Mahitaji ya umeme ulimwenguni yanakua kwa kasi ya kutisha, ambapo ifikapo mwaka 2035 yanatarajiwa kuongezeka kwa zaidi ya saa 10,000 za terawati, kiasi ambacho ni sawa na matumizi yote ya sasa ya nchi zilizoendelea.

Kuibuka kwa akili mnemba kuna nafasi kubwa katika ongezeko hili kwani teknolojia hiyo inaendeshwa na vituo vya data ambavyo hutumia umeme mwingi; kituo kimoja cha ukubwa wa kati hutumia umeme sawa na kaya 100,000.

Mwezi Desemba mwaka jana, watunga sera, makampuni ya teknolojia, na viongozi wa sekta ya nyuklia walikutana katika makao makuu ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) mjini Vienna, Austria ili kuchunguza fursa za nishati ya nyuklia katika kuwezesha upanuzi wa AI.

media:entermedia_image:cc3bf0fb-fa64-43f0-8eff-46e4e564fcd5

© Unsplash/Geoffrey Moffett

Nishati ya nyuklia kama mshirika wa Akili Mnemba

Kufunza mifumo ya kisasa ya Akili Mnemba kunahitaji maelfu ya vipengele vya uchakataji kufanya kazi mfululizo kwa wiki au miezi. Manuel Greisinger, meneja mwandamizi wa Google anayeshughulikia AI, amesisitiza hitaji la nishati thabiti akisema, “tunahitaji umeme safi, thabiti na usio na kaboni unaopatikana saa 24 kwa siku. Hili haliwezi kufikiwa kwa nishati ya upepo na jua pekee. AI ni injini ya siku zijazo, lakini injini bila mafuta haina faida. Nishati ya nyuklia si chaguo tu, bali ni kiungo muhimu kisichoepukika cha mfumo wa nishati wa baadaye.”

Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Rafael Mariano Grossi, anaamini kuwa sekta ya nyuklia imekusudiwa kuwa mshirika wa nishati kwa mapinduzi ya AI. Anabainisha kuwa, “nishati ya nyuklia pekee ndiyo inayoweza kukidhi mahitaji matano ya uzalishaji wa umeme wa kaboni kidogo, kutegemewa kwa saa 24, msongamano mkubwa wa nguvu, utulivu wa gridi, na uwezo thabiti wa kukua.”

Hivi sasa, vinu vipya 71 vinajengwa duniani kote ili kuongezea vinu 441 vinavyofanya kazi sasa. Makampuni makubwa ya teknolojia yameahidi kuunga mkono lengo la kuongeza uwezo wa nishati ya nyuklia duniani mara tatu ifikapo mwaka 2050.

Kwa mfano, Microsoft imesaini mkataba wa miaka 20 ulioruhusu kitengo kimoja cha mtambo wa nyuklia wa Three Mile Island nchini Marekani kuanza kufanya kazi tena. Nchi kama Ufaransa na Uingereza zinaongeza ujenzi wa vinu, huku Poland ikiharakisha ushiriki wake; pia Russia inabaki kuwa muuzaji mkuu wa teknolojia ya vinu vya hali ya juu wakati China ikipiga hatua kubwa katika Akili Mnemba na nyuklia kwa pamoja.

Je, ujenzi wa vinu vidogo ni suluhisho?

Hitaji la nishati ya haraka pia linachochea ujenzi wa vinu vidogo vya kisasa (SMRs) ambavyo vinaweza kuwekwa karibu na maeneo ya viwanda ikijumuisha vituo vya data. Grossi anaongeza kuwa, “vinu vya aina hii vina ukubwa mdogo na mifumo ya usalama iliyoboreshwa, na vinaweza kuwekwa karibu na maeneo ya viwanda, ikijumuisha kampasi za vituo vya data. Makampuni ya teknolojia yanayovitumia hayatalazimika kuwa na wasiwasi kuhusu vikwazo vya usambazaji wa gridi ya kikanda au upotevu wa nishati wakati wa usafirishaji.”

Google imekuwa kampuni ya kwanza duniani kusaini mkataba wa kununua nishati kutoka kwa vinu vidogo kadhaa ambavyo vinaweza kuanza kazi ifikapo mwaka 2030. Aidha, kampuni hiyo inatafiti mifumo ya jua kutoka anga za juu ili kuwezesha mifumo ya Akili Mnemba iliyo kwenye obiti, huku satelaiti mbili za majaribio zikitarajiwa kurushwa mapema mwaka 2027.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *