
Dar es Salaam. Access Bank Tanzania Limited imetambuliwa kama Benki Bora kwa ufanisi wa muunganiko wa mipata na upanuzi wa soko la Tanzania katika Tuzo za Global Brand Frontier 2025, hatua inayothibitisha nafasi yake katika ukuaji wa kimkakati na uboreshaji wa huduma za kifedha nchini.
Tuzo hiyo imetolewa na taasisi ya Boston Brand Research & Media, ikitambua mafanikio ya benki hiyo katika kuunganisha mipata kwa ufanisi huku ikiendelea kupanua wigo wake wa soko bila kuathiri ubora wa huduma.
Waandaaji wa tuzo wamesema utendaji wa Access Bank Tanzania unaonesha uwezo wa kuendesha mabadiliko kwa utulivu, kuongeza ufanisi wa kiutendaji na kuleta thamani ya muda mrefu kwa wateja na wadau wake.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Access Bank Tanzania, Imani John, amesema mafanikio hayo yanatokana na juhudi za pamoja za wafanyakazi wa benki hiyo na ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali.
“Tuna furaha kupokea utambuzi huu unaoakisi nidhamu, ushirikiano na bidii ya timu yetu. Kuunganisha mipata mikubwa sambamba na kupanua wigo wa soko kumetuhitaji kujifunza kwa kuendelea na kuwa na mwelekeo wa malengo ya pamoja,” amesema John.
Ameongeza kuwa anatoa shukrani kwa wateja, wakaguzi, wanahisa, wanakamati na wafanyakazi wote wa Access Bank Tanzania kwa imani na msaada wao, akisisitiza kuwa benki itaendelea kutoa huduma kwa uwajibikaji na kujenga taasisi imara yenye manufaa ya muda mrefu kwa Watanzania.
Tuzo za Global Brand Frontier hutolewa kwa mashirika yanayoonesha uongozi, ubunifu na ubora katika sekta mbalimbali duniani. Kwa Access Bank Tanzania, utambuzi huu unaonesha mchango wake unaokua katika sekta ya huduma za kifedha na dhamira ya kujenga benki jumuishi na yenye mtazamo wa mbele.
Kwa sasa, benki hiyo inaendelea kupanua mtandao wake, kuboresha huduma na kutumia teknolojia za kisasa ili kukidhi mahitaji yanayobadilika ya watu binafsi, wafanyabiashara wadogo na wa kati pamoja na makampuni makubwa nchini.
Access Bank Tanzania, ambayo awali ilijulikana kama BancABC Tanzania, ni tawi la Access Bank PLC na imeidhinishwa na Benki Kuu ya Tanzania.
Benki hiyo ina matawi katika miji ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Dodoma, pamoja na mtandao wa mawakala 936 wa Access Wakala na maduka 98 ya BancEasy.
Mnamo 2024, benki hiyo iliunganishwa rasmi na Access Bank Group, moja ya makundi makubwa ya kifedha barani Afrika yenye uwepo katika nchi 24, zaidi ya vituo 700 vya huduma na wateja zaidi ya milioni 63. Kupitia mtandao huo wa kikanda, Access Bank Tanzania inanufaika na teknolojia, uzoefu na mifumo imara ya utawala wa benki mama.
Katika utekelezaji wa ajenda yake ya maendeleo endelevu, Access Bank Tanzania inaunganisha maadili ya uwajibikaji wa kijamii na kimazingira katika shughuli zake, ikilenga kukuza ukuaji wa kiuchumi wenye tija na athari chanya kwa jamii.