Dar es Salaam. Tukio la Rich Mavoko kuondoka ndani ya WCB Wasafi lilikuwa la kihistoria kwa kuwa alikuwa ndiye msanii wa kwanza kuondoka katika lebo hiyo ya Diamond Platnumz tangu kuanzishwa kwake.
Ikiwa ni takriban miaka saba imepita tangu hilo kutokea, bado kuna mjadala mpana kuhusu uamuzi wake huo na athari ulizoacha katika safari yake ya muziki na chapa yake kiujumla. Utakumbuka kuwa Rich Mavoko alijiunga na WCB Wasafi 2016 akiwa msanii wa tatu kusainiwa, baada ya Harmonize na Rayvanny, mshindi wa BET 2017.
Tofauti na wenzake hao, Rich Mavoko aliingia WCB Wasafi akiwa tayari ni msanii mkubwa mwenye mashabiki wengi na nyimbo zilizokuwa zimetamba sana kama Silali, Follow Me, Pacha Wangu, One Time, Marry Me na kadhalika.
Umaarufu wake ulimweka katika nafasi ya kipekee kiasi cha kuanza kulinganishwa kimuziki na Diamond, jambo lililozua mijadala mikubwa kwenye tasnia kwamba nani mkali zaidi. Mwaka 2018, Rich Mavoko aliondoka WCB Wasafi baada ya mvutano mkubwa uliodumu kwa muda na hata kufikia Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kwa lengo la kupata usuluhishi.
Kipindi hicho, zilienea taarifa kwamba kusainiwa kwake katika lebo hiyo kulikuwa na lengo la ‘kumuua kimuziki’, madai ambayo yalikanushwa vikali na uongozi wa WCB Wasafi. Hata hivyo, Rich Mavoko aliwahi kueleza kuwa kabla ya kusaini mkataba huo hakuwahi kukutana wala kuzungumza na Diamond moja kwa moja!.
Alieleza kuwa ni rapa AY aliyemkutanisha na meneja wa Diamond, Sallam SK wakiwa Uganda, kwenye show ya mwanamuziki wa huko, Jose Chameleone, ndipo mazungumzo ya kujiunga na WCB Wasafi yalipoanzia.
Akiwa chini ya WCB Wasafi, Rich Mavoko alitoa kazi zilizopokelewa vizuri na mashabiki, zikiwemo Ibaki Stori (2016), Kokoro (2016) akiwa na Diamond, na Rudi (2017) aliyoshirikiana na Patoranking kutokea Nigeria. Hata hivyo, licha ya mafanikio hayo, safari yake ndani ya lebo haikudumu kwa muda mrefu, aliamua kushika njia aliyoona ni sahihi kwake, huku lebo ikibaki na msimamo wake. Kwa mujibu wa kauli zake mwenyewe, Rich Mavoko hakulipa fedha yoyote ili kuondoka WCB Wasafi, tofauti na Harmonize aliyelazimika kulipa kile kinachoitwa fidia ya mkataba.
Ushahidi wa kimazingira unaoonekana na hadi leo unaunga mkono kauli hiyo. Video zote za nyimbo alizotoa chini ya WCB Wasafi, kama Ibaki Stori, Kokoro na Rudi, ziliondolewa kwenye mtandao wa YouTube.
Aidha, chaneli yake ya awali iliyokuwa na video hizo pamoja na kazi zake nyingine za zamani haikutumika tena tangu aondoke WCB Wasafi, na hadi leo hii ipo hivyo. Inaaminika kuwa chaneli hiyo ilibaki chini ya umiliki wa WCB Wasafi, jambo lililomlazimu Rich Mavoko kuanzisha chaneli mpya iitwayo Billionea Kid mnamo Agosti 14, 2018.
Hadi sasa, kazi zake katika chaneli hiyo zimefanikiwa kutazamwa (views) zaidi ya mara milioni 21.9, idadi ambayo bado ni ndogo ikilinganishwa na wenzake walioondoka Wasafi wakiwa na chaneli zao.
Baada ya kuachana na WCB Wasafi, nyimbo zake zilizofanya vizuri zaidi YouTube ni Naopoga (views milioni 2.4), Mapenzi (milioni 1.7), Wamoto (milioni 1.7), Ndegele (milioni 1.4) na Usizuge (milioni 1.3).
Hii ni tofauti kubwa ukilinganisha na Harmonize na Rayvanny ambao wameendelea kupata namba kubwa zaidi kutokana na kuondoka na majukwaa yao waliyoyajenga awali.
Utakumbuka wimbo wa kwanza wa Rich Mavoko kuachia baada ya kuondoka WCB Wasafi ulikuwa Ndegele, uliotoka Agosti 17, 2018, huku video yake ikiongozwa na Director Adam Juma.
Licha ya yote, Rich Mavoko hajawa mzungumzaji sana wa tukio la kuondoka WCB Wasafi kama ilivyo kwa Harmonize. Pia sio msanii wa matukio au kiki za mitandaoni kama ulivyo utamaduni wa lebo hiyo.
Ni wazi kuwa ukimya huu unamfanya kutozungumziwa sana kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, jambo ambalo huwenda linaathiri mapokezi ya kazi zake anapozitoa. Ukweli ni kwamba, katika tasnia ya muziki ya sasa hasa hapa Bongo, kujadiliwa na kuonekana mara kwa mara ni sehemu ya mafanikio, na hata kuikuza chapa.
Wasanii wengi wakubwa hulipa fedha ili majina yao yaandikwe na kujadiliwa, wakitambua kuwa hapo ndipo nguvu ya umaarufu wao ilipo ila kwa Rich Mavoko imekuwa tofauti kidogo. Hata lebo yake, Billionea Kid hajawahi kumsaini msanii yeyote na hii ni tofauti na wenzake, Harmonize na Rayvanny kupitia lebo zao, Konde Music Worldwide na Next Level Music (NLM), tayari walishaini wasanii.