
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amewataka Watanzania kudumisha umoja wa kitaifa na kuepuka ubaguzi wa Uzanzibar na Utanganyika, akisisitiza kuwa mshikamano ni msingi wa kupata suluhu ya changamoto za kisiasa na kijamii zinazoikabili nchi.
Amesema matatizo ya ndani, ikiwemo changamoto za demokrasia ya kweli na haki, yanapaswa kutatuliwa kwa mshikamano wa kitaifa badala ya kutegemea msaada kutoka mataifa ya Magharibi, akieleza kuwa mazingira ya siasa za dunia kwa sasa si shwari.
Profesa Lipumba ameyasema hayo leo Jumanne, Januari 27, 2026, wakati wa maadhimisho ya miaka 25 ya tukio la Januari 27, 2001, ambapo wafuasi wa CUF walifariki dunia wakidai haki za kidemokrasia Zanzibar.
Amesema licha ya Tanzania kuwa Taifa huru kwa miongo kadhaa, bado haijafikia demokrasia ya kweli, akieleza kuwa tangu uhuru nchi imekuwa ikikumbwa na migogoro ya kisiasa na kijamii inayochangiwa na kukosekana kwa mfumo wa haki wa kidemