Ripoti hito Athari za UNHCR 2025: Hatua dhidi ya Dharura Mpya na Migogoro ya Muda Mrefu” inaonesha taswira nzito ya ufurushwaji wa watu unaosababishwa na migogoro inayoongezekai, majanga yanayojirudia na milipuko mipya ya vurugu, huku rasilimali za kukabiliana na hali hiyo zikiendelea kupungua.

“Mwaka 2025, ufurushwaji wa watu ulitokea katika mazingira ya migogoro ya muda mrefu, majanga yanayojirudia, na milipuko mipya ya vurugu na dharura nyingine zinazoibuka, zikiwemo hatari za majanga ya asili,” amesema Ayaki Ito, Mkurugenzi wa Programu za Dharura na Msaada wa UNHCR. 

Ameongeza kuwa “Katika mazingira haya, timu za UNHCR ziliendelea kuchukua hatua dhidi ya mahitaji ya watu waliolazimika kukimbia makwao, hata wakati vikwazo vikubwa vya rasilimali vilipopunguza uwezo wetu.”

Kutoka Afrika hadi Asia, mahitaji yaongezeka 

Katika mwaka mzima, timu za UNHCR zilibaki mstari wa mbele katika baadhi ya dharura zenye changamoto kubwa zaidi duniani. 

Mwaka jana Shirika hilo liliwasaidia watu waliokimbia ghasia mpya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, kuelekea Burundi na Uganda, kusaidia waliokuwa wakikimbia mapigano mapya ndani na nje ya Sudan Kusini, na kulinda mamilioni ya Waafghan waliorejea au kulazimishwa kurejea kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Pakistan.

Wakati huo huo, migogoro ya muda mrefu ilizidi kuimarika. Vita vinavyoendelea Sudan, mashambulizi yaliyoongezeka Ukraine, na mapigano ya silaha yanayozidi nchini Colombia yaliendelea kusababisha ufurushwaji wa watu mara kwa mara na mara ya pili, na kuongeza hatari kwa mamilioni ya watu ambao tayari walikuwa wamekimbia makazi yao.

Msaada wa kuokoa maisha watolewa chini ya shinikizo kubwa

Licha ya upungufu wa ufadhili, UNHCR ilitoa msaada muhimu kwa kiwango kikubwa. Nchini Sudan pekee, shirika liliwapatia watu nusu milioni maji safi

Pia lilitoa msaada wa kifedha kwa takribani Waafghan nusu milioni waliorejea na Wasyria 120,000 waliorejea makwao, pamoja na kutoa zaidi ya huduma milioni moja kwa watu waliokimbia makazi yao ndani ya Ukraine na katika nchi zinazowahifadhi wakimbizi.

Kwa ujumla, UNHCR ilisimamia aukukabili dharura 24 zilizo hai katika nchi 16 mwaka 2025, zikiwemo dharura 10 mpya. 

Kati ya hizo, saba zilikuwa miongoni mwa operesheni kali, tata na kubwa zaidi ambazo UNHCR ilikabiliana nazo mwaka jana, hususan Sudan na nchi jirani za Sudan Kusini na Chad.

Hata hivyo, ripoti hiyo inaonya kuwa kupungua kwa ufadhili kulizuia kwa kiasi kikubwa kasi, ukubwa na wigo wa msaada wa kuokoa maisha, na hivyo kupunguza idadi ya watu walioweza kufikiwa.

Mtazamo wa 2026: Hatari zinaongezeka, pengo la ufadhili lapanuka

Tukiangalia mbele, UNHCR inaonya kuwa migogoro na ukosefu wa utulivu unaoendelea katika nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Sudan, Sudan Kusini, Ukraine na Venezuela unatarajiwa kusababisha ufurushwaji mpya au kuongeza shinikizo kwa jamii ambazo tayari ni dhaifu mwaka 2026. 

Kwa pamoja, hali hizi zinaathiri takribani watu milioni 52 waliolazimishwa kuhama na zinawakilisha theluthi moja ya mahitaji ya ufadhili wa UNHCR duniani kwa mwaka 2026.

“Hatari zilizo mbele yetu ni wazi,” amesema Ito. “Migogoro inaongezeka, ikisababisha ufurushwaji  mpya na kuongeza mateso ya mamilioni ya watu ambao tayari wamekimbia na kupoteza kila kitu.”

Ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuendelea kujihusisha kikamilifu ili kushughulikia chanzo cha ufurushwaji wa watu, akisisitiza kuwa hatua za kibinadamu pekee hazitoshi.

Hatua za haraka bado ni muhimu 

UNHCR imesisitiza umuhimu wa Mfumo wake wa Hatua za  Dharura (Emergency Response Mechanism), unaotumia ufadhili unaonyumbulika kuimarisha maandalizi ya kimataifa na kuwezesha timu kuchukua hatua mara moja katika saa za mwanzo muhimu za dharura.

Kwa wakati huu,” amesema Ito, “UNHCR itaendelea kutoa utaalamu wake, mitandao na zana zake kujiandaa kwa migogoro, kuchukua hatua za kuokoa maisha na kujenga njia za kujitegemea na kupata suluhu za kudumu.”

Kadri mahitaji ya kibinadamu yanavyoendelea kuongezeka mwaka 2026, shirika hilo linaonya kuwa bila ufadhili wa kutosha, pengo kati ya mahitaji na hatua litaendelea kupanuka  likiwa na athari kubwa kwa wakimbizi.

TAGS: Wakimbizin a wahamiaji, UNHCR, pengo la ufadhili 2025, msaada wa kibinadamu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *