Morogoro. Mbali na dereva wa lori kuhama njia na kugongana uso kwa uso na basi, ajali iliyosababisha vifo vya watu 10 na wengine 23 kujeruhiwa, mvua na mwendokasi pia vinatajwa kuwa chanzo.
Baadhi ya majeruhi wakizungumza leo, Januari mosi, 2026, wakiwa wodini katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, wameeleza waliyoshuhudia katika ajali hiyo iliyotokea jioni ya Desemba 31, 2025, katika Kijiji cha Maseyu, Kata ya Gwata, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, barabara kuu ya Morogoro – Dar es Salaam.
Samson Godfrey, majeruhi wa ajali hiyo, amesema walikuwa wakisafiri kwa mwendo wa kawaida, basi walilopanda likiwa kwenye njia sahihi kabla ya lori kuingia ghafla upande wao.
Askari wa kikosi cha zimamoto na uokoaji mkoa wa Morogoro wakinasua miili ya marehemu walioteketea kwa moto na kunasa kwenye basi dogo la abiria lililogongana uso kwa uso na lori la mizigo eneo la Maseyu kata ya Gwata barabara ya Morogoro – Dar es Salaam usiku wa Desemba 31. Picha Hamida Shariff
“Tulikuwa kwenye line yetu, ghafla lori lilikuwa linaovateki, dereva wa basi akashindwa kulikwepa. Baada ya kugongana, gari likapinduka na kuanza kuwaka moto. Nilijikokota kupitia dirishani, mguu wangu umevunjika, lakini niliweza kujiokoa,” amesema Godfrey.
Kwa upande wake, Pelegrini Mdimu, ambaye pia ni majeruhi, amesema mvua kubwa ilikuwa ikinyesha wakati ajali ikitokea, hali iliyoongeza hatari barabarani.
“Niliondoka stendi ya Morogoro saa moja usiku kwenda kazini Tanga. Tulipofika Maseyu, lori lilitugonga uso kwa uso. Nilijikuta nipo mtaroni, baadaye nikazinduka nikiwa hospitali,” amesema.
Samson Mmali, miongoni mwa majeruhi, akizungumza na Mwananchi jana, Desemba 31, 2025, alisema licha ya dereva wa lori kuvamia njia yao, pia dereva wa basi alikuwa akiendesha kwa mwendokasi, hali iliyochangia ukubwa wa ajali hiyo.
“Ile ajali ilitokana na lori la mizigo lililokuwa linataka kuyapita magari yaliyokuwa mbele yake bila tahadhari, na dereva wetu alikuwa kwenye mwendokasi, kwa hiyo akashindwa kulimudu gari,” amedai Mmali.
Diwani wa Gwata, Adam Ramadhan, amesema yeye pamoja na wananchi wengine walifika eneo la tukio baada ya ajali kutokea, wakaanza kazi ya uokozi kabla ya vyombo vya ulinzi kufika.
“Tulifanikiwa kuwaokoa abiria watano kabla ya Polisi na Zimamoto kufika. Moto ulikuwa mkali, lakini mvua kubwa ilisaidia kuudhibiti,” amesema.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk Joseph Kway, amesema walipokea majeruhi 23, wakiwamo watoto watano.
“Majeruhi ni 23, wanaume 13 na wanawake 10. Wengi walikuwa na majeraha ya mifupa, kichwa na mwili. Watatu wako chini ya uangalizi maalumu, lakini hali zao zinaendelea kuimarika,” amesema.
Askari wa kikosi cha zimamoto na uokoaji mkoa wa Morogoro wakiwa wamebeba majeruhi waliomuokoa kwenye ajali iliyotokea baada ya basi dogo kugongana na lori la mizigo kisha kuwaka moto eneo la Maseyu barabara ya Morogoro – Dar es Salaam usiku wa Desemba 31 mwaka Jana. Picha Hamida Shariff
Dk Kway amesema majeruhi wote walipata matibabu stahiki, ikiwamo kufanyiwa upasuaji, huku watano wakitarajiwa kuruhusiwa baada ya madaktari kujiridhisha na maendeleo yao.
Kuhusu waliokufa, amesema mwili mmoja pekee ndio umetambuliwa.
Akizungumza baada ya kuwajulia hali majeruhi, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Awadh Juma Haji, amesema uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa lori.
“Dereva wa lori alihama njia kwenye eneo lenye kona kali na mteremko mkali, akagongana uso kwa uso na basi. Uzembe huo ulisababisha magari yote mawili kuwaka moto,” amesema.
Amesema Jeshi la Polisi litachukua hatua kali za kisheria dhidi ya dereva aliyesababisha ajali hiyo, huku akitoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani, hususan katika maeneo hatarishi.
“Dereva mwenye uelewa wa sheria asingeovateki kwenye eneo hatari. Tunawakumbusha madereva kuendesha kwa tahadhari ili kuzuia maafa kama haya,” amesema.
Taarifa ya awali
Taarifa iliyotolewa jana, Desemba 31, 2025, na Jeshi la Polisi ilieleza watu 10 wamefariki dunia na wengine 18 walijeruhiwa katika ajali hiyo iliyohusisha basi la abiria aina ya Mitsubishi Fuso, mali ya Kampuni ya Bill Mawio, na lori la mizigo aina ya Howo lenye tela, mali ya Kampuni ya Kikori. Magari yote mawili yaliteketea kwa moto baada ya ajali hiyo.
Askari wa kikosi cha zimamoto na uokoaji mkoa wa Morogoro wakiwa wamebeba majeruhi waliomuokoa kwenye ajali iliyotokea baada ya basi dogo kugongana na lori la mizigo kisha kuwaka moto eneo la Maseyu barabara ya Morogoro – Dar es Salaam usiku wa Desemba 31 mwaka Jana. Picha Hamida Shariff
Basi la abiria lilikuwa likiendeshwa na Swalehe Adamzi, likitokea kituo cha mabasi ya mikoani Msamvu, Morogoro, kuelekea mkoani Tanga, huku lori likiwa na shehena ya mbolea likitokea Dar es Salaam kuelekea mkoani Mbeya.
Taarifa ya Polisi ilieleza chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa lori, aliyejaribu kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari, huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha na kusababisha barabara kuwa na utelezi.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro limetoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za haraka pindi ajali au majanga yanapotokea ili kusaidia uokoaji wa maisha na mali.
Daniel Myala, Ofisa Operesheni wa jeshi hilo mkoani hapa, amewataka madereva na watumiaji wengine wa barabara kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Imeandikwa na Jackson John, Hamida Shariff na Juma Mtanda.