KIKOSI cha Pamba Jiji kimerejea kambini kujifua tayari kwa ngwe iliyosalia na Ligi Kuu Bara pamoja na michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) iliyosimamishwa tangu mapema Desemba mwaka jana kupisha fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 inayoendelea huko Morocco.

Pamba Jiji inayoshika nafasi ya tatu kwa sasa katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa imecheza mechi tisa, ikishinda nne sare nne na kupoteza moja imevuna pointi 16 ikilingana na Yanga iliyocheza mechi sita, zote zikiwa nyuma ya kinara wa ligi hiyo kwa sasa JKT Tanzania yenye pointi 17 kupitia mechi 10.

Akizungumza na Mwanaspoti, Francis Baraza amesema wameanza kurejea kambini tangu Desemba 29 na kuanza mazoezi tayari kwa kujenga timu shindani itakayoanzia pale ilipoishia, kiu kubwa ni kufanya vizuri zaidi msimu huu.

PAMB 01

“Tumerudi mapema ili kuanza kurudisha utimamu wa mwili kwa wachezaji kabla ya ligi haijaanza tena Januari 21, wachezaji walikuwa na mapumziko ya muda mrefu ambayo huwa na kawaida ya kuwarudisha nyuma,” amesema Baraza na kuongeza;

“Hakuna mchezaji ambaye hatambui ugumu tulionao kutokana na ushindani mkubwa uliopo tangu kuanza kwa ligi, hivyo makubaliano ni kuwahi kurudi ili kujijenga kwa ushindani. Lengo ni kumaliza katika Top 5.”

PAMB 02

Baraza amesema anaamini kuwahi kwao kurudi kutaongeza kasi ya ubora kikosini lakini pia atafanyia kazi upungufu aliouona mwanzoni mwa ligi kabla ya kurudi kwa ushindani. Kuhusu usajili amesema hatakuwa na mabadiliko makubwa kikosini mwake kutokana na wachezaji wengi alionao kuweza kufiti na kuendana na ushindani huku akiweka wazi kuwa wataongeza nguvu eneo la ulinzi.

“Ni kweli ni kipindi cha usajili kwenye kikosi changu mpango ni kuongeza beki wa kati. Maeneo mengine kuna wachezaji wengi bora ambao wapo zaidi ya wawili hivyo tutatoa kwa mkopo baadhi ili kwenda kuboresha vipaji vyao.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *