Nyota wa Senegal, Sadio Mane amesema kuwa aliamua kuwakataza wenzake kugomea mechi ya fainali ya AFCON 2025 dhidi ya Morocco jana kwa vile tukio hilo linaharibu taswira ya soka.

Katika dakika za lala salama za mechi hiyo, Kocha Mkuu wa Senegal, Pape Thiaw aliwaamuru wachezaji wake kutoka nje ya uwanja kufuatia uamuzi wa Refa Jean-Jacques Ndala kuamuru penalti kwenda langoni mwao baada ya Brahim Diaz kufanyiwa faulo na Malick Diouf.

Hata hivyo Sadio Mane alionekana kutokubaliana na uamuzi wa kuondoka uwanjani ambapo alionekana akiwashawishi wenzake kuendelea na mchezo.

Uamuzi wa Senegal kurejea uwanjani na kuendelea na mchezo, ulikuwa na faida kwa upande wao kwani Morocco walikosa mkwaju huo wa penalti uliopigwa na Brahim Diaz na baadaye ikatwaa ubingwa kwa ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Pape Gueye.

Akizungumzia mchezo huo, Mane anasema kuwa kwake ni bora wangepoteza mechi kuliko kugomea mchezo.

“Mpira wa miguu ni kitu cha kipekee, dunia ilikuwa inaona, dunia inapenda soka na nadhani mpira wa miguu ni burudani hivyo tunapaswa kutoa taswira nzuri kwa mpira wa miguu.

“Nadhani ingekuwa ni uchizi kutocheza kwa sababu gani, refa ametoa penalti na sisi tutoke nje ya mchezo. Nadhani ingekuwa jambo baya hasa kwa soka la Afrika. Nipo tayari kupoteza kuliko hili kutokea katika soka letu.

“Nadhani ni vibaya sana. Mpira wa miguu hautakiwi kusimama hata kwa dakika 10 lakini nini tunatakiwa kufanya? Tunatakiwa kukubaliana kwamba tumefanya lakini jambo zuri nk kwamba tulirudi na kucheza mechi na kilichotokea kilishashatokea,” amesema Mane.

Ushindi huo wa jana umeifanya Senegal kutwaa kwa mara ya pili ubingwa wa AFCON na Mane alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mashindano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *