
Makamu wa Rais wa Venezuela, Delcy Rodríguez, amelaani vikali shambulio la kijeshi la Marekani aliloliita kinyume cha sheria, ambalo limesababisha kutekwa kwa Rais Nicolás Maduro na Mkewe Cilia Flores. Rodríguez ameitaka Marekani iwaachilie wawili hao mara moja na akaonya kuwa Venezuela iko tayari kujilinda.
Akihutubia taifa moja kwa moja siku ya Jumamosi, Rodríguez alieleza kuwa shambulio la alfajiri lilikuwa “la kinyama,” akishutumu Washington kwa kuizingira Venezuela kwa lengo la kubadilisha utawala na kunyakua utajiri wa taifa hilo.
Amesema: “Tunataka kuachiliwa mara moja kwa Rais Nicolás Maduro na mkewe Cilia Flores, rais pekee wa Venezuela.” Ameongeza kuwa, hujuma hiyo imefichua malengo halisi ya Marekani.
Amesema Marekani inafuatilia lengo moja tu nalo ni “kubadilisha utawala wa Venezuela ili wanyakue nishati, madini na rasilimali zetu za asili.”
Ameongeza kuwa: “Wanataka kutufanya watumwa tena. Hatutakuwa watumwa tena, hatutakuwa koloni ya dola lolote, kwa namna yoyote ile.”
Rodríguez ameongeza kuwa serikali iko tayari kulinda taifa na rasilimali zake, akisisitiza kuwa wananchi wa Venezuela wameghadhishwa na “utekaji huu usio halali na usio wa kisheria” wa rais na mkewe. Pia aliwataka raia kubaki watulivu katika hali hii inayoendelea.