
Mbu Aedes albopictus ambaye hujulikana pia kama Mbu Marara wa Asia ni mbu wa maeneo ya kitropiki, lakini kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, aligunduliwa kwa mara ya kwanza nchini Austria mwaka 2012 na tangu wakati huo ameenea katika majimbo yote ya Austria ikiweko Graz.
Kutokana na ongezeko hilo jiji la Graz liliomba msaada wa IAEA, yenye makao yake makuu Vienna, Austria ili kuanzisha utafiti wa MRR yaani Mark-Release-Recapture, kwa kiswahili, Weka Alama-Achia-Kamata Tena.
Lengo lilikuwa kutathmini uwezekano wa matumizi ya baadaye ya Mbinu ya Wadudu Tasa au (Sterile Insect Technique – SIT) katika kudhibiti ongezeko la idadi ya mbu huyo vamizi.
Hanano Yamada, mtaalamu wa wadudu katika Maabara ya Kudhibiti Wadudu Waharibifu ya Kituo cha Pamoja cha FAO/IAEA anaelezea wanachofanya..
“Sasa tunazalisha mbu dume ambao kisha tunawapeleka kwenye mionzo ili wawe tasa. Kuwafanya tasa kunamaanisha hawaweza kuzaliana. Pindi tunapowaachia shambani wanakutana kimwili na mbu jike mwitu ambao nao hawataweza kupata watoto wowote na hivyo baada ya muda mrefu tutapunguza idadi ya mbu mwitu.”
Katika kipindi cha wiki saba kuanzia mwezi Agosti hadi Septemba mwaka 2025 takribani mbu dume tasa 800,000, waliachiliwa katika eneo la hekta 15 la bustani za kilimo kusini mwa Graz.
Matokeo ya awali ya utafiti wa Graz yaliyochapishwa mwezi huu yameonesha kuwa kiwango cha mayai yasiyo na watoto wa mbu kilikuwa asilimia 70 na idadi ya mbu jike waliotaga mayai yenye mbu hatarishi ilipungua.
IAEA inasema hiyo inaonesha kuwa mbu dume tasa wanaweza kushindana kwa mafanikio na mbu dume wa mwituni, na kwamba kuachiliwa kwao kunaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya mbu katika mazingira ya mijini yenye msongamano mkubwa.
Matokeo ya sasa ni fursa ya kupanga majaribio ya baadaye ya SIT chini ya mazingira ya Austria, ikiwemo usambazaji wa mbu dume tasa, muda wa kuishi, utendaji wa kukutana kimwili mbu dume tasa na mbu jike wa porini, na uwezekano wa utekelezaji wa jumla wa operesheni.
Kwa kuzingatia matokeo haya, Jiji la Graz na IAEA wanaandaa mapendekezo kuhusu hatua zinazofuata kwa msimu wa mbu wa mwaka 2026.