Ulaya. Uhusiano wa gwiji wa Barcelona, Andres Iniesta (41), na mkewe Anna Ortiz (39), ni moja kati ya simulizi za mapenzi zenye mvuto mkubwa, simulizi iliyoanzia ufukweni kama bahati na sasa inasimama kama historia.
Safari ya mapenzi ya Iniesta na Anna ilianza katika mgahawa mdogo wa ufukweni (chiringuito) mwaka 2007, wakati huo, Iniesta alikuwa tayari ni staa wa Barcelona, lakini bado alikuwa kijana anayetazama huku na kule.
Kwa upande wake, Anna alikuwa akifanya kazi kama muhudumu wa mgahawa huo, na alishangazwa kumuona mchezaji maarufu eneo hilo na hakujua kuwa angekuja kuwa mwanaume wa maisha yake.
“Nilikutana naye usiku wa sherehe za San Juan (Juni 23) 2007, nilienda kukutana na mtu kwenye chiringuito ambapo alikuwa akifanya kazi hapo, na mara tu nilipoingia na kumuona Anna, nilimpenda,” alieleza Iniesta.
Walianza kukutana nje ya saa za kazi, na ndani ya miezi michache walijikuta wakipendana sana, na hatimaye Anna alihamia nyumbani kwa Iniesta kama mpenzi, kisha akawa mchumba, mke na sasa mama watoto.
Baada ya kuwa pamoja kwa takribani miaka minne hadi mitano, hatimaye Iniesta na Anna walifunga ndoa hapo Julai 8, 2012, ambapo shughuli nzima ilifanyika huko Costa Dorada, Tarragona nchini Hispania.
Harusi yao ilikuwa ya kifahari ikihudhuriwa na wageni takribani 700 wakiwemo wachezaji wenzake wa Barcelona kwa wakati huo. pamoja na wachezaji kutoka timu nyingine.
Miongoni mwa mastaa wakubwa wa soka waliokuwepo ni Lionel Messi, Xavi Hernandez, Gerard Pique, Carles Puyol, Cesc Fabregas, Sergio Busquets, Pedro, Victor Valdes, Iker Casillas na Samuel Eto’o.
Pia walihudhuria makocha kama Pep Guardiola, Vicente del Bosque, Luis Aragones na Jose Camacho, pamoja na marais wa zamani na wa wakati huo wa Barcelona Joan Laporta na Sandro Rosell.
Hadi sasa ndoa ya Iniesta na Anna imebarikiwa kupata watoto wenye afya na furaha. Binti yao wa kwanza, Valeria alizaliwa mnamo Aprili 2011, kabla hata ya ndoa yao.
Kwa ujumla wamejaliwa watoto watano, mabinti watatu na wavulana wawili, waliozaliwa kati ya mwaka 2011 hadi 2023.
Hata hivyo, Machi 2014, familia ilipitia kipindi kigumu walipompoteza mtoto wa kiume aliyekuwa tumboni kutokana na mimba kuharibika, tukio lililowaumiza sana lakini pia kuwaimarisha zaidi.
Baadaye, waliendelea kubarikiwa watoto wengine ambao ni Paolo (2015), Siena (2017), Romeo (2019) na Olympia (2023), na siku zote wanandoa hao wameonyesha ni kiasi gani wanawapenda watoto wao.
Kutoka kukutana ufukweni hadi kuwa wenzi wa maisha waliopitia furaha na huzuni pamoja, Iniesta na Anna wameza kujenga familia imara inayoheshimika ndani na nje ya uwanja wa soka.
Anna aliyezaliwa Desemba 11, 1986 huko Catalunya, Hispania katika familia ya kipato cha kati, anapenda maisha ya utulivu na hapendi vyombo vya habari kuingilia maisha yake binafsi.
Maisha yake ya awali hayakuwa rahisi kama yalivyo leo, kabla ya kukutana na Iniesta, Anna alikuwa akifanya kazi kama mhudumu wa mgahawa mdogo, hivyo alitoka chini kabisa kimaisha.
Pamoja na changamoto hizo, tangu mwanzo alikuwa na mtazamo chanya na alipambana hadi kufika alipo kwa sasa, si tu mke wa mwanasoka maarufu bali mbunifu maarufu wa mavazi na mfanyabiashara aliyefanikiwa.
Kwa kuwa ana jicho kali la mitindo na akili yenye ubunifu, alifuata ndoto yake ya kuwa mbunifu wa mavazi, na tayari amefanya kazi katika miradi mingi ya kampuni kubwa huko Catalunya.
Alipata umaarufu zaidi Instagram baada ya uhusiano wake na Iniesta kuwekwa wazi, na kwa sasa hutumia mtandao huo vizuri akiweka picha zake na familia, pamoja na kutangaza kazi zake za mitindo.
Iniesta mara nyingi humchukulia Anna kama bahati yake (lady luck), mwanamke aliyempa utulivu na nguvu ya kuendelea kung’ara uwanjani akishinda mataji yote makubwa Hispania, Ulaya na duniani.
Kipindi ambacho mashabiki walikuwa wanaona na kufurahia mafanikio ya Iniesta, nyuma ya pazia kulikuwa na upendo na msaada wa dhati kutoka kwa Anna.
Katika kipindi chote cha mafanikio na changamoto za Iniesta kama kukumbwa na majeraha na msongo wa mawazo, Anna alikuwa karibu naye kila wakati.
Na sasa Iniesta anachukuliwa kuwa mmoja wa viungo bora kabisa kuwahi kucheza soka, alianza safari yake katika akademi ya Barcelona (La Masia), na baadaye akawa mmoja wa wachezaji bora zaidi duniani.
Baadhi ya mataji aliyoshinda akiwa na Barcelona ni Ligi Kuu Hispania (La Liga) mara tisa, Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA CL) mara nne, UEFA Super Cup mara mbili na Kombe la Dunia la Klabu mara tatu.
Katika kikosi cha timu ya taifa ya wakubwa ya Hispania, Iniesta ameshinda Mashindano ya Mataifa ya Ulaya (Euro) mara mbili (2008 & 2012), na Kombe la Dunia 2010, michuano iliyofanyika nchini Afrika Kusini.