Saratani ya shingo ya kizazi ni nini?

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani kupitia machapisho yake kwenye wavuti wake na pia kwenye mtandao wa X zamani Twitter, linasema saratani ya shingo ya kizazi hutokea katika eneo la kuingia kwenye kizazi cha mwanamke, ambapo ni sehemu inayounganisha mfuko wa uzazi na sehemu ya uke. Ugonjwa huu huanza taratibu na mara nyingi hauoneshi dalili katika hatua za awali.

HPV: Chanzo kikuu cha saratani

Karibu asilimia 99 ya visa vyote vya saratani ya shingo ya kizazi vinahusishwa na maambukizi ya virusi hatarishi viitwavyo Human Papilloma virus (HPV). HPV ni virusi vya kawaida sana vinavyosambazwa kupitia ngono. Ingawa maambukizi mengi ya HPV huisha yenyewe bila kusababisha dalili, maambukizi yanayodumu kwa muda mrefu yanaweza kusababisha saratani kwa wanawake.

Virusi aina ya Human Papiloma (HPV) ni maambukizi ya kawaida ya zinaa ambayo yanaweza kuathiri vibaya ngozi, sehemu za siri na koo. Takriban watu wote wanaofanya ngono wataambukizwa wakati fulani wa maisha yao, kwa kawaida bila dalili.

Mara nyingi mfumo wa kinga huondoa HPV kutoka kwa mwili. Maambukizi ya mara kwa mara ya HPV yanaweza kusababisha seli zisizo za kawaida kukua, ambazo huendelea na kuwa saratani.

Kwa vipi maambukizi yanaweza kuchochoea saratani

Maambukizi ya mara kwa mara ya HPV kwenye shingo ya kizazi ikiwa haitatibiwa, husababisha asilimia 95 ya saratani ya mlango wa kizazi. Kwa kawaida, inachukua miaka 15-20 kwa seli zisizo za kawaida kuwa saratani, lakini kwa wanawake walio na kinga dhaifu, kama vile wenye Virusi Vya Ukimwi, (VVU) isiyotibiwa, mchakato huu unaweza kukuwa haraka na kuchukua miaka 5-10. 

Sababu za hatari zinazoweza kusababisha saratani ni pamoja na kiwango cha aina ya HPV, hali ya kinga mwilini, uwepo wa magonjwa mengine ya zinaa, idadi ya kuzaa watoto, ujauzito wa kwanza katika umri mdogo, matumizi ya uzazi wa mpango wakutumia homoni, na kuvuta sigara.

Mwanafunzi akipatiwa chanjo dhidi ya HPV katika kituo cha afya kusini magharibi mwa Côte d'Ivoire.

© UNICEF/Frank Dejongh

Mwanafunzi akipatiwa chanjo dhidi ya HPV katika kituo cha afya kusini magharibi mwa Côte d’Ivoire.

Takwimu za kutisha duniani

Saratani ya shingo ya kizazi ni saratani ya nne kwa wingi zaidi miongoni mwa wanawake duniani. Takwimu za mwaka 2022 zinaonesha kuwa takribani wanawake 660,000 waligunduliwa na ugonjwa huu kote duniani, huku takribani wanawake 350,000 wakifariki kutokana na saratani ya mlango wa kizazi.

Kinga na uchunguzi wa mapema

Wataalamu wa afya wanasisitiza kuwa kinga ya msingi kupitia chanjo ya HPV ni njia bora ya kuzuia ugonjwa huu. Aidha, uchunguzi wa mara kwa mara na matibabu ya mapema ya vidonda vinavyoweza kusababisha saratani ni njia muhimu za kuzuia visa vingi vya ugonjwa huu.

Kukuza ufahamu wa umma, utowaji wa habari na huduma ni muhimu katika kuzuia na kudhibiti katika kipindi cha maisha yote.

Kupata chanjo katika umri wa miaka 9-14 ni njia nzuri sana ya kuzuia maambukizi ya HPV, saratani ya mlango wa kizazi na saratani zingine zinazohusiana na HPV.

Uchunguzi kuanzia umri wa miaka 30 (miaka 25 kwa wanawake wanaoishi na VVU) unaweza kugundua ugonjwa wa kizazi, ambao unapotibiwa, pia huzuia saratani ya shingo ya kizazi.

Katika umri wowote wenye dalili au mashaka, kugunduliwa mapema na kufuatiwa na matibabu ya haraka kunaweza kutibu saratani ya shingo ya kizazi.

Njia zingine muhimu za kuzuia maambukizo ya HPV ni pamoja na:

  • Kutovuta sigara au kuacha kuvuta sigara
  • Kutumia kondomu 
  • Kutahiriwa kwa wanaume kwa hiari.

Matibabu na matumaini

Saratani ya shingo ya kizazi ikigunduliwa mapema, ni mojawapo ya saratani zinazotibika kwa mafanikio makubwa. Hata hivyo, saratani inayogunduliwa katika hatua za mwisho bado inaweza kudhibitiwa kwa matibabu sahihi pamoja na huduma za kutuliza maumivu na kuboresha ubora wa maisha ya mgonjwa.

Ndoto ya dunia isiyo na saratani ya shingo wa kizazi

Kwa kutumia mkakati wa kina unaojumuisha kuzuia, kuchunguza na kutibu, wataalamu wanaamini kuwa saratani ya shingo ya kizazi inaweza kutokomezwa kama tatizo la afya ya umma ndani ya kizazi kimoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *