*KUFUNGULIWA BARABARA ZA MJI KUNAENDA KUINUA UCHUMI NJOMBE*

Wakazi wa Njombe wamesema ufunguzi na uboreshaji wa barabara za ndani ya halmashauri ya mji njombe unataraji kuongeza kasi ya shughuli za kiuchumi kwa wananchi, hasa kwa kuwawezesha kufikisha bidhaa kwa urahisi kwenye masoko na kupunguza changamoto za usafirishaji.

Wakizungumza mbele ya Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini, Deodatus Mwanyika, wakati akikagua miundombinu ya barabara, Lucy Nyahululi na Stephano Ngailo wamesema kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya miundombinu mibovu ya barabara, na kupelekea gharama kubwa za usafirishaji na kupunguza faida kwa wakulima.

Wakazi hawa wanasema kufunguliwa kwa barabara za ndani kutarahisisha usafirishaji wa mazao kutoka shambani hadi sokoni na kama haitoshi itavutia wafanyabiashara wengi zaidi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mji huo kwa ujumla.

Deodatus Mwanyika, mbunge wa Njombe mjini amesema serikali imejipanga kuendelea kufungua na kuboresha barabara zote kwa kasi, lengo kubwa ni kuifanya Njombe kufikia hadhi ya manispaa.

Mwanyika ameongeza kuwa miundombinu ya barabara ni miongoni mwa vigezo muhimu vinavyoangaliwa katika kufikia hadhi hiyo.

Mhandisi wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Njombe, Nideo Mwinuka, amesema wanaendelea kushughulikia changamoto za miundombinu ya barabara hususan katika kipindi cha mvua, huku akieleza kuwa pamoja na matengenezo ya barabara zilizopo, lakini bado ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami na changarawe unaendelea katika maeneo mbalimbali ya halmashauri hiyo.

Mwandishi @dkhan1410
#RFAOnline
#HabariStartv.

Mwisho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *