Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeitaka Serikali kuongeza jitihada za kulinda usalama na afya ya wafanyakazi nchini kwa kupanua wigo wa usimamizi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), ili kuifikia kikamilifu sekta isiyo rasmi.

Kamati hiyo imesema licha ya sekta binafsi kuajiri mamilioni ya Watanzania, bado inakabiliwa na changamoto kubwa za usalama kazini, hali inayowaweka wafanyakazi katika hatari ya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hawa Chakoma, wakati akihitimisha kikao kati ya Kamati na Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) kilichofanyika leo Januari 19, 2025, bungeni Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, akizungumza wakati wa kujibu hoja zilizoibuliwa na wajumbe wa Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii leo, Januari 19, 2026.

Kikao hicho kililenga kupokea na kujadili taarifa ya muundo na utekelezaji wa majukumu ya taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ikiwamo OSHA na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).

Chakoma ameipongeza OSHA kwa mchango wake katika kuimarisha usalama na afya mahali pa kazi kupitia ukaguzi, utoaji wa miongozo na ushauri wa kitaalamu kwa waajiri na wafanyakazi.

Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mfumo madhubuti wa ufuatiliaji ili kuhakikisha mapendekezo yanayotolewa wakati wa ukaguzi yanatekelezwa ipasavyo.

“Kamati imebaini kuwa baadhi ya waajiri hufuata sheria na kanuni za usalama pale tu wanapotembelewa na wakaguzi wa OSHA, lakini baada ya hapo hupuuza taratibu hizo, jambo linalowaweka wafanyakazi katika hatari kubwa,” amesema Chakoma.

Aidha, Kamati imeishauri Serikali kutafuta mbinu bunifu za kuijumuisha sekta isiyo rasmi katika mfumo rasmi wa usimamizi wa masuala ya usalama na afya kazini, hatua inayolenga kulinda nguvu kazi kubwa inayojishughulisha na shughuli za kujiajiri, hususan katika sekta nyeti kama usafirishaji, ujenzi na biashara ndogondogo.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati hiyo na Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Kafiti William Kafiti, amesema kikao hicho kimeiwezesha Kamati kupata uelewa wa kina kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano).

Amesema uelewa huo utaongeza ufanisi wa Kamati katika jukumu lake la kuishauri Serikali na kusimamia taasisi husika kwa maslahi ya wafanyakazi na waajiri.

Akiwasilisha taarifa kwa niaba ya Serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, amesema OSHA na WCF zina mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuleta ustawi wa wafanyakazi na waajiri nchini.

Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuziimarisha taasisi hizo ili ziweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

OSHA ni miongoni mwa taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), zenye jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Na. 5 ya mwaka 2003, ambayo inaweka msingi wa kitaifa wa kulinda usalama na afya ya wafanyakazi pamoja na uwekezaji katika shughuli zote za kiuchumi nchini.

Kwa wito huo wa Kamati ya Bunge, macho sasa yanaelekezwa kwa Serikali kuona ni kwa namna gani itachukua hatua za haraka na za kudumu kuhakikisha haki ya kufanya kazi katika mazingira salama inalindwa kwa wafanyakazi wote, hususan waliopo katika sekta isiyo rasmi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *