
Iringa. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Allan Bukumbi ametoa wito kwa wakazi wa mkoa huo kusherehekea Mwaka Mpya kwa utulivu na nidhamu ili kulinda usalama.
Akizungumza Mjini Iringa leo Alhamisi Januari Mosi, 2026, Bukumbi amesema Jeshi la Polisi limeimarisha ulinzi katika maeneo yote muhimu na litaendelea kuwepo karibu na wananchi katika kipindi chote cha shamrashamra za kusherehekea Mwaka Mpya.
Amesema kipindi hiki huambatana na mikusanyiko mikubwa ya watu, hivyo nidhamu ya kila mwananchi ni muhimu katika kudumisha usalama na kuzuia vitendo vya kihalifu.
Kwa upande wa usalama barabarani, Kamanda Bukumbi amewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuwa waangalifu ili kuepusha ajali ambazo mara nyingi huongezeka wakati wa sikukuu.
Pia, amewataka wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao ili kuzuia madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi ya baruti au milipuko ya kienyeji.
Amesisitiza pia ushirikiano wa wananchi ni nguzo muhimu katika kuhakikisha sherehe zinafanyika kwa usalama na kila mmoja anasherehekea bila hofu.
“Jeshi la Polisi linawahakikishia wananchi kuwa litakuwa bega kwa bega nanyi kulinda usalama katika maeneo yote ya Mkoa wa Iringa wakati wa sherehe hii ya Mwaka Mpya,” amesema kamanda huyo.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi mkoani Iringa, leo Januari Mosi, 2026, wameiambia Mwananchi Digital kuwa wameanza mwaka kwa amani na furaha, wakisifu hali ya usalama na kutoa wito kwa Jeshi la Polisi kuendelea kudumisha mshikamano na wananchi.
Wananchi hao wamesema waliukaribisha mwaka 2026 kwa utulivu, huku wakieleza matumaini ya mafanikio, afya njema na mabadiliko chanya katika maisha yao.
Mkazi wa Mshindo, Rose Mlowe, amesema:
“Leo tumeamka mapema na tunaendelea na shamrashamra za sikukuu pamoja na familia. Hakuna fujo, kila mtu ana furaha na tunaupokea mwaka huu kwa matumaini mapya.”
Naye Deogratius Mwakaluka wa Ilala amesema:
“Tunaishukuru Serikali na Jeshi la Polisi kwa kuweka mazingira salama. Tumeenda kanisani salama na sasa tupo nyumbani kwa amani, tukiombeana heri bila vurugu.”
Kwa pamoja, wananchi hao wameahidi kuutumia mwaka 2026 kwa bidii, kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na kuwasihi wenzao kuepuka fujo, kufuata sheria na kudumisha amani kwa ustawi wa jamii nzima.