Spika wa Bunge la Iran amesema kwamba vitendo vya kigaidi vya hivi karibuni nchini Iran vilikuwa kiungo cha mwisho cha Vita vya Siku 12, na kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani ziliwaunga mkono magaidi waliowaua raia wa Iran, polisi na askari usalama.

Mohammad Baqer Qalibaf, aliyasema hayo jana katika mazungumzo yake ya simu na Bw. Numan Kurtulmuş, Spika wa Bunge la Uturuki. Akiashiria matukio ya hivi karibuni katika uhusiano wa kibunge na wa kikanda, Qalibaf amesisitiza udharura wa kupanuliwa zaidi ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi na kuimarishwa mwingiliano kati ya nchi hizo mbili.

Vilevile mepongeza misimamo iliyo wazi ya Rais, Waziri wa Mambo ya Nje na Bunge la Uturuki katika kuunga mkono serikali ya Iran na watu wake na kusisitiza kwamba: “Matukio ya karibuni nchini Iran yalikuwa operesheni kubwa ya kigaidi na uhalifu unaofanana na ule wa magaidi wa ISIS wenye ukatili mkubwa zaidi.”

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu amesema kwamba jaribio hilo la mapinduzi na vitendo vya kigaidi vilikuwa kiungo cha mwisho katika Vita vya Siku 12 vya Marekani na Israel dhidi ya taifa la Iran, akiongeza: “Utawala wa Kizayuni na Marekani zimewafadhili waziwazi magaidi waliowaua watu wa Iran, na katika baadhi ya matukio, vyombo vyetu vya sheria na usalama, ili kufidia kushindwa kwao huko nyuma.”

Mohammad Baqer Qalibaf amesisitiza kwamba, kutokana na juhudi za vikosi vya usalama, polisi na mahudhurio ya wananchi, amani imerejeshwa katika miji yote ya Iran. Amesema: “Utawala wa Kizayuni unataka kudhoofisha nchi zote za Kiislamu na kuzigawa.”

Kwa upande wake, Spika wa Bunge Kuu la Uturuki, Numan Kurtulmuş ameelezea masikitiko na kutoa rambirambi zake kutokana na mauaji ya mamia ya Wairani wakati wa hujuma ya kigaidi ya hivi karibuni na kusisitiza kwamba: “Usalama na ustawi wa Iran ni usalama na ustawi wa Uturuki, na maumivu yanu ni maumivu yetu.”

Spika wa Bunge Kuu la Uturuki, ameunga mkono mtazamo wa Dkt. Qalibaf kuhusu utawala wa Kizayuni wa Israel na kuongeza: “Nguvu kuu ya utawala wa Kizayuni ni kuharibu umoja wa nchi za Kiislamu na kuzigawanya.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *