Musoma. Mahakama Kuu ya Tanzania, imelitangaza Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kuwa ndiye mmiliki halali wa msikiti wa Masjid Rahman, uliojengwa kwa ufadhili wa aliyekuwa Rais wa Libya, Muammar Gaddafi.

Fedha za ujenzi wa msikiti huo ambao unajumuisha msikiti, hosteli na nyumba ya makazi, ziliombwa kwa Gaddafi na Baba wa Taifa wakati wa uhai wake, Hayati Julius Nyerere. Ujenzi wake ulianza mwaka 1999 na ukakamilika mwaka 2000.

Shauri la mgogoro huo wa ardhi namba 19695 la mwaka 2024 lilifunguliwa na Bodi ya Wadhamini ya Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya Bakwata, ambayo mahakama imeipa ushindi.

Hukumu ya shauri hilo ambayo imewekwa katika tovuti ya mahakama leo Jumanne, Juni 23, 2026, imetolewa Juni 18, 2026 na Jaji Marline Komba wa Mahakama Kuu, Masjala ya Musoma akisema mdai ameshindwa kuthibitisha umiliki huo.

Wadai katika shauri hilo wameeleza kuwa Waislamu wa Kijiji cha Butiama (Butiama Muslim Community), walijikusanya na kujipanga kujenga msikiti huo.

Walitafuta fedha kwa ajili ya ujenzi huo kutoka kwa Mwalimu Nyerere na kufanikiwa kujenga msikiti, hosteli na nyumba ya makazi na ujenzi wake ulianza mwaka 1999 na kukamilika mwaka 2000 ambapo msikiti ulianza kutoa huduma.

Mwaka 2015, baadhi ya wanachama kutoka Jumuiya ya Waislamu Butiama, waliamua kuungana na waliokuwa wanadai katika shauri hilo, wakidai ndio wamiliki halali wa ardhi hiyo huku baadhi wakijiweka kando.

Kulingana na aya ya 14 na 17 ya hati ya madai, mgogoro uliibuka mwaka 2018 kuhusiana na majengo na ukusanyaji wa kodi ya pango kutoka kwa wapangaji, hivyo mdai katika shauri hilo akaiomba mahakama imtangaze ndio mmiliki halali.

Ushahidi wao ulivyokuwa

Katika kuthibitisha madai yao, wadai waliita mashahidi mbalimbali akiwemo shahidi namba 1, Aziz Magambo aliyeeleza kuwa mwaka 1998, Waislamu wa kijiji cha Butiama waliomba ardhi katika serikali ya kijiji ili kujenga msikiti huo.

Ombi lao liliidhinishwa na shahidi namba 3, Zacharia Wambura ambaye alikuwa mwenyekiti wa kijiji na mwaka 2005, waislamu wa Butiama waliomba haki ya kumiliki kimila eneo hilo na kufanikiwa kupata hati hiyo ya kimila.

Kulingana na ushahidi huo, ujenzi wa msikiti huo ulifanikiswa na Mwalimu Nyerere ambaye aliomba fedha kutoka kwa mfadhili (Gaddaf) na msikito huo ulikuwa na malengo ya kutumiwa na waislamu wote wa Butiama pamoja na wageni.

Magambo aliieleza mahakama kuwa, akiwa mjumbe wa kamati ya ujenzi wa msikiti huo, alieleza kuwa mipango yote ya ujenzi wa msikiti huo ilisimamiwa na ofisa aliyeteuliwa na Mwalimu Nyerere na haukuwa chini ya jumuiya yoyote.

Shahidi namba 2, Bakari Irinda, aliijulisha mahakama kuwa wakati wote wa ujenzi, Bakwata haikutoa msaada wowote wa kifedha kusaidia mradi huo kwa sababu waliambiwa kuwa kila kitu kiligharamiwa na Mwalimu Nyerere.

Imam wa msikiti huo, Nassoro Swaibu, aliyeteuliwa kuwa Imam mwaka 2017, alisema kitendo cha Bakwata kuwa na ofisi katika eneo hilo kilikuwa kinaibua msuguano na Waislamu wa Bunda juu ya nani ni mmiliki wa eneo hilo.

Shahidi huyo alishikilia msimamo kuwa lengo la awali la kujenga msikiti huo ni kutengeneza eneo la kuabudu kwa Waislamu wa Butiama na wageni wote na hilo ndio lilisukuma ombi la kiwanja na ufadhili wa ujenzi wa msikito huo.

Katibu wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania (Baraza Kuu) aliyekuwa shahidi namba 6, alisema Waislamu wa kijiji cha Butiama waliingia kuwa wanachama wa Baraza Kuu Desemba 31, 2015 na kupewa cheti (shahada).

Alilalamika kuwa Bakwata wanahodhi mali ambayo hawaimiliki huku akikiri kuwa kabla ya kujiunga na Baraza Kuu, hakuwa anafahamu ni taasisi gani ya Waislamu wa Butiama walikuwa na unachama nayo, wala kufahamu kamati ya ujenzi.

