
Utafiti wa chanjo uliogharamiwa na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC) nchini Guinea‑Bissau umekosolewa vikali na wataalamu wa afya pamoja na maafisa wa ndani ya taasisi hiyo, huku afisa mmoja wa CDC akiuulinganisha na jaribio maarufu la kaswende la Tuskegee.
Jarida la Marekani la The New Republic liliripoti Alhamisi kwamba utafiti huo, uliopokea ufadhili wa dola milioni 1.6 kutoka CDC, unachunguza athari za chanjo ya homa ya ini B kwa idadi ya vifo vya watoto, magonjwa na ustawi wa muda mrefu ya watoto.
Jarida la afya la Inside Medicine lilinukuliwa likiripoti kuwa lilipata taratibu za utafiti huo, ambao katika tangazo la Federal Register umeelezwa kama “jaribio la nasibu lililodhibitiwa ili kutathmini athari za chanjo ya homa ya ini B kwa watoto wachanga katika vifo vya mapema, magonjwa, na maendeleo ya muda mrefu.”
Kulingana na ripoti hiyo, jaribio hilo linawahusisha watoto wachanga nchini Guinea‑Bissau na linalinganisha mbinu tofauti za utoaji chanjo badala ya kutumia placebo.
Wasiwasi kuhusu utafiti huo ulielezwa na afisa mmoja wa CDC ambaye hakutajwa jina, aliyeliambia jarida la Inside Medicine na kulifananisha jaribio hilo na “jaribio la Tuskegee,” ambamo serikali ya Marekani iliwaacha makusudi wanaume Weusi wa Alabama waishi na kaswende bila matibabu kati ya mwaka 1932 na 1972.
Baada ya kuchapishwa kwa ripoti hiyo, afisa mwandamizi wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa Afrika (Africa CDC)Africa alitangaza kwamba utafiti huo umefutwa.
Mgogoro huo umeibuka katikati ya mjadala mpana kuhusu sera za chanjo na maadili ya utafiti wa afya ya umma chini ya serikali ya sasa ya Marekani, huku wakosoaji wakidai kuwa utafiti huo umeonyesha mabadiliko katika vipaumbele vya CDC.