Katika hotuba yake yam waka 2026 kwa nchi wanachama kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, Guterres amesema mfumo wa kimataifa uko chini ya shinikizo kubwa katika wakati ambao ushirikiano wa kimataifa unahitajika zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa bado ni taasisi muhimu ikiendelea kusukuma mbele juhudi za usimamizi wa akili mnemba, hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, mageuzi ya ufadhili wa maendeleo, misaada ya kibinadamu na juhudi za amani duniani.

“Dunia inahitaji suluhu na Umoja wa Mataifa unazitoa,” amesema, huku akionya kuwa miundo iliyopo haifai tena kwa changamoto za sasa.

Taasisi zilizoundwa mwaka 1945 hazilingani na mahitaji ya leo

Kiini cha hotuba hiyo ni wito mkali wa kuhuisha mifumo ya utawala wa dunia. Katibu Mkuu ameonya kuwa taasisi zilizoanzishwa baada ya Vita vya Pili vya Dunia hazioneshi tena uhalisia wa kisiasa, kiuchumi na kijamii wa leo.

“Mifumo iliyoundwa mwaka 1945 haifai tena kwa changamoto za leo,” amesema, akitaja miundo ya mamlaka iliyopitwa na wakati, upinzani dhidi ya mageuzi, na kuyumba kwa hali ya kifedha ndani ya Umoja wa Mataifa kama vitisho kwa uhalali na ufanisi wa taasisi hiyo.

Amesisitiza kuwa mageuzi lazima yaende zaidi ya masuala ya bajeti, yakijumuisha uwakilishi wa haki zaidi hususan kwa nchi zinazoibukia kiuchumi pamoja na mabadiliko ya ujasiri katika taasisi za kifedha za kimataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Utawala wa Sheria uko hatarini

Katibu Mkuu ameeleza misingi mitatu mikuu ya mwongozo, akianza na haja ya kuheshimiwa kikamilifu kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.

“Heshima ya kuchagua kwa sheria za kimataifa inadhoofisha utaratibu wa dunia,” ameonya, akirejelea kuongezeka kwa kutokuwajibika, ukosefu wa usawa uliokithiri, na mkusanyiko wa nguvu mikononi mwa wachache wakiwemo matajiri na makampuni makubwa ya teknolojia kama vitisho vya moja kwa moja kwa demokrasia, haki za binadamu na maadili ya pamoja.

Amesisitiza kuwa maendeleo ya kasi ya teknolojia, hususan akili mnemba, lazima yasimamiwe kwa manufaa ya umma. “Teknolojia lazima itumikie ubinadamu si faida au mamlaka”.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anatoa hotuba katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, akizungumza na mkutano huo juu ya kazi ya shirika hilo na vipaumbele vyake kwa mwaka 2026.

UN Photo/Manuel Elías

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akitoa hotuba kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, akihutubia baraza Kuu kuhusu kazi za shirika hilo na vipaumbele vyake kwa mwaka 2026.

Amani, tabianchi na maendeleo havitengeki

Akitoa wito wa “jitihada zisizokoma za kuleta amani yenye haki,” Guterres amesema kuwa amani haiwezi kudumishwa bila maendeleo, usawa na kuheshimiwa kwa haki za binadamu.

Ametaja migogoro inayoendelea Gaza, Ukraine, Sudan na maeneo mengine kama ushahidi wa gharama ya kutochukua hatua, akihimiza hatua zinayozingatia kikamilifu sheria za kimataifa.

Pia ameonya kuwa maendeleo kuelekea Malengo ya Maendeleo Endelevu yako “nje ya mkondo, yakikwamishwa na madeni, ukosefu wa ufadhili wa kutosha na ukosefu wa usawa unaoongezeka”.

Mabadiliko ya tabianchi, amesema, ni tishio la kiusalama na dhuluma ya kimaadili. Katibu Mkuu ametoa wito wa kupunguza haraka uzalishaji wa hewa ukaa, mpito wa haki wa nishati, kuongezwa kwa ufadhili wa tabianchi, na ulinzi bora kwa jamii zilizo hatarini zaidi.

Kujenga umoja katika enzi ya migawanyiko

Nguzo ya mwisho ya hotuba hiyo imelenga mshikamano wa kijamii, huku Katibu Mkuu akionya kuwa ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni, taarifa potofu na mgawanyiko wa kijamii vinaendelea kudhoofisha jamii duniani.

“Watu wengi sana wanahisi wametengwa na maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” amesema, akiongeza kuwa hali hiyo inachochea hofu na migawanyiko.

Amehimiza serikali kujenga jamii jumuishi kwa kulinda haki za wahamiaji na wakimbizi, kuwekeza katika mshikamano wa kijamii, kuwawezesha wanawake, vijana, watu wa jamii za asili na watu wenye ulemavu, na kulinda nafasi ya kiraia na uhuru wa msingi.

Wito wa kukomesha kutowajibika

Akihitimisha hotuba yake, Katibu Mkuu amewataka nchi wanachama kupinga hali ya kutowajibika na migawanyiko, kuthibitisha tena Mkataba wa Umoja wa Mataifa kama dira ya maadili, na kuchukua hatua kwa haraka kwa mshikamano.

“Umoja wa Mataifa ni ahadi iliyo hai,” amesema ukumbusho kwamba licha ya tofauti zetu, ubinadamu bado unaweza kuungana kukabiliana na changamoto za pamoja.

Akionya kuwa hatari za kimataifa zinaongezeka na muda unaendelea kupungua, hivyo amesema hatua za pamoja si tu zinawezekana bali ni za lazima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *