
“Tunazihimiza kwa nguvu pande zote mbili kuzingatia mara moja usitishaji mapigano unaolingana na makubaliano ya Januari 18,” Umoja wa Mataifa umeliambia Baraza hilo ukionya kuwa hali halisi bado ni tete sana.
Akilihutubia Baraza hilo la Usalama, Khaled Khiari, Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Mashariki ya Kati, Asia na Pasifiki, amesema kuwa juhudi za kupunguza mvutano kati ya Serikali ya Syria na Vikosi vya Kidemokrasia vya Syria SDF, zimekwama licha ya juhudi za kidiplomasia zinazoendelea.
Mazungumzo yakwama, wakati unayoyoma
Bwana. Khiari amesema kuwa awamu mpya ya mazungumzo kati ya Serikali ya Syria na SDF yaliyolenga kutekeleza makubaliano ya tarehe 10 Machi 2025 hayakuleta mafanikio ya maana.
Hata hivyo, tarehe 20 Januari, Urais wa Syria ulitangaza kuwepo kwa “maelewano ya pamoja kati ya pande hizo mbili, yaliyotoa kipindi cha siku nne kwa SDF kufanya mashauriano ya ndani.”
SDF imeeleza kujitolea kwao kuunga mkono usitishaji mapigano, lakini muda wa kufikia makubaliano kamili unaelekea kuisha.
“Sasa tumefika siku mbili ndani ya kipindi hiki muhimu,” ameonya Bwana. Khiari, akibainisha kuwa mapigano bado yanaendelea katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Hassaké na pembezoni mwa Aïn el-Arab, ambako kumekuwa na kubadilishana risasi na mapigano makali.
Mgogoro wa kibinadamu bado ni mkubwa
Mbali na hali ya kiusalama, Bwana. Khiari amesisitiza dharura ya mgogoro wa kibinadamu, akitoa wito wa kujizuia, kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu na kuendeleza mazungumzo ya kisiasa ili kuzuia mateso zaidi kwa raia.
UN yaendelea kutoa misaada ya kibinadamu
Licha ya mapigano kuongezeka na changamoto kubwa za kufikia wahitaji, Umoja wa Mataifa na washirika wake wanaendelea kutoa misaada ya kibinadamu kote Syria, eameeleza maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa.
Edem Wosornu, Mkurugenzi wa Idara ya Uendeshaji na Utetezi katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura OCHA, mbele ya Baraza la Usalama amesema kuwa Mfuko wa Kibinadamu wa Syria umetenga dola milioni 2.5 kwa ajili ya kutoa msaada wa dharura kwa watu waliolazimika kuyahama makazi yao na kupunguza athari za msimu mkali wa baridi.
Ameongeza kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR limechukua usimamizi wa kambi ya Al-Hol, ambayo inawahifadhi maelfu ya wanawake na watoto wanaoshukiwa kuwa na uhusiano na Daesh/ISIL.
Dalili za kurejea nyumbani zipo, lakini ukata waendelea
Bi. Wosornu ameeleza kuwa, licha ya changamoto, kuna dalili chanya, akisema kuwa zaidi ya wakimbizi na watu waliokimbia makazi yao milioni tatu wamerudi nyumbani tangu Desemba 2024, huku hali ya uhakika wa chakula ikionesha maboresho madogo nchini humo.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa mafanikio hayo bado ni dhaifu.
“Ili kudumisha na kujenga juu ya mafanikio haya, uwekezaji zaidi katika urejeshaji na maendeleo unahitajika, sambamba na ufadhili wa kibinadamu wa kutosha, unaotabirika na endelevu,” amesema.
Wito wa diplomasia na ufadhili
Bi. Wosornu amewashukuru wafadhili wote kwa kuendelea kusaidia wananchi wa Syria kwa miaka mingi, akikaribisha tangazo la hivi karibuni la Marekani la kujumuisha Syria miongoni mwa operesheni za kibinadamu zitakazoungwa mkono kupitia mifuko ya pamoja inayosimamiwa na OCHA.
Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa “Diplomasia hai ni muhimu ili kuzuia ghasia zaidi na kulinda raia”.