Katika kipindi hicho, wanawake na wasichana walikumbwa na mashambulizi ya kila mara ya mabomu na ukatili wa kijinsia, huku wakitengwa na misaada ya kibinadamu. Kutokana na mashambulizi ya kujirudia katika vituo vya afya, dawa ziliisha, na wanawake wajawazito walilazimika kujifungua bila msaada wa mtaalamu yeyote.

Mgogoro huo ulipamba moto mnamo Oktoba 2025. 

“Tulichimba mahandaki ili kujificha na kujikinga ndani yake,” anasema Rania, binti wa miaka 22, ambaye alikuwa mjamzito wakati huo. “Kulikuwa na makombora kila siku.” 

Zaidi ya watu 107,000 wengi wao wakiwa wanawake na watoto – walitoroka El Fasher kwa miguu, bila usafiri, chakula, wala fedha.

Wakati wa safari ya kuelekea kambi ya Al Affad, Rania aliishiwa nguvu na kuzimia njiani, huku akishuhudia wanawake wenzake wakijifungua pembezoni mwa barabara. 

“Ilikuwa inavunja moyo na kutisha,” anasema Rania, ambaye hatimaye alifikishwa hospitalini na kufanyiwa upasuaji wa dharura ili kuokoa maisha yake na ya mtoto wake.

Zainab alikaribishwa vivyo hivyo: “nilikuwa nikingoja kupokea hema, lakini nilijifungua kabla,” aliiambia UNFPA, Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu, ambalo ni shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Afya ya Uzazi.

media:entermedia_image:1e763c49-60e7-42d3-a3b0-b28c0d4b077e

UNFPA Sudan

Mhudumu wa afya wa timu ya kliniki tembezi ya UNFPA anatoa huduma za afya kwa wanawake na watoto waliokimbia makazi yao huko Gedaref, mashariki mwa Sudan.

Wahudumu wa afya waliibuka kuwa Mashujaa 

Hata wahudumu wa afya hawakusalimika. Mkunga Madina Bashir alifungiwa ndani ya msikiti mmoja mjini El Fasher kwa karibu mwaka mmoja akiwa na wanawake wengine 65. Walinusurika kwa kunywa maji ya mvua na kula mimea iliyoota uani.

“Msikiti ulipovamiwa, waliwachukua wanaume wote na kuwalazimisha wanawake kutoka nje bila viatu. Baadhi ya wanawake walikuwa wajawazito – mmoja alijifungua barabarani kwa sababu hatukuweza kufikia hudumakwa wakati.”

Dkt. Ikhlas Ahmed Abdallah, ni daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya wanawake na uzazi kutoka nchini Sudan, na pia ni mama wa watoto watatu, anasimulia jinsi alivyolazimika kulala hospitalini kwa usalama wake. “Kati ya nyumba yangu na hospitali, kulikuwa na zaidi ya mabomu 100 kwa siku. Tulifanya upasuaji tukitumia mashuka na vyandarua vilivyokatwa kwa sababu hatukuwa na vifaa.”

Leo, Dkt. Ikhlas na Madina wenyewe ni wakimbizi katika kambi ya Al Affad, lakini wameendelea na azma yao ya kuokoa maisha kwa kujiunga na timu za matibabu zinazoungwa mkono na UNFPA.

Farha Ahmed, mwanamke aliyepoteza baba, kaka, na mume wake katika vita, alikutana na Dkt. Ikhlas baada ya kutembea kwa wiki nzima akiwa mjamzito huku akimbeba binti yake wa miaka mitatu.

“Nilikuwa nimechoka sana… nilikuwa nimekaa kwenye joto kali, chini ya jua, bila chakula. Dkt. Ikhlas alinipata na kunipeleka hospitali,” anasema Farha akishukuru.

Kwa Dkt. Ikhlas na timu yake, kazi inaendelea licha ya magumu. “Madaktari wakimbizi tunakabiliwa na matatizo mengi, lakini tunaendelea kufanya kazi ya kibinadamu hapa,” anahitimisha daktari huyo.

UNFPA inaendelea kufanya kazi katika Jimbo la Kaskazini kwa kuimarisha huduma ya dharura ya uzazi katika Hospitali ya Wazazi ya Al Dabbah na kuendesha kliniki ya afya ya uzazi katika kambi ya Al Affad. Timu za wakunga wanaozunguka pia zinatumwa na mafunzo yanatolewa kwa wakunga wa jamii na watoa huduma za afya kuhusu usimamizi wa kimatibabu na kupinga vitendo vya ubakaji. 

Baada ya siku 1,000 za vita, karibu theluthi mbili ya idadi ya watu nchini Sudan wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu. Shirika la UNFPA linahitaji dola milioni 4.8 ili kuendeleza huduma za afya ya uzazi na ulinzi kwa wanawake, lakini hadi sasa ni robo tu ya fedha hizo zimepatikana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *