Dar es Salaam. Mwanamuziki wa Bongofleva, Diamond Platnumz amekuwa akisifika kwa kutoa video nzuri za nyimbo zake kitu kichompatia umaarufu na namba kubwa katika mtandao wa YouTube ambapo anaongoza kwa Afrika.

Diamond anaweza kuwa na wimbo usiovutia kwa wengi, lakini linapokuja suala la video, basi anahakikisha wengi wanakuwa upande wake. Hata hivyo, kuna warembo waliobeba sifa za kipekee katika video zake kama ifuatavyo:

1. Avril: Je, unamkumbuka Avril wa Kenya aliyetamba katika wimbo Chokoza (2010)? Basi huyo ndiye mwimbaji wa kwanza nje ya Bongo kufanya kazi na Diamond kama video vixen akionekana katika video ya wimbo Kesho (2012).

2. Wema Sepetu: Miss Tanzania 2006, Wema ana historia kubwa katika muziki wa Diamond, ndiye mrembo pekee aliyetajwa mara nyingi zaidi katika nyimbo za mwanzilishi huyo wa WCB Wasafi. Wema aliyetokea pia katika video ya wimbo, Moyo Wangu (2012), anatajwa katika nyimbo za Diamond kama na Nimpende Nani (2012), Kesho (2012) na Fire (2017). 

3. Rara: Ni mwanamitindo asiye na drama nyingi hasa mitandaoni na ni kati ya warembo wachache walioonekana katika video mbili za Diamond. Amefanya hivyo kwenye Yatapita (2023) na Msumari (2025).

4. Tanasha Donna: Kabla ya muziki, Tanasha kutokea Kenya alikuwa akifanya kazi ya mitindo chini ya wakala, Dominique Model’s huko Brussels nchini Ubelgiji, kisha baadaye akafanya utangazaji wa redio. Mwanzoni mwa uhusiano wake na Diamond ndipo alianza kufanya muziki kisha wakaja kushirikiana katika wimbo wao, Gere (2020) ambao katika video yake walionyesha jinsi gani wanapendana.

5. Esma Platnumz: Je, wajua kuwa dada wa Diamond alionekana katika video ya kwanza ya mwimbaji huyo, Kamwambie (2009) ambayo ndio ilimtambulisha kimuziki?

6. Ndiyo: Esma ameonekana mwishoni kabisa mwa video hiyo na alifanya hivyo ili kumsaidia kuokoa gharama za kuwalipa video vixens maana wakati huo hakuwa na fedha. 

7. Zuchu: Ni mwanamuziki wa pili wa kike kwa Diamond kimsaini katika lebo yake, WCB Wasafi, kwa sasa Zuchu ni kati ya waimbaji waliofanikiwa zaidi kimuziki katika miaka hii mitano tangu alipotoka rasmi. Wakiendelea kugonga vichwa vya habari kwa uhusiano, tayari wameshatoa video nne kati ya nyimbo sita walizoshirikiana. Video hizo ni Cheche (2020), Litawachoma (2020), Mtasubiri (2022) na Inama (2025).

8. Zari The Bosslady: Katika wimbo wake, Fire (2017) akimshirikisha Tiwa Savage kutoka Nigeria ndipo Diamond kwa mara ya kwanza anamtaja mpenzi wake wa zamani na mzazi mwenzake, Zari, katika muziki wake. Kwa kipindi cha takribani miaka minne walichokuwa pamoja Zari alihusika kwa namna moja au nyingine katika muziki wa Diamond akitokea katika video zake mbili, Utanipenda (2015) na Iyena (2018).

9. Malaika Salatis: Huyu anatoka kisiwa cha Reunion ambacho kipo mashariki mwa Madagascar na Kusini Magharibi mwa Mauritius, na hadi sasa ndiye video vixen wa kimataifa aliyefanya kazi nyingi na Diamond. Malaika amecheza sehemu kubwa katika video ya Diamond, Jeje (2020) iliyotazamwa zaidi YouTube Afrika kwa mwaka huo na pia alionekana katika video ya wimbo, Gidi (2022) chini ya mradi wa Global Spin.

10. Hamisa Mobetto: Ni mwanamitindo aliyefanya mambo mengi ikiwemo muziki ambapo alisikika katika wimbo wa Diamond, Mbosso na Lava Lava (Jibebe), kisha akaendelea kutoa kazi zake hadi EP, Yours Truly (2022). Hamisa, mshindi wa tuzo ya Young C.E.O Round Table 2023 kabla hapo alishatokea katika video mbili za Diamond, Mawazo (2012) na Salome (2016) ambayo ilishirikisha warembo wengine akiwemo Tunda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *