
Viongozi kadhaa wakuu wa Kanisa Katoliki nchini Marekani wametoa taarifa wakikosoa vikali sera ya mambo ya nje ya Washington na kusema kwamba nafasi yake ya kimaadili katika jukwaa la kimataifa inatiliwa shaka, kuhusiana na migogoro kama ya Ukraine, Venezuela na Greenland.
Taarifa hiyo, iliyosainiwa na Askofu Mkuu wa Chicago, Kardinali Blase Joseph Cupich, Askofu Mkuu wa Washington, Kardinali Robert W. McElroy, na Askofu Mkuu wa Newark, Kardinali Joseph W. Tobin, imesema nchi hiyo inashuhudia “mjadala wa kina na mkali zaidi kuhusu msingi wa kimaadili wa mienendo ya Marekani duniani tangu baada ya kipindi cha Vita Baridi.”
Gazeti la New York Times limetoa maoni kuhusu hatua hiyo, likisema kwamba ukosoaji wa makadinali dhidi ya utawala wa Rais Donald Trump ni kielelezo cha ongezeko la ukosoaji wa Kanisa Katoliki dhidi ya viongozi wakuu wa Marekani.
Makardinali hao watatu wamegusia matukio ya hivi karibuni nchini Venezuela, Ukraine na Greenland wakisema yanaibua maswali ya msingi kuhusu utumiaji wa nguvu za kijeshi, na kutoa wito kwa kile walichokiita “sera ya kigeni yenye maadili ya kweli,” ambapo hatua za kijeshi hutumika kama suluhisho la mwisho katika hali mbaya, na si kama chombo cha kawaida cha sera ya kitaifa.
Gazeti la New York Times limeeleza kwamba waliotia saini taarifa hiyo hawakutaja majina ya nchi zilizotajwa, lakini muktadha jumla unaashiria tishio la Rais Donald Trump la kutaka kutwaa Greenland “kwa kutumia mabavu.”
Makardinali wa Marekani wameeleza wasiwasi wao kuhusu kuibuka kwa mfumo wa dunia unaotegemea mabavu na udhibiti wa kibabe badala ya amani na uhuru.
Mapema mwezi huu, Rais Donald Trump wa Marekani alikuwa ameambia New York Times kwamba maamuzi yake kama amiri jeshi mkuu yanaongozwa na “maadili yake binafsi,” akiongeza kwamba, “Sihitaji sheria ya kimataifa.”