Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekaribisha kukabidhiwa kambi ya anga ya Ain al Asad kwa vikosi vya jeshi la Iraq na kuitaja hatua hiyo kuwa ishara ya kuimarishwa utuvulivu na mamlaka ya kujitawala Iraq.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari baada ya kumlaki mwenzake wa Iraq, Fuad Hussein mjini Tehran jana Jumapili, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araqchi, alisema kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq amefanya ziara Tehran muda mfupi baada ya uchaguzi wa Bunge wa Iraq.

Araqchi amemshukuru Fuad Hussein kwa ziara yake nchini na kusema pande mbili tayari zimefanya duru mbili za majadiliano yaliyozaa matunda. 

Amesisitiza kuwa kukabidhiwa kwa Iraq kambi ya anga iliyokuwa ikidhibitiwa na Marekani ni hatua iliyoungwa mkono pakubwa na Jamhuri ya Kiislamu. 

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran kwa mara nyingine tena amethibitisha nia thabiti ya Tehran ya kuiona Iraq ikiwa imara, inayojitawala na yenye muundo huru wa kisiasa.  

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria uhusiano unaozidi kuimarika kati ya mataifa hayo mawili na kueleza kuwa makumi ya maelfu ya wanafunzi wa Iraq wanasoma nchini Iran, na zaidi ya raia milioni saba husafiri kati ya nchi hizo mbili kila mwaka.

Araqchi ameongeza kuwa yeye na mwenzake wa Iraq wamejadili mapendekezo ambayo yanaweza kuratibiwa kidiplomasia kati ya Iran na Iraq ili kuboresha amani na utulivu katika kanda hii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *