Akizungumza wakati wa ziara yake ya kwanza rasmi tangu ateuliwe  kuwa Kamishna Mkuu, Salih akiwa mjini N’Djamena amesema ukubwa wa mateso aliyoyaona miongoni mwa wakimbizi wa Sudan waliowasili hivi karibuni mashariki mwa Chad ni wa kusikitisha sana na unahitaji hatua za haraka kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.

“Watu wanafika wakiwa hawana chochote isipokuwa majeraha ya kisaikolojia na hofu,” amesema Salih. “Wamepitia ukatili usioelezeka, kulazimika kufungasha virago mara kwa mara, na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Dunia haiwezi kupuuza mgogoro huu.”

Wafungasha virago bila chocchote isipokuwa matumaini

Wakati wa ziara zake katika makazi ya wakimbizi nchini Chad, Salih amekutana na familia zilizokimbia mapigano makali huko Darfur siku chache tu zilizopita. Wengi wao walikuwa tayari wamefurushwa mara kadhaa tangu mgogoro huo uanze.

Wanawake wameelezea kubakwa, huku wengine wakisimulia kuuawa kwa wazazi na ndugu zao. Wengi waliwasili Chad wakiwa wamebeba tu kile walichoweza, wakitafuta usalama baada ya miaka ya hofu na vurugu.

Tangu Aprili 2023, zaidi ya wakimbizi 900,000 wa Sudan wameingia mashariki mwa Chad, huku wageni wapya wakiendelea kuwasili kila siku.

Kwa ujumla, vita vya Sudan vimewasababisha watu milioni 12 kuhama makazi yao, wakiwemo zaidi ya wakimbizi milioni 4.3 katika eneo zima.

“Huu sasa ni mgogoro mkubwa zaidi wa watu kufurushwa makwao duniani,” amesisitiza Salih. “Nyuma ya takwimu hizi kuna watu halisi ambao maisha yao yamesambaratika.”

Barham Salih, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Ajili ya Wakimbizi, anatembea na maafisa wa Chad na wafanyikazi wa UNHCR kwenye mpaka wa Chad na Sudan huko Adre, kutembelea wakimbizi waliohamishwa tangu Aprili 2023.

© UNHCR/Hélène Caux

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa wakimbizi na Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, Barham Salih akiwa katika uwanja wa ndege wa Adre Barham Salih, akiwatembelea wakimbizi huko Adre kwenye mpaka wa Chad na Sudan.

Hali ngumu na ukata wa fedha

Ingawa UNHCR inaendelea kuongoza juhudi za kuokoa maisha nchini Chad, Salih ameonya kuwa upungufu wa fedha unazidi kudhoofisha operesheni za kibinadamu.

Familia nyingi za wakimbizi hazina makazi ya kutosha, upatikanaji wa maji uko chini sana ya viwango vya dharura, na vyoo vilivyojaa kupita kiasi vinaongeza hatari za kiafya. 

UNHCR imeongeza kuwa viwango vya msongo wa mawazo ni vya juu sana, lakini huduma za afya ya akili zinawafikia wachache tu kati ya wanaohitaji msaada. Maelfu ya watoto bado hawajaweza kurejea shuleni.

“Tunafanya kila tuwezalo, lakini pengo kati ya mahitaji na rasilimali linaendelea kupanuka,” amesema Salih. “Bila msaada zaidi, hali itazidi kuwa mbaya.”

Kujenga mnepo licha ya mgogoro

Licha ya changamoto hizo, Salih ameangazia programu zinazosaidia wakimbizi na jamii zinazowahifadhi kujenga upya maisha yao kwa heshima na utu.

Katika eneo la Iridimi, amekutana na wanafunzi wakimbizi wanaopata ujuzi wa kidijitali na lugha ili kuendeleza masomo yao na kuongeza fursa za ajira. 

Huko Farchana, ametembelea bustani za masoko ambako wakimbizi na jamii za  wenyeji hulima na kuuza mazao pamoja. 

Nako Abeche, amekutana na kundi la wanasheria, madaktari na walimu waliokimbia Sudan ambao sasa wanaweza kuendelea na taaluma zao nchini Chad.

“Wakimbizi si waathirika tu,” amesema Salih. “Wakipewa fursa, wanachangia kikamilifu katika jamii zinazowahifadhi.”

Chad yapongezwa kwa kudumisha haki ya kuhifadhi wakimbizi

Salih ameipongeza Chad kwa kuendelea kutoa hifadhi na kuheshimu ulinzi wa kimataifa wa wakimbizi licha ya changamoto kubwa za kiuchumi na shinikizo la mazingira.

Katika mazungumzo yake na Rais Mahamat Idriss Déby Itno mjini N’Djamena, Salih amethibitisha tena dhamira ya UNHCR ya kuunga mkono wakimbizi na jamii zinazowahifadhi kwa ushirikiano na Serikali.

Pia amesisitiza utayari wa UNHCR kushirikiana na Serikali na wadau wengine kutekeleza mbinu jumuishi ya makazi, zinazolenga kuimarisha huduma kwa wakimbizi na jamii za wenyeji kwa pamoja, huku zikipanua fursa za kiuchumi zinazoshirikishwa.

“Ukarimu wa Chad ni mfano kwa dunia,” amesema Salih. “Lakini mshikamano lazima ugawanywe. Wakimbizi na jamii zinazowapokea hawawezi kuachwa kukabiliana na mgogoro huu peke yao.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *