Rais wa Marekani, Donald Trump ametangaza hatua hiyo kupitia mtandao wa kijamii, huku Mwanasheria Mkuu wa serikali ya Marekani akisema kuwa Rais Maduro na mkewe watakabiliwa na mkono kamilifu wa haki na sheria ya kimarekani kwenye ardhi na mahakama ya Marekani kwa kuzingatia mashtaka ya kwanza dhidi yao ya mwaka 2020 wakati wa awamu ya kwanza ya uongozi wa Trump.
Operesheni za vikosi maalum vya Marekani ilianza na mashambulizi ya usiku kucha katika mji mkuu wa Venezuela, Caracas na viunga vyake.
Tayari Venezuela imetangaza hali ya hatari nchi nzima, huku idadi ya majeruhi au vifo pamoja na kiwango cha uharibifu bado kuthibitishwa.
Kauli ya Venezuela
Rais Nicolás Maduro Moros wa Venezuela ndiye alitoa hotuba ndefu zaidi kuliko viongozi wengine kwenye mjadala mkuu wa mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la UN. Hotuba yake ilidumu dakika 48.
Serikali ya Venezuela imelaani kitendo hicho kama “uvamizi wa kijeshi” uliofanywa na Marekani ambao unafuatia miezi kadhaa ya mvutano ikiwemo kuimarishwa kwa shughuli za jeshi la Marekani kwenye pwani ya Venezuela na msururu wa mashambulizi dhidi ya boti zinazodaiwa kusafirisha dawa za kulevya.
Marekani iliagiza kukamatwa kwa meli za kusafirishia mafuta zilizowekewa vikwazo huku kukiwa na vitidsho ya kwamba itazindua operesheni za ardhini ili kumuondoa madarakani Rais Maduro.
Utawala wa sheria
“Katibu Mkuu ana hofu kubwa juu ya mvutano unaoendelea Venezuela, uliofikia kilele hii leo kwa Marekani kutekeleza hatua ya kijeshi nchini humo, na kile kinachoweza kukumba ukanda huo,” imesema taarifa iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa leo Jumamosi Januari 3.
“Bila kujali hali ilivyo nchini Venezuela, hali hii inawakilisha mfano hatari. Katibu Mkuu anaendelea kusisitiza umuhimu wa kuheshimiwa kikamilifu—na wote—kwa sheria za kimataifa, ikiwemo Chata ya Umoja wa Mataifa,” taarifa hiyo imesema.
“Ana wasiwasi mkbwa kwamba sheria ya kimataifa haijaheshimiwa,” imesema taarifa hiyo ikiongeza kuwa Katibu Mkuu anatoa wito kwa pande zote kushiriki kwenye mazungumzo jumuishi kwa mujibu wa sheria ya kimataifa ya haki za binadamu.
Ulinzi kwa raia wa Venezuela
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadmu Volker Türk also naye ametaka kila pande kujizua na kwamba sheria ya kimataifa ya haki za binadamu iheshimiwe.
“Ulinzi wa raia wote wa Venezuela ni muhimu na lazima uwe mwongozo wa hatua zozote zile zitakazofuatia.”
Tayari Venezuela imetaka kuitishwa kwa kikao cha dharura cha Baraza la Usalama jijini New York, Marekani
Trump kazungumza na waandishi wa habari
Kwa upande wake, Rais Trump akizungumza na waandishi wa habari mchana wa Jumamosi Januari 3 kwenye makazi yake ya kifahari ya Mar-a-Lago jimboni Florida kusini mwa Marekani amesema Marekani iliazimia “kuendesha Venezuela” hadi patakapokuweko na kipindi ‘salama, sahihi na cha kisheria cha mpito wa madaraka.’
“Likiwa ni taifa lenye akiba kubwa zaidi ya nishati ya mafuta duniani kampuni za mafuta za Marekani zitaboresha a kukarabati miundombinu iwe ya kisasa ili nchi hiyo iweze kuwa na rasilimali za fedha,” amesema Rais Trump.