
Kutoka kwa timu ya kisheria ya utetezi ya Gambia, Jessica Jones amesisitiza jinsi Rohingya walivyokumbana na “kushushwa hadhi kwa muda mrefu na kauli za chuki kutoka kwa maafisa wakuu na wanachama wengine wa jeshi la Myanmar.”
Bi. Jones pia amerejelea video iliyoshapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook Agosti 2017 iliyoonesha mwanajeshi akitoa “Amari ya wazi ya kuchochea ghasia za halaiki dhidi ya Rohingya” matendo ambayo yangekuwa kinyume cha wazi na wajibu wa Myanmar chini ya Mkataba wa Mauaji ya Halaiki wa 1948.
Alisema kwao, nami nakuelezea nikinukuu, “Tutafuta vijiji ambavyo wanyama hao wanaishi. Tuna silaha, tuna risasi. Hivyo ndivyo tulivyokuja navyo, na silaha na ari ya kushambulia wanyama hao. Kama unaweza kubeba upanga, bamba upanga. Kama unaweza kubeba fimbo, bamba fimbo. Beba kile unachoweza na kabiliana kwa ujasiri na wanyama hawa.”
Gambia, taifa lenye wingi wa Waislamu, linadai kwamba viongozi wa kijeshi wa Myanmar walifanya matendo makali ya ukatili wa halaiki dhidi ya watu wa Rohingya kutoka 2016 hadi 2018 katika Jimbo la Kaskazini la Rakhine.
Madhara haya yalijumuisha mauaji ya halaiki, kuuawa kiholela hadi wananchi 10,000 ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto, ukatili mkubwa wa kingono na kuwasha moto kwa makusudi mamia ya vijiji.
Mashambulizi ya kikabila
Mnamo 2017, kiongozi wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wakati huo, Zeid Ra’ad Al-Hussein, alieleza ghasia dhidi ya Rohingya kama mfano wa “usafishaji wa kikabila uliosababisha takriban watu 700,000 miongoni mwao kukimbilia Bangladesh nchi jirani, ambako wengi bado wako leo hii”.
Mwaka 2020, mahakama ya kimataifa iliyoamuru Myanmar kusitisha vitendo yake vya mauaji ya halaiki, kufuatia ombi la Gambia, ambayo sasa inatafuta kuwajibishwa kwa Myanmar kwa matendo yake na kuhakikisha fidia kwa waathirika.
Myanmar kwa muda mrefu imedai kwamba haikuwalenga kwa makusudi watu wa Rohingya na ilitaja kuwa ilikuwa ikitekeleza operesheni za kupambana na waasi.
Kesi ya kihistoria
Kesi hii inaonekana kama hatua ya kihistoria, kwani ni mara ya kwanza majaji wa ICJ kuamuru katika mzozo ulioletwa na nchi ambayo haikuhusishwa moja kwa moja na jinai inayodaiwa.
Wiki ijayo, mashahidi watatu wa Rohingya wamepangwa kutoa ushahidi wao wa kutisha mahakamani kama “wanachama wa kundi lisilo sahihi, wakati usio sahihi na mahali pasipo sahihi walioshuhudia mauaji ya wake na watoto wao,” amesema Philippe Sands wa Gambia, katika maelezo ya hitimisho.
ICJ ni taasisi ya juu ya kisheria ya Umoja wa Mataifa. Inatatua mizozo ya kisheria kati ya nchi na kutoa maoni ya ushauri juu ya masuala ya sheria za kimataifa. Haihukumu watu binafsi, bali inaamua uwajibikaji wa nchi.
Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa The Hague hadi Januari 29.