Mwongozo huo unasisitiza kuwa maeneo ya wazi ya umma ni muhimu kwa afya, ukuaji, na ustawi wa watoto, huku ukionya kuwa kadri miji inavyozidi kukua, nafasi salama za watoto kucheza, kutembea na kuungana na wenzao zinazidi kupungua.

Takwimu mpya za mashirika hayo zinaonesha hali ya kushtua ambapo duniani kote, ni asilimia 44 tu ya wakazi wa mijini ndio wanaoishi karibu na maeneo ya wazi ya umma. Hali hiyo ni mbaya zaidi katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, ambapo idadi hiyo inashuka hadi asilimia 30 pekee. 

Maeneo ya watoto kucheza ni haba

Mashirika hayo yamesema mamilioni ya watoto wanaoishi mijini wanakabiliwa na ukosefu wa maeneo ya kuchezea, huku uchafuzi wa mazingira, msongamano wa magari, na majanga ya tabianchi yakizidi kuzuia uhuru wao wa kutembea na kustawi.

Dkt. Etienne Krug, Mkurugenzi wa Idara ya Kuzuia Magonjwa wa WHO, amebainisha umuhimu wa hatua hiyo kuwa “Upatikanaji wa maeneo ya umma yaliyo salama na jumuishi umeunganishwa moja kwa moja na afya ya watoto, ukuaji, ujifunzaji, na mahusiano ya kijamii. Hii ni haki ya mtoto.”

Mwongozo huo unaojulikana kama SPACES, unatoa mfumo wa vitendo wenye misingi sita mikuu ya kuzingatia wakati wa kupanga na kusimamia maeneo ya umma ambayo ni, usalama, michezo, upatikanaji, afya ya mtoto, usawa, na uendelevu

Kupitia misingi hii, miji inahimizwa kupunguza hatari za barabarani, kuweka fursa za michezo mitaani, na kuhakikisha hewa safi na vivuli vinapatikana kwa ajili ya watoto.

Hivi sasa, zaidi ya asilimia 55 ya watu duniani wanaishi mijini, na idadi hiyo inatarajiwa kufikia asilimia 68 ifikapo mwaka 2050. Kwa kuwa ukuaji mkubwa wa miji unatarajiwa kutokea katika nchi zinazoendelea, WHO inasisitiza kuwa huu ni wakati wa kipekee wa kuelekeza maendeleo ya miji katika njia inayolinda na kukuza afya ya kizazi kijacho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *