Utafiti wa hivi karibuni wa lishe wa SMART, uliofanyika kati ya tarehe 19 na 23 Desemba na kuwachunguza takribani watoto 500, umebaini kiwango cha Utapiamlo Mkali wa Jumla GAM cha asilimia 53.
Kati ya watoto waliopimwa, asilimia 18 waligundulika kuwa na Unyafuzi SAM, hali inayotishia maisha huku asilimia 35 wakikabiliwa na Utapiamlo wa Kati MAM.
Takwimu hizi ni miongoni mwa viwango vya juu zaidi kuwahi kurekodiwa katika utafiti wa lishe uliosanifiwa popote duniani, na ni zaidi ya mara tatu ya kizingiti cha dharura cha Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO, cha asilimia 15.
Mtoto akipatiwa matibabu ya utapiamlo
Maisha ya watoto yako hatarini
“Unyafuzi unapofikia kiwango hiki, muda unakuwa jambo muhimu zaidi,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russell akiongeza kuwa “Watoto wa Um Baru wanapigania maisha yao na wanahitaji msaada wa haraka. Kila siku inayopita bila upatikanaji salama na usio na vikwazo wa misaada huongeza hatari ya watoto kudhoofika zaidi na kufa kwa sababu zinazoweza kuzuilika kabisa.”
Utafiti huo wa UNICEF pia unaonesha kuwa kiwango cha vifo vya jumla katika eneo hilo kimefikia viwango vya dharura, ukisisitiza hatari ya haraka na inayoongezeka inayowakabili watoto.
Watot wakipata matibabu ya utapiamlo Sudan
Ufurushwaji wa watu na magonjwa vyaongeza hatari
Kwa mujibu wa UNICEF wakazi wengi wa Um Baru ni familia zilizofurushwa hivi karibuni ambazo zilikimbia ongezeko kubwa la mapigano mjini Al Fasher mwishoni mwa Oktoba. Idadi kubwa ya watoto miongoni mwao hawajapatiwa chanjo dhidi ya surua na magonjwa mengine yanayozuilika kwa chanjo, hali inayowaweka katika hatari kubwa ya milipuko ya magonjwa na matatizo zaidi ya kiafya.
Mgogoro huu unatokea wakati hali ya usalama ikiendelea kuzorota, jambo ambalo limezuia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa misaada ya kibinadamu na kuchelewesha utoaji wa msaada wa kuokoa maisha.
Mapigano yanayoendelea katika na karibu na eneo hilo yanazuia juhudi za kuongeza kwa haraka huduma muhimu za afya na lishe.
Hali ya usalama imesababisha watu wengi kutawanywa Darfur wakiwemo watoto
Kaskazini mwa Darfur kitovu cha mgogoro
Kaskazini mwa Darfur bado ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi katika mgogoro wa utapiamlo unaoendelea kuongezeka nchini Sudan.
Kufikia Novemba mwaka huu, karibu watoto 85,000 waliokuwa na utapiamlo mkali sana au unyafuzi walikuwa wamepokelewa kwa matibabu katika jimbo hilo pekee.
Ingawa UNICEF imeweka mapema vifaa muhimu vya kuokoa maisha, ikiwemo Chakula cha Tiba Kilicho Tayari Kutumika RUTF, kiwango cha mahitaji kinazidi kwa mbali uwezo wa sasa wa kukabiliana na hali hiyo, na huduma za kina za afya na lishe zinahitajika kwa dharura.
Mtoto wa Sudan katika KAMBI ya DALI, TAWILA – Darfur. Familia yake ilikimbia El Fasher, ambapo njaa iliyokuwa ikiendelea ilithibitishwa mnamo Oktoba 2025
Ufikiaji wa kibinadamu na kusitishwa mapigano
UNICEF inatoa wito kwa pande zote katika mgogoro huo kuruhusu upatikanaji wa haraka, salama na usio na vikwazo wa misaada ya kibinadamu ili msaada wa kuokoa maisha uwafikie watoto na familia zao.
Shirika hilo linaonya kuwa bila kusitishwa kwa mapigano kwa misingi ya kibinadamu kunakotabirika na kuheshimiwa, wafanyakazi wa misaada hawawezi kutoa kwa usalama chakula, maji safi, huduma za afya na ulinzi.
UNICEF pia inaitaka jumuiya ya kimataifa hususan nchi zilizo na ushawishi kwa pande zinazohusika katika mgogoro kuongeza kwa dharura shinikizo la kidiplomasia na kisiasa ili kuhakikisha kusitishwa kwa mapigano kwa misingi ya kibinadamu kunakubaliwa, kunaheshimiwa na kunatekelezwa, ikionya kuwa watoto wanaendelea kulipa gharama kubwa zaidi ya ucheleweshaji huo.