Brazil. Beki wa Real Madrid, Eder Militao (27), tayari amefunga ndoa na mpenzi wake, Taina Castro (25), ila uhusiano wao una simulizi ya kushangaza iliyoibua hisia mseto na mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki.
Katika ulimwengu wa soka la kisasa ambapo umaarufu na macho ya umma huandamana na kila hatua ya mchezaji, si rahisi kwa mastaa wengi kusimamia maisha yao ya binafsi kwa utulivu.
Hata hivyo, Militao, beki wa timu ya taifa ya Brazil (Selecao), safari yake ya mapenzi na Taina imekuwa ya kipekee kwani imeambatana na uamuzi mgumu, na hatimaye mwanzo mpya wa maisha ya familia.
Uamuzi mgumu ulioleta mjadala, unatokana na ukweli kwamba Taina ni mpenzi wa zamani wa mchezaji wa Flamengo, Leo Pereira, ambaye kwa sasa amechumbiana na Karoline Lima, aliyekuwa mpenzi wa Militao!.
Hivyo kwa kifupi tunaweza kusema wamebadilishana Militao kamchukua aliyekuwa mpenzi wa Pereira ambaye ni Taina, huku Pereira akimchukuwa aliyekuwa mpenzi wa Militao ambaye ni Karoline.
Uamuzi huu wa kushangaza uliwapa wachambuzi wa burudani na udaku kazi ya ziada huku kukiwa na gumzo kubwa katika mitandao ya kijamii lakini kwa Militao na Taina hawakujali, waliendelea na kile walichokiamini.
Walikuja kufunga ndoa ya kiserikali ikiwa ni baada ya Taina kuhama kwao Brazil na kwenda kuishi na Militao nchini Hispania ambapo hadi sasa wapo huko pamoja na familia yao ya watoto watatu.
Kwa pamoja wanawalea watoto hao watatu waliowapata katika mahusiano yao yaliyopita Militao ana mtoto mmoja aitwaye Cecilia aliyezaa na Karoline. Kwa upande wake Taina, alizaa watoto wawili na Pereira, Helena na Matteo.
Maisha yao ya kila siku huko Hispania yamejengwa juu ya msingi wa mshikamano ambapo Taina amechukua jukumu la kulea watoto wote akijenga familia iliyounganisha historia mbili tofauti, lakini yenye lengo moja.
Wakati Militao akipambana kila siku uwanjani kama beki tegemeo wa timu, Taina anaendelea kuwa nguzo yake muhimu akimpa faraja na tumaini la maisha huku wakiendelea kumsubiri mtoto wao wa kwanza.
Mwanzoni, hawakuwa na haraka ya kuweka wazi kilichokuwa kikiendelea kati yao lakini kwa muda mrefu tayari vyombo vya habari vya Hispania na Brazil vilishaanza kuunganisha dots kuhusu uwepo wa penzi lao.
Hatimaye uhusiano wao uliwekwa hadharani mnamo Juni 2024 Taina alipomsindikiza Militao kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA CL) iliyofanyika Wembley, ambapo Madrid ilichapa Dortmund mabao 2-0.
Bila makelele, bila sherehe kubwa, wawili hao walifunga ndoa ya kiserikali mwaka huo huo, ilikuwa ndoa yenye utulivu iliyojaa maana zaidi kuliko maonyesho, kisha ikafuata harusi.
Harusi yao ya kifahari ilifanyika Julai 18, 2025 katika hoteli ya Palacio Tangara huko Sao Paulo nchini Brazil, ambapo takribani wageni 350 wakiwemo familia, marafiki wa karibu na watu mashuhuri walihudhuria.
Ilikuwa ni harusi ya kifahari na yenye hadhi ya kipekee huku mandhari ya bluu tulivu ikitawala. Taina akiwa amevalia gauni la kuvutia kutoka chapa ya Marie Lafayette, alipendeza vilivyo kama bibi harusi wa kisasa.
Mwanamuziki maarufu wa Brazil, Gusttavo Lima alitumbuiza live mbele ya maharusi na wageni, huku harusi yote ikikadiriwa kugharimu takribani Euro308,200 (takribani Sh889 milioni) kwa sasa.
“Maisha huja kwa mshangao zaidi pale unapofuata moyo wako,” ni kauli aliyowahi kuitoa Taina kupitia ukurasa wake wa Instagram akimaanisha kufurahia matokeo ya uamuzi wake.
Lakini Taina ni nani hasa?, kwa mujibu taarifa chache zilizopo, mrembo huyu alizaliwa mwaka 2001 huko Brazil. Baba yake anaitwa Sergio Castro, lakini hajawahi kuweka wazi kuhusu mama yake, ndugu zake au maisha yake ya awali.
Kwa sasa ni mtu maarufu katika Instagram akiwa ana wafuasi zaidi ya milioni 1.6, anatumia mtandao huo vizuri kama mshawishi wa chapa ambapo kila mara huweka maudhui yanayohusu familia na mitindo ya maisha.
Ingawa hapo awali hakuwa maarufu sana mitandaoni, ila tangu uhusiano wake na Militao uwekwe wazi, Taina amekuwa sura inayojulikana sana kwenye mitandao ya kijamii na katika maisha ya beki huyo.
Uwezo wa kufanya kazi zake za urembo na mitindo kwa ufanisi huku akiendelea kuitunza familia vizuri na kwa ukaribu, umefanya apendwe na kuheshimiwa na mashabiki na wafuasi wake wengi mitandaoni.
Hadi sasa Taina anatambulika na wengi si tu kama mke wa Militao, bali kama mwanamke anayetambua kitu gani anachotaka maishani na kuwa tayari kukipigania bila kusita wala kuona aibu.
Kwa pamoja, Militao na Taina wameandika hadithi ya mapenzi inayothibitisha kuwa nyuma ya umaarufu na vichwa vya habari, kuna maisha halisi ya watu wanaopenda, kuumia na kisha kuamua kuanza upya kiroho safi tu!.