Rabat, Morocco. Pazia la Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 linafungwa rasmi leo kuanzia saa 4:00 usiku kwa mchezo wa fainali utakaozikutanisha Senegal na wenyeji Morocco kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdallah, Rabat, baada ya Nigeria jana kunyakua medali ya mshindi wa tatu kwa kuifunga Misri kwa mikwaju ya penalti.
Ni fainali inayokutanisha timu mbili ambazo zimekuwa na mwenendo mzuri kwenye fainali hizo kuanzia katika hatua ya makundi hadi leo hii zinapokutana kwenye Fainali.
Katika mechi tano ambazo kila moja imecheza kwenye AFCON awamu hii, zote zimekuwa na matokeo ya kufanana ambapo kila timu imeibuka na ushindi mara tano na kutoka sare moja.
Utofauti baina yao unaletwa na mabao ya kufunga na kufungwa ambayo zimepata kwenye mechi zao.
Senegal yenyewe katika mechi sita zilizopita za mashindano hayo, imefunga mabao 12 huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili.
Morocco imefunga mabao tisa huku safu yake ya ulinzi ikifungwa bao moja tu ambalo iliruhusu katika hatua ya makundi.
Historia yakoleza moto
Kabla ya leo, timu hizo zimewahi kukutana mara 38 katika mechi tofauti kwa miaka yote iliyopita.
Idadi hiyo ya michezo waliyokutana inaifanya Morocco iwe namba tatu katika orodha ya timu ambazo zimekutana mara nyingi na Senegal katika historia yake ya soka la kimataifa.
Timu pekee zilizocheza dhidi ya Senegal mara nyingi zaidi ni Guinea iliyokutana nayo mara 53 na Mali ambayo imeumana nayo mara 43.
Kwa upande wa Morocco, ni Tunisia pekee ambayo wamecheza nayo mara nyingi zaidi ambapo imecheza mechi 55 dhidi yao hivyo Senegal ni ya pili kwao katika orodha ya timu ambazo imekutana nazo mara nyingi.
Cha kushangaza zaidi ni kwamba, pamoja na historia hiyo ndefu ya kucheza mara 38, timu hizo mbili hazijawahi kabisa kukutana katika AFCON.
Hili ni jambo la ajabu sana ukizingatia nguvu, hadhi na mafanikio ya mataifa haya mawili kwa miaka mingi, pamoja na ukweli kwamba kwa jumla wamecheza mechi 145 katika historia ya AFCON—lakini cha kushangaza ni kwamba hawajawahi kukutana uso kwa uso katika michuano hiyo hadi sasa.
Morocco imekuwa na ubabe mkubwa dhidi ya Senegal ambapo katika mechi 38 walizowahi kukutana, imeshinda mechi 21 huku Senegal wakipata ushindi mara tisa, na mechi nane zikimalizika kwa sare na Morocco imefunga mabao 51 wakati huo Senegal ikiwa imefunga mabao 25.
Vita nne za kibabe
Ni mechi ambayo itakuwa na vita nne kubwa ambazo mamilioni ya wapenzi wa kandanda barani Afrika watakuwa wakitamani kuona nani atakuwa mshindi kwa kila moja.
Vita ya kwanza inazihusu timu zenyewe ambayo ni ya kuwania kutwaa taji hilo. Morocco inasaka taji hilo kwa mara ya pili tangu ilipolichukua mara ya kwanza mwaka 1976 kama ilivyo wa Senegal ambayo nayo ilichukua mwaka 2021.
Makocha Walid Regragui wa Morocco na Pape Thiaw baada ya kukosa taji hilo wakiwa wachezaji, kila mmoja sasa anawania kulichukua akiwa kocha.
Vita ya kuwania zawadi ya ufungaji bora nayo itaamriwa kama ilivyo kwa vita ya kuwania tuzo ya kipa bora wa mashindano hayo.