“Hali ya majira ya baridi tuliyoihofia sasa imekuwa hali halisi,” amesema Mwakilishi wa UNICEF nchini Ukraine, Munir Mammadzade, akizungumza na waandishi wa habari katika hii leo mjini Geneva Eswis. 

Ameongeza kuwa “Mashambulizi makali yanaharibu mifumo muhimu ya nishati na maji wakati halijoto ikizidi kushuka iko chini ya nyuzijoto sufuri.”

Familia zilizo na watoto hukusanyika ndani ya hema la 'Point of Invincibility' lililotengenezwa kwa joto huko Kyiv, Ukraine, wakati wa kukatika kwa umeme kwa majira ya baridi. Wazazi hujaza vifaa na kuandaa vinywaji vya moto wakati watoto wakicheza na vitu vya kuchezea na udongo wa mfano, kwa msaada wa vifaa vya misaada ya kwanza ya kisaikolojia ya UNICEF na huduma za kisaikolojia.

© UNICEF/Oleksii Fili

Familia zinatafuta mahali pa joto pa kuzuia baridi na msaada ndani ya hema la kuhama wakati wa kukatika kwa umeme wakati wa majira ya baridi kali huko Kyiv, Ukraine.

Maisha katika nyuzijoto ya -18

Kote nchini Ukraine kwa mujibu wa UNICEF familia nyingi zimekosa Vipasha joto, umeme na maji kwa siku kadhaa huku halijoto ikishuka hadi nyuzi joto -18C.

“Watoto na familia zao wako katika hali ya kupambana kuishi kila wakati,” amesema Mammadzade. “Maisha nyumbani katika maghorofa ni kujilinda dhidi ya mashambulizi yasiyokoma na kuhimili baridi kali.”

Katika moja ya kitongoji mjini Kyiv, mama mmoja aitwaye Svitlana anajitahidi kumtunza binti yake wa miaka mitatu, Arina, katika ghorofa ya kumi bila vipasha joto wala umeme kwa zaidi ya siku tatu.

“Hana uwezo wa kumuogesha mtoto au kuandaa chakula cha moto,” ameeleza Mammadzade. “Anamfunika Arina kwa nguo nyingi na kushuka ngazi kumi gizani hadi kwenye hema lililo nje ili angalau wapate joto.”

Mahema ya dharura yatoa joto na msaada wa kisaikolojia

Mahema hayo, yaliyoanzishwa na Huduma za Dharura za Serikali ya Ukraine kwa msaada wa UNICEF, yamekuwa tegemeo muhimu kwa familia nyingi. 

Ndani yake, watoto na wazazi hupata joto, chakula cha moto, huchaji simu zao na kuzungumza na wanasaikolojia.

“Wakati mwingine familia hukaa tu ndani kupata hali ya joto,” amesema Mammadzade. “Hilo pekee ni ahueni.”

UNICEF pia imeweka vifaa vya msaada wa kisaikolojia, ikiwemo michezo na vifaa vya kuchezea, ili kuwasaidia watoto na watu wazima kukabiliana na hofu na msongo wa mawazo unaochochewa na giza, baridi na mashambulizi ya mara kwa mara.

Watoto wachanga wako katika hatari kubwa zaidi

UNICEF imeonya kuwa athari za kimwili na kiakili kwa watoto ni kubwa. Kukaa muda mrefu kwenye baridi kali huongeza hatari ya magonjwa ya kupumua, huku hofu na msongo wa mawazo vikiongeza madhara ya kisaikolojia.

“Watoto wachanga ndio walio hatarini zaidi,” amesisitiza Mammadzade. “Watoto wadogo na wachanga hupoteza joto la mwili kwa haraka na wako kwenye hatari kubwa ya hypothermia na magonjwa ya kupumua hali ambazo zinaweza kuhatarisha maisha bila joto na huduma za afya.”

Elimu nayo imeathirika pakubwa amesema. Baridi kali imesababisha shule na vituo vya chekechea katika mji wa Kyiv na maeneo mengine kurejea masomo ya mtandaoni. Hata hivyo, kukatika kwa umeme mara kwa mara kunavuruga masomo hayo, na kuwaacha watoto wengi bila fursa ya kujifunza.

Mammadzade amesema“Kwa watoto wengi, elimu imekuwa tena jambo lisilo na uhakika.” 

media:entermedia_image:07c774c8-b413-44b7-89ec-2911ab7b0df4

© UNOCHA/Matteo Minasi

Msichana mwenye umri wa miaka mitano akingoja pamoja na mama yake kupanda basi kwenda Poland kutoka Zaporizhzhia kusini mwa Ukrainia. “Maisha ya watoto bado yanatumiwa na mawazo ya kuishi na sio utoto,” UNICEF ilionya.

Kukimbizana na muda kurejesha huduma

Licha ya uharibifu mkubwa, mafundi wa nishati na maji wanafanya kazi bila kuchoka kurejesha huduma za umeme, vipasha joto na maji.

“Mara tu uharibifu unapofanyika, mafundi hodari wako tayari kazini,” amesema Mammadzade. “Ni mashindano dhidi ya muda.”

UNICEF inaunga mkono juhudi hizo kupitia hatua zake kubwa za majira ya baridi zinazolenga kusaidia watu milioni 1.65, wakiwemo watoto 470,000.

Uwekezaji uliofanywa miezi na hata miaka iliyopita sasa unaokoa maisha.

“Baada ya mashambulizi ya hivi karibuni na kukatika kabisa kwa umeme Zaporizhzhia na Dnipro, hospitali ziliendelea kufanya kazi kwa sababu jenereta na mifumo ya nishati ya jua iliwekwa mapema kabla ya majira ya baridi,” amesema Mammadzade.

Kyiv, UNICEF ilisambaza jenereta kutoka kwenye akiba zilizowekwa awali ili kuzuia kusimama kabisa kwa huduma muhimu baada ya vituo vya joto kuharibiwa. 

Shirika hilo pia linatuma jenereta 79 zenye uwezo mkubwa kote nchini na kutoa msaada wa fedha wa majira ya baridi kwa zaidi ya watu 183,000, wakiwemo watoto 86,000.

Kupitia mfumo wa elimu, misaada ya majira ya baridi inasaidia shule na vituo vya chekechea 1,500 kukarabatiwa haraka na kuendelea kutoa mazingira salama kwa wanafunzi takribani 445,000.

Kuongezeka kwa vifo vya watoto na majeruhi 

Takribani miaka minne tangu kuanza kwa vita, UNICEF inasema maisha ya watoto nchini Ukraine bado yamegubikwa na hofu na mateso.

“Maisha ya watoto bado yanatawaliwa na mawazo ya kuishi, siyo ya utoto,” amesema Mammadzade.

Onyo hilo linakuja wakati ambapo kumekuwa na ongezeko la asilimia 11 la idadi ya watoto waliouawa au kujeruhiwa mwaka 2025 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. 

Takriban watoto 92 waliuawa na 652 kujeruhiwa mwaka jana pekee. 

Tangu kuanza kwa vita kamili, zaidi ya watoto 3,200 wameuawa au kujeruhiwa.

UNICEF imerudia kutoa wito wa kusitisha mara moja mashambulizi dhidi ya maeneo ya raia na miundombinu muhimu.

“Hii ni miundombinu ambayo watoto wanategemea kuishi,” amesema Mammadzade. Hivyo “Lazima ilindwe.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *