WFP inakadiria kuwa watu milioni 318 duniani wanakabiliwa na viwango vya dharura vya njaa au zaidi mwaka huu, huku mamia ya maelfu tayari wakiishi katika hali zinazofanana na baa la njaa. 

Hata hivyo, shirika hilo linasema linafanya kazi kwa chini ya nusu ya bajeti inayohitajika ya dola bilioni 13, hali inayolazimisha kupunguza mgao wa chakula kwa mamilioni ya watu walio hatarini zaidi.

Rania Dagash-Kamara, Mkurugenzi Mtendaji Msaidizi wa WFP anayeshughulikia Ushirikiano na Ubunifu, akizungumza Davos amesema “Dunia haiwezi kujenga masoko thabiti juu ya msingi wa watu milioni 318 wenye njaa. Njaa husababisha watu kufungasha virago, migogoro na ukosefu wa utulivu na haya yote yanavuruga masoko ambayo biashara zinayategemea.”

Pengo la ufadhili linazidisha mgogoro wa kimataifa

WFP inaonya kuwa bila uwekezaji wa haraka, athari zitakuwa mbaya, mgao wa chakula kupunguzwa, milo kukatwa na dharura ya kibinadamu kuongezeka kwa kasi. 

Shirika linasema pengo la ufadhili linamaanisha kwa sasa shirika hilo linaweza kufikia takribani theluthi moja tu ya walio katika uhitaji mkubwa zaidi.

Dagash-Kamara amesisitiza kuwa njaa si tatizo la kimaadili pekee bali pia ni tatizo la kiuchumi. 

Nimekuja Davos nikiwa na mgogoro unaozidi kuongezeka na pia nikiwa na suluhisho, amesema. “Wekezeni katika uthabiti wa kimataifa ambao makampuni yenu yanauhitaji kwa kuunga mkono uwezo wetu uliothibitishwa wa kupunguza njaa.”

Sekta binafsi imethibitisha inaweza kuleta mabadiliko

Shirika hilo linaelekeza kwenye rekodi imara ya ushiriki wa sekta binafsi. Mwaka 2025, makampuni yalikuwa wafadhili wa pili kwa ukubwa wa juhudi za WFP nchini Palestina, na wa kwanza kuunga mkono hatua zake nchini Ukraine mwaka 2022. Tangu 2020, mchango wa sekta binafsi kwa WFP umevuka dola bilioni 2.

Katika kipindi ambacho rasilimali za umma kwa mashirika ya kibinadamu zinapungua, WFP inasema ushirikiano na sekta binafsi unazidi kuwa muhimu zaidi.

Teknolojia kama kichocheo cha athari kubwa

WFP pia inaomba ushiriki wa viongozi wa teknolojia, ikionyesha matumizi yake yanayopanuka ya akili mnemba na mifumo ya kidijitali. Shirika linasema mabadiliko yake ya kidijitali yanatarajiwa kuleta akiba ya dola milioni 92 kwa mwaka, huku uboreshaji wa minyororo ya ugavi unaotumia AI ukitarajiwa kuokoa dola milioni 25 kwa mwaka mara utakapotekelezwa kikamilifu.

Zana za kujifunza kwa mashine sasa zinatoa onyo la mapema la siku 60 kuhusu hatari za uhaba wa chakula katika zaidi ya nchi 90, huku mifumo ya AI ya kugundua udanganyifu ikihakikisha kila dola inayotolewa inawafikia walengwa.

Swali si kama teknolojia inaweza kukabiliana na njaa kwa kiwango kikubwa  tunajua inaweza, amesema Dagash-Kamara. Swali ni kama tutakuwa na rasilimali za kufanya hivyo.

Wito wa kuchukua hatua kutoka Davos

WFP inazihimiza kampuni na viongozi wa biashara kufanya njaa na uhakika wa chakula kuwa kipaumbele cha juu, kuwekeza katika minyororo ya ugavi inayohimili misukosuko, kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema inayotumia AI, na kutumia ushawishi wao wa kibiashara kuhamasisha ufadhili mpya.

Ujumbe kutoka Davos uko wazi, kutokomeza njaa si wajibu wa kibinadamu pekee ni msingi wa uthabiti wa kiuchumi na ustawi wa pamoja wa dunia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *