
Jeshi la Marekani limeanzisha mashambulizi mapya dhidi ya boti zinazodaiwa kuwa zimehusika na magendo ya dawa za kulevya, huku mvutano kati ya Wahington na Venezuela ukipamba moto.
Kamandi ya Kusini ya Jeshi la Marekani imeeleza kuwa jana Jumatano ilizishambulia meli tano zinazodaiwa kuhusika na utoroshaji wa dawa za kulevya na kuuwa watu 8.
Hata hivyo Kamandi ya Jeshi la Marekani haikuweka wazi mahali palipojiri mashambulizi hayo siku ya Jumanne na jana Jumatano. Mashambulizi ya hapo awali ya jeshi la Marekani yalifanyika katika Bahari ya Caribbean na mashariki mwa Bahari ya Pacific.
Kamandi ya Kusini ya Jeshi la Marekani imeeleza kuwa boti tatu zilishambuliwa Jumanne wiki hii wakati zilipokuwa zikisafiri pamoja katika njia ilizozitaja kuwa za mihadarati.
Hadi sasa Marekani haijawasisha nyaraka wala ushahidi huru wa kuthibitisha madai yake.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu na wataalamu wa sheria za kimataifa wanasema kuwa oparesheni zinazofanywa na Marekani ni sawa na mauaji ya kiholela, na kueleza kwamba walengwa ni raia wa kawaida ambao si tishio lolote kwa Marekani.
Marekani imekusanya idadi kubwa wanajeshi katika visiwa vya Caribbean, kiwango ambacho kimetajwa kuwa hakijawahi kushuhudiwa katika miongo kadhaa ya karibuni.
Serikali ya Trump na maafisa wa kijeshi wa ngazi ya juu wa nchi hiyo wamekosolewa vikali kufuatia mashambulizi ya Marekani katika eneo la Caribbean yaliyouawa makumi ya watu hadi sasa.