairobi inapaswa kwenda kwenye mkutano huu ikiwa na dhamira ya kuonyesha kile kinachowezekana nchini Kenya.
“Maeneo muhimu ni pamoja na ufadhili wa miradi ya tabianchi. Ikumbukwe kuwa Kenya imekuwa kinara wa hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa nchi zilizo hatarini. Pia, kuna suala la madeni na nafasi ya Kenya katika uchumi wa Afrika Mashariki,” amesema Adhere.
Amebainisha pia kuwa G7 ni jukwaa muhimu la kutafuta uwekezaji wa kimataifa.
Miongoni mwa masuala ambayo Rais Ruto anaweza kuyapa uzito ni urekebishaji wa madeni.
“Baadhi ya madeni hayo yanatokana na nchi za G7. Hivyo wanaweza kujadili namna ya kuyarekebisha ili yaendane na hali ya ndani ya nchi. Kwa sasa karibu nusu ya bajeti iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha, John Mbadi, inaelekezwa katika ulipaji wa madeni. “Hilo ni tatizo kubwa ambalo linaweza kujadiliwa na washirika wa maendeleo,” amesema.
Mkutano huo wa G7 unafanyika wiki chache baada ya Kenya kufanikiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Africa Forward jijini Nairobi, jambo linaloimarisha nafasi yake kama kitovu muhimu cha uchumi na diplomasia katika Afrika Mashariki, hasa katika biashara, ulinzi wa amani, nishati jadidifu na ubunifu wa teknolojia.
“Mbali na diplomasia, Kenya, pia, inaiona G7 kama jukwaa muhimu la kujadiliana kuhusu ushirikiano wenye manufaa katika maeneo yenye mahitaji makubwa zaidi,” amesema Adhere.
Ingawa Kenya imealikwa katika mikutano mitatu ya G7 tangu mwaka 2017, ushiriki wake wa mwaka huu umevutia zaidi kutokana na taarifa za kutoshirikishwa kwa Afrika Kusini kufuatia shinikizo linalodaiwa kutoka Marekani.
“Nadhani hili ni jambo zuri kwa Kenya,” amesema Adhere, akibainisha kuwa Afrika Kusini haina nafasi ya kudumu katika kila mkutano wa G7.
Changamoto za kisiasa za ndani
Taasisi ya utafiti wa sera za kimataifa ya Chatham House imeonya kuwa matarajio ya kimataifa ya Rais Ruto yanakabiliwa na mazingira magumu ya kisiasa nchini mwake.
Katika uchambuzi wake, mtafiti wa Programu ya Afrika wa Chatham House, Fergus Kell amesema maandamano ya hivi karibuni nchini Kenya dhidi ya kituo cha karantini ya Ebola kinachojengwa na Marekani pamoja na mgomo wa usafiri uliosababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta, yanaonyesha namna mazingira ya kimataifa yanavyoendelea kuathiri siasa za ndani.
“Ushiriki wa Kenya katika G7 ambao utabaki kuwa wa alama tu hautasaidia kupunguza shinikizo hizi. Hata hivyo, mjadala wa mkutano huu kuhusu ukosefu wa usawa katika mfumo wa uchumi wa dunia unaweza kuipa Kenya nafasi ya kuzungumzia changamoto za kimuundo ambazo zimekuwa zikizuia uamuzi wake wa ndani,” ameandika Kell.
“Mjadala huu wa G7 unakuja katika wakati mwafaka kwa Kenya. Changamoto kubwa ambayo imekuwa ikiikabili Kenya katika miaka ya karibuni ni mzigo wa deni la taifa, ambapo gharama za kulihudumia zinatumia zaidi ya theluthi moja ya mapato ya serikali,” ameongeza.
“Kwa kuwa China ndiyo mkopeshaji mkubwa zaidi wa nchi moja kwa moja kwa Kenya, imekuwa ikilaumiwa kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, hiyo si picha kamili ya hali halisi. Kumekuwa pia na ongezeko la mikopo ambayo Kenya imekuwa ikichukua kutoka katika masoko ya kimataifa ya kibiashara.”
Deni la taifa la Kenya, pamoja na deni lililohakikishwa na serikali, linajumuisha madeni ya ndani na mikopo kutoka nje ya nchi. Kwa mujibu wa Chatham House, kiwango cha deni la taifa nchini humo kimekuwa kikiongezeka tangu mwaka 2013.
“Viongozi wa Kenya wanapaswa kubeba sehemu kubwa ya lawama kwa ongezeko la haraka la madeni yasiyo na tija. Hata hivyo, athari zisizo za moja kwa moja za mazingira ya uchumi wa dunia zimefanya suluhisho la tatizo hilo kuwa gumu zaidi na lenye maumivu makubwa,” amesema Kell.