
Sherehe za kuadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar, zinazofikia kilele chake Jumatatu ijayo, zimeendelea kushika kasi huku shamrashamra za kila aina zikishuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.
Katika kipindi hiki, Serikali imezindua na kuweka mawe ya msingi au kukagua utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo yenye thamani ya mabilioni ya shilingi.
Miradi hiyo inahusisha ujenzi na ukarabati wa barabara, miundombinu ya madaraka mijini na vijijini, hospitali, vituo vya afya, shule pamoja na shughuli za michezo na burudani zinazofanyika mchana na usiku.
Bila shaka, hatua hizi ni dalili za maendeleo na juhudi za Serikali kuboresha maisha ya wananchi.
ata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, yapo maeneo mawili nyeti ambayo, kwa mtazamo wa uchambuzi huu, yalipaswa kupewa uzito wa kipekee zaidi unaolingana na huduma ya mgonjwa aliyelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
Maeneo hayo ni upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na uhakika wa umeme, hususan katika maeneo mengi ya mjini Zanzibar na vitongoji vyake, pamoja na sehemu kadhaa za Visiwani kwa ujumla.
Kwa muda mrefu sasa, wananchi katika maeneo mbalimbali wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji.
Mabomba ya nyumbani na ya nje yamegeuka kuwa mapambo yasiyo na maana Kinachozidisha kero ni hali ya Mamlaka ya Maji Zanzibar (Zawa), kuendelea kutuma ankara za malipo na ada za huduma, ilhali kwa miezi miwili au mitatu, hata tone moja la maji halijawahi kupatikana.
Ukiangalia vipindi vinavyotoa fursa kwa wananchi kutoa maoni yao kupitia redio mbalimbali na matangazo ya Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), zaidi ya robo tatu ya sauti zinazopata nafasi huibua kilio cha ukosefu wa maji safi na salama au umeme wa uhakika.
Hali hii haiwezi kuridhisha hata kidogo. Mbali na usumbufu mkubwa unaowakumba wananchi katika maisha yao ya kila siku, changamoto hizi zinawarudisha nyuma wengi katika harakati za kujitafutia kipato. Kuna watu wanaotegemea maji au umeme kuendesha shughuli zao za kiuchumi, iwe ni biashara ndogo, huduma za kijamii au uzalishaji na hivyo, kukosekana kwa huduma hizo kunamaanisha kukosekana kwa mapato na kuongezeka kwa umaskini.
Ni katika muktadha huo ambapo hoja inaibuka kuwa masuala ya maji na umeme yalipaswa kupewa kipaumbele kikubwa, sawa au hata zaidi ya kile kilichotolewa kwa maandalizi ya mashindano makubwa ya kandanda ya Kombe la Mapinduzi, ambayo yametumia mabilioni ya shilingi.
Swali la msingi linalojitokeza kipi ni muhimu zaidi katika maisha ya binadamu, michezo na burudani au maji na umeme?
Ingawa michezo na burudani ni muhimu kwa afya ya mwili, akili na husaidia kujenga mshikamano wa kijamii, hazina maana wala ladha panapokuwepo uhaba mkubwa wa huduma za msingi.
Kwa hali kama hii, ni vigumu kwa mwananchi kuacha kuhangaika kutafuta maji ya matumizi ya nyumbani na badala yake, aende kuangalia mpira au kujivinjari katika burudani za muziki.
Ni kweli kuwa wapo wachache wanaoweza kutafsiri hoja hizi kwa misingi ya ubinafsi au mitazamo ya kisiasa, lakini lengo la uchambuzi huu ni kuwasilisha kero za wananchi kwa wahusika ili zipatiwe ufumbuzi. Hili limekuwa jukumu la msingi katika jamii na halipaswi kuwekewa vikwazo.
Kwa mantiki hiyo, ni vyema kutafakari upya vipaumbele vyetu kama jamii na kama Serikali. Tunapaswa kuchukua hatua zote zilizo ndani ya uwezo wetu kuhakikisha matatizo ya maji na umeme yanapatiwa ufumbuzi wa haraka na wa kudumu.
Baada ya hapo, ndipo itakapokuwa na maana zaidi kusherehekea mafanikio kwa michezo na burudani.
Pongezi zinastahili kutolewa kwa viongozi wa Wizara ya Maji ambao, licha ya uhaba wa rasilimali, wamekuwa wakijitahidi kutembelea maeneo yenye matatizo na kutoa maelekezo ambayo yameleta nafuu katika baadhi ya maeneo.
Hata hivyo, kwa upande wa umeme, juhudi hizo bado hazionekani vya kutosha. Malalamiko mengi bado hayapatiwi majibu ya haraka, hata pale yanapohusu hitilafu zinazoweza kuhatarisha maisha ya wananchi.
Kwa hitimisho huu ni wakati wa kubadilika. Wananchi wanahitaji maji safi na salama pamoja na umeme wa uhakika.