
Taarifa ya WFP iliyotolewa leo jijini Roma, Italia inafafanua kuwa tangu kurejea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe Aprili 2023, WFP imewafikia zaidi ya wanawake, wanaume na watoto milioni 10 walio katika mazingira magumu zaidi nchini Sudan kwa msaada wa chakula cha dharura, fedha taslimu na lishe. Shirika hilo linaendelea kutoa msaada wa chakula unaookoa maisha kwa wastani wa watu milioni nne kila mwezi, ikiwa ni pamoja na maeneo ambayo hapo awali yalikuwa magumu kufikika katika maeneo ya Darfur na Kordofan, pamoja na majimbo ya Khartoum na Al Jazira.
“Maendeleo haya yaliyopatikana kwa juhudi kubwa sasa yako hatarini kubatilishwa,” amesema Ross Smith, Mkurugenzi wa WFP wa Maandalizi na Uokoaji wa Dharura. “WFP imelazimika kupunguza mgao wa chakula hadi kiwango cha chini kabisa cha kuendelea kuishi. Kufikia mwisho wa Machi, tutakuwa tumemaliza akiba yetu ya chakula nchini Sudan. Bila ufadhili wa haraka wa ziada, mamilioni ya watu watabaki bila msaada muhimu wa chakula ndani ya wiki chache.”
WFP ina timu zilizopo maeneo husika na uwezo wa kupanua shughuli zake ili kuokoa maisha zaidi, endapo kutakuwa na ufadhili. Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, karibu watu milioni 1.8 walioko katika maeneo yenye njaa au hatarini kukumbwa na njaa wamepokea msaada wa kila mwezi wa WFP, jambo lililosaidia kupunguza makali ya njaa katika maeneo tisa. Mafanikio ya hivi karibuni, yakiwemo msafara wa pamoja wa Umoja wa Mataifa uliokwenda Kadugli mwezi Oktoba, yamefungua fursa ndogo ya kuzifikia familia zilizokuwa zimekatiwa msaada kwa miezi kadhaa.
Baada ya zaidi ya miaka miwili ya mapigano, zaidi ya watu milioni 21 wanakabiliwa na njaa kali nchini Sudan. Njaa ya kupindukia (famine) imethibitishwa katika baadhi ya maeneo ya nchi ambako miezi ya mapigano imefanya upatikanaji wa wahudumu wa misaada kuwa mgumu sana, na karibu watu milioni 12 wamelazimika kuyahama makazi yao.
Kwa sasa, watoto milioni 3.7 pamoja na akina mama wajawazito na wanaonyonesha pia wanakabiliwa na utapiamlo. Tafiti za hivi karibuni zinaonesha viwango vya juu sana vya utapiamlo katika baadhi ya maeneo ya Kaskazini mwa Darfur, ambako zaidi ya nusu ya watoto wadogo wanakabiliwa na utapiamlo.
“Siku elfu moja za vita ni siku elfu moja nyingi kupita kiasi. Kila siku mapigano yanapoendelea, familia zinaingia zaidi kwenye njaa na jamii zinasukumwa karibu na ukingo wa maangamizi,” anasema Smith. “Tunaweza kubadili mwelekeo na kuzuia kuenea kwa hali ya njaa kali, lakini hilo linawezekana tu ikiwa tutapata ufadhili wa kusaidia familia hizi zilizo katika mazingira magumu zaidi.”
WFP inahitaji kwa dharura dola za Marekani milioni 700 ili kuendelea na shughuli zake nchini Sudan kuanzia Januari hadi Juni.