Shahidi namba 7, Abubakar Nyerere, alisema alijiunga na Uislamu mwaka 2000 na kuteuliwa kuwa katibu wa msikiti wa Masjid Rahman mwaka 2019 na kwamba msikiti huo ulijiunga na Baraza mwaka 2015 na kupewa cheti namba SO 7668.

Alieleza kuwa anafahamu mwaka 2014 Bakwata waliomba kupatiwa eneo la ofisi na kutoa barua ya maombi iliyopokewa kama kielelezo P8 na walipewa kwa muda wa miaka mitano na mwaka 2017 walichukua umiliki na kugoma kuondoka.

Ushahidi wa Bakwata

Shahidi namba 1 wa upande wadaiwa, Salum Nyusika, pia  alielezea kuwa msikiti huo uliopo Butiama ulijengwa kwa ufadhili wa Gaddafi kupitia kwa Mwalimu Nyerere ambaye ndiye aliyeomba ufadhi na ujenzi ukaanza 1999 na kukamilika 2000.

Alieleza kuwa sherehe za ufunguzi wa msikiti huo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo aliyekuwa makamu wa Rais, Dk Omary Ally Juma.

Alisema baada ya ufunguzi huo, msikiti huo uliwekwa chini ya uendeshaji wa Bakwata na funguo zilikabidhiwa kwa Kaimu Mufti wa Tanzania.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, uendeshaji wa msikiti huo ulikuwa wa amani kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2021 ambapo kuliibuka kikundi cha watu kikidai msikiti huo, na mashauri kadhaa yalifunguliwa na kutupwa na mahakama.

Ni ushahidi wake kuwa kama Baraza Kuu ndio walikuwepo mwaka 2017, kwanini mashauri yaliyotupwa yalikuwa yanafunguliwa kwa majina tofauti.

Alipoulizwa swali la dodoso, shahidi huyo alishikilia msimamo kuwa aliupokea msikitio huo na nyaraka za makabidhiano anazo na kusisitiza kuwa msikiti wa Masjid Rahman ni mali ya Bakwata na walipewa na Mwalimu Nyerere.

Shahidi namba 2, Nuru Jabil Mruma, ambaye ni mjumbe wa board, alisema awali msikiti huo wa haukuwa na hati, na wao ndio waliomba umiliki Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) na walipewa kibali na Kabidhi Wasii Mkuu.

Ili kuthibitisha kuwa wakati wa ujenzi wa msikiti huo Bakwata walikuwepo, alitoa mawasiliano mbalimbali kati ya Bakwata na kamati ya ujenzi ikiwamo mapato na matumizi ya ujenzi huo ambapo mahakama ilipokea mawasiliano kama kielelezo.

Shahidi namba 3, Imam Bilal Rashid Ntahonpagaze, alisema yeye anaishi katika eneo hilo la msikiti na kusisitiza kuwa msikiti huo ni mali ya Bakwata kwani hata ankra za maji zilikuwa zinaelekezwa kwa Bakwata na sio walalamikaji.

Hukumu ya Mahakama

Katika hukumu yake, Jaji Komba alisema katika mashauri ya madai, kanuni inayoongoza ni kwamba yule anayetoa madai, ndiye anapaswa kuyathibitisha.

Jaji alisema kulingana na uchambuzi wake, walalamikaji wameshindwa kuthibitisha madai yao ya umiliki wa eneo lililokuwa linabishaniwa kwani walipaswa kuthibitisha kama walipata kibali cha Kabidhi Wasii Mkuu.

“Hilo ndilo hitaji la kisheria kwa chombo chochote cha wadhamini kilichosajiliwa. Ni lazima kipate baraka za Kabidhi Wasii mkuu,” alisema Jaji Komba.

Jaji Komba alisema ni ukweli ulio dhahiri kuwa msikiti wa Masjid Rahman ulijengwa kwa ajili ya Waislamu wa Butiama na uko wazi kwa kila mtu na kwamba walalamikaji na walalamikiwa wamekuwa wakiswali pamoja katika msikiti huo.

“Mlalamikaji na walalamikiwa waliabudu pamoja na maimamu wawili waliohudumia jamaa walikuwa wa pande mbili na wote wawili (wakati huo huo) walichukua nyumba za Imam ndani ya eneo hilo la msikiti,” alisema Jaji.

Kutokana na uchambuzi wa ushahidi, Jaji Komba alitoa amri kuwa Bakwata ndio wamiliki halali wa ardhi hiyo yenye mgogoro iliyopo Butiama ulipo msikiti wa Masjid Rahman na kwamba Waislamu na wageni wana haki ya kuutumia.

Mbali na kuwapa haki Bakwata, Jaji alisema waliofungua shauri hilo watawajibika kulipa gharama za shauri hilo la ardhi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *