Hivi sasa, WFP na washirika wake wanaendesha mamia ya maeneo ya usambazaji wa chakula na maghala 20 ndani ya Gaza, ikiwemo maeneo ya kaskazini kama Bait Lahia na kambi ya Jabalia ambapo wanatoa vifurushi vya chakula, vifurushi vya mkate, milo ya moto, na milo ya shule.
Kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mzozo, zaidi ya watu milioni moja wanapokea mgao kamili wa unga wa ngano na masanduku ya chakula kila mwezi, huku milo ya moto zaidi ya 400,000 ikitolewa kila siku kupitia majiko 45 ya kijamii.
Wapalestina waliohamishwa wanaoishi katika mahema ya muda kati ya magofu na majengo yaliyoharibiwa kando ya pwani ya Gaza.
Licha ya mafanikio hayo, takwimu za Awamu Jumuishi ya Uhakika wa Chakula (IPC) za mwezi Desemba zinaonesha kuwa asilimia 77 ya idadi ya watu bado wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, huku zaidi ya watu 100,000 wakiwa katika kiwango cha juu zaidi cha njaa (IPC-5). Karibu kila familia katika Ukanda wa Gaza inategemea misaada ya chakula ili kuishi.
Mwakilishi na Mkurugenzi wa WFP nchini Palestina, Maxime Le Lijour, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza usaidizi huo:
“Siku mia moja baada ya usitishaji vita, mahitaji ya watu bado ni makubwa na mafanikio yaliyopatikana katika usalama wa chakula bado ni tete. Tunapaswa kuendeleza mtiririko wa misaada ya kuokoa maisha huku tukianza kujenga upya maisha, utofauti wa lishe, na uwezo wa watu kujitegemea kuelekea mchakato wa kurejea katika hali ya kawaida.”
Mbali na chakula, WFP inasaidia kutoa ruzuku ya fedha kidijitali kwa kaya 60,000 ili kununua bidhaa katika masoko ya ndani, ingawa mfumuko wa bei bado ni changamoto kubwa kwa familia nyingi. Pia, kupitia mpango wa lishe, shirika hilo linawafikia wanawake na watoto 200,000 walio katika hatari ya utapiamlo, halkadhalika kutengeneza fursa za ajira kupitia viwanda vya kuoka mikate.
Hata hivyo, operesheni hizi zinakabiliwa na vikwazo vya miundombinu iliyoharibika na ukosefu wa mifumo ya usafirishaji wakati wa baridi. Ingawa mafanikio makubwa yamefikiwa katika kuzuia baa la njaa, hali bado ni tete na inahitaji ufunguzi wa kudumu wa njia zote za mipakani pamoja na utulivu wa usalama ili kuzuia eneo hilo kurejea katika baa la njaa.
WFP imebainisha kuwa barabara salama za kupitia Jordan na Misri, pamoja na ufunguzi wa barabara ya Salah Eddin, ni mambo ya lazima ili kuongeza ufanisi wa usambazaji.
Taarifa ya WFP imehitimisha kwa kutoa onyo kuhusu hali ya hewa ikisema familia nyingi bado hazijajiandaa vyema kukabiliana na miezi ya baridi kali wakiwa nje, kwani mamia ya maelfu bado wamefurushwa kutoka makazi yao na wanaishi kwenye mahema au majengo yaliyoharibiwa vibaya hivyo usitishaji vita thabiti na upatikanaji wa misaada bila vikwazo ndiyo njia pekee ya kuhakikisha utu, utulivu, na matumaini kwa wananchi wa Gaza katika mwaka wa 2026.