Dar es Salaam. Mke wa Saidi Fella, Sweet Fella, amewaomba Watanzania walioguswa na kuumwa kwa mumewe, waweze kumchangia mumewe ili aweze kurejeshwa India mara ya pili kwa ajili ya matibabu, kwani hali yake bado haiko sawa.
Akizungumza na Mwananchi, Sweet Fella amesema, amepata malalamiko mengi kuwa familia hawataki watu watoe misaada wala kwenda kumuona, kitu ambacho siyo sahihi.
Sweet Fella amesema, anajua kuugua mume wake kwake ni ibada na kwamba yupo pamoja naye bega kwa bega hadi dakika za mwisho, ila kwa yeyote atakayeguswa familia iko tayari kupokea chochote.
“Hakuna kitu kibaya, mtu unauguza halafu yanazuka maneno mengi ambayo yanakuwa ya uongo. Mimi binafsi wala familia hakuna mtu aliyekataza Fella asisaidiwe na Watanzania. Yuko ndani huu ni mwaka mmoja sasa toka arudi India kwa matibabu.
“Anaendelea na matibabu ya hapa na pale ana kliniki anaenda kwa wiki mara 2, ana fanya mazoezi kila siku asubuhi ambapo kwa mwezi ni milioni moja na laki mbili. Kuna dawa anaendelea nazo kutumia ili aweze kukaa sawa, pia anatakiwa kurudi India kwa mara ya pili,”amesema
Amesema kutokana na hayo hawawezi kukataa misaada kutoka kwa watu walioguswa na kuumwa kwake.
“Hivyo ni ruksa kwa walioguswa na hali hiyo na wanaotamani kusaidia gharama za matibabu na safari ya India. Mchango wowote unaweza kutumwa kupitia namba 0713781414 ambayo ni namba ya kwake Mkubwa Fella”, amesema Sweet Fella.
Utakumbuka kauli hii imekuja baada ya kusambaa kwa taarifa zikidai mke huyo wa Fella hataku misaada yoyote kutoka kwa Watanzania.
Taarifa za kuumwa kwa Said Fella ‘Mkubwa Fella’ ziliibuka kwenye mitandao ya kijamii Januari, 2025 kuwa amepooza miguu huku wengi wakidai Diamond amemtelekeza.
Hata hivyo baada ya kupata taarifa hizo Mwananchi ilimtafuata nyumbani kwake Mbagala kata ya Kilungule, jijini Dar es Salaam na kuzungumza na baadhi ya ndugu zake ambao walidai hali yake haikuwa nzuri hata kuzungumza na mtu kwa muda mrefu alikuwa anashindwa.
Machi,4, 2025 Mwananchi iliripoti hali ya kiafya ya Mkubwa Fella aliyekuwa akisumbuliwa na presha na kupooza miguu. Hata hivyo Fella alisema afya yake imezidi kuimarika baada ya kutoka India kupata matibabu, ambapo huko India gharama zote aligharamia Diamond Platnumz.
Ilipofika Mei, 2025 Fella alisema kutokana na hali yake kuwa mbaya kwa matatizo hayo. Alikata tamaa ya kupona lakini kwa wakati huo anamshukuru Mwenyezi Mungu kwani anaendelea vizuri.
“Nina furaha kwani kwa sasa naendelea vizuri, hali yangu inaimarika kila siku na nimeanza kufanya mazoezi ya kutembea kila ifikapo jioni.
“Ukweli mimi nimeumwa sana yaani nimeumwa kweli hadi nikawa nimekata tamaa ya kupona, ila namshukuru Mungu sana hadi sasa naweza kuongea na wewe hivi na kutembea vizuri kwa kufanya mzoezi, ilikuwa balaa,” amesema Mkubwa Fella.
Januari 6, 2026 Sweet Fella, aliandika kwa akaunti yake ya Instagram kuwa, anapamba mwenyewe kumuuguza Mkubwa Fella, ila haoni watu wake wa karibu hata kumjulia hali kama ilivyokuwa zamani alikuwa akipigiwa simu za kila wakati usiku wa manane kumuamsha Fella aende kuwasaidia kazi zao hao watu wa karibu.
Katika hao aliwataja watu ambao wapo kipaumbele kutoa sapoti ni Msanii wa muziki wa bongo felva Mbosso, Meneja Said Kessy, na Muddy K rafiki wa karibu wa Mkubwa Fella.