Rais Donald Trump wa Marekani ametangaza kuwa, kuanzia Februari Mosi, ataweka ushuru wa 10% kwa nchi zinazopinga kuunganishwa Greenland na Marekani na kwamba, kuanzia tarehe Mosi Juni ushuru huo utaongezwa na kufikia 25%.

Washington imesema kwamba ushuru huo utaendelea kutekelezwa hadi Marekani itakaponunua Greenland. Denmark, Norway, Sweden, Finland, Uholanzi, Ufaransa, Ujerumani na Uingereza ni miongoni mwa nchi zitakazojumuishwa katika ushuru huo.

Ingawa Donald Trump alizungumzia suala la kuinunua Greenland wakati wa muhula wake wa kwanza wa urais, lakini katika muhula wake huu wa pili katika Ikulu ya White, amesisitiza kama moja ya matakwa yake makuu.

Katika miezi ya mwanzo ya kipindi hiki, Trump alitangaza kwa kauli zilizo wazi kwamba Marekani inataka kuinunua Greenland kwa sababu za kiusalama, kiuchumi na kistratijia, na analitambua suala hili kuwa sehemu ya maslahi muhimu ya Marekani katika karne ya 21.

Sasa Trump ameenda mbali zaidi na ameonya wazi kwamba, upinzani wa washirika kwa mahitaji haya unaweza kuwa na gharama za kiuchumi; msimamo unaoonyesha kuwa wazo la kununua Greenland sasa limekuwa sera nzito na sehemu ya mkakati wa serikali yake wa mashinikizo na utumiaji mabavu wa kiuchumi, kiasi kwamba, sasa imeweka rasmi ushuru wa 10% kwa nchi zinazopinga nia yake ya kunyakua Greenland.

Vitendo hivi vinafanyika wakati watu wa Greenland wamesisitiza rasmi kuendelea na hali iliyopo na kusalia chini ya Denmark. Kadhalika, maelfu ya watu wa Denmark walikusanyika katika mji wa Copenhagen na kulaani madai na vitisho vya Trump vya kuikalia kwa mabavu Greenland.

Viongozi wa Ulaya pia wamechukua msimamo dhidi ya matakwa haya ya Trump. Katika radiamali zao kwa jaribio la Trump kutwaa Greenland, nchi za Ulaya zimesisitiza kuwa, zitatetea mamlaka ya Denmark juu ya kisiwa hiki. Ujerumani na Ufaransa pia zimetuma vikosi vya kijeshi huko Greenland.

Kwa hakika, Trump ameingia uwanjani kwa lugha ya mabavu; lugha ambayo imekuwa sifa kuu ya tabia yake katika uhusiano wa kigeni wa Marekani kwa miaka mingi na imechukua nafasi ya diplomasia ya kawaida. Kwa mtazamo huu, mashinikizo ya kiuchumi si wenzo wa kukamilisha siasa, bali kiini chake.

Katika sera ya Trump, ushuru huo umepata maana mpya na ya kutia wasiwasi. Ushuru sio tena chombo cha kusaidia uzalishaji wa ndani au kurekebisha usawa wa biashara, lakini kimekuwa chombo cha adhabu ya kisiasa. Nchi yoyote ambayo haiendani na matakwa ya Washington itakabiliwa na shinikizo la kiuchumi badala ya mazungumzo.

Kuwekwa ushuru wa 10% dhidi ya nchi ambazo zimepinga mradi wa unyakuzi wa Greenland kunatuma ujumbe wazi kabisa: Kupinga Marekani kuna gharama zake. Hapa ndipo hasa mahali ambapo ushuru hugeuka kutoka chombo cha kiuchumi na kuwa silaha ya kulazimisha kisiasa.

Trump ameonyesha mara kwa mara kuwa katika msamiati wake wa kisiasa, ushuru sio suluhisho la mwisho, lakini ni radiamali ya kwanza. Badala ya kujaribu kujenga maafikiano au kuwashawishi washirika, anaamua kuharibu uhusiano na kutoa mashinikizo, na badala ya diplomasia ya kimataifa, anafuata sera hatari ya “ama uwe pamoja nami au dhidi yangu”.

Kinachofanya tabia hii kuwa ya kutisha zaidi ni kuhalalisha unyanyasaji wa kiuchumi katika ngazi ya kimataifa. Kwa kutumia mara kwa mara ushuru huo kama chombo cha vitisho, Trump amejaribu kuanzisha mantiki ya mabavu na ubabe kama sheria halali katika mahusiano ya kimataifa.

Ushuru wa kibabe wa Trump unaonyesha aina ya mtazamo wa dharau kwa nchi zingine; mtazamo ambao hauwaoni na ushirika, na badala yake ni wa ufuasi. Kwa sera hii, Trump anajaribu kulazimisha matakwa yake na kuzuia muqawama wowote.

Kwa muhtasari wa hadithi ya Greenland na sera ya ushuru ya Trump, inaonyesha kuwa kutumia shinikizo la kiuchumi kama njia ya kuweka utashi sio mkakati mzuri, lakini ni ishara ya kushindwa kusukuma mbele gurudumu la siasa kupitia njia halali na za kisheria.

Uzoefu wa miaka ya hivi karibuni umeonyesha kwamba, sera hiyo haiimarishi nafasi ya Marekani wala kuongezeka kwa ushawishi wake, bali hatau hizo zinapelekea kuibuka muqawama, miungano mbadala na kujitenga polepole kwa washirika kutoka Washington.

Katika fremu hii, sera ya Trump ya ushuru imekuwa sababu ya kufifisha nafasi ya Marekani katika mfumo wa kimataifa, badala ya kuwa chombo cha kujenga mamlaka; njia ambayo muendelezo wake hauna matunda mengine ghairi ya kuiongezea gharama Washintgton.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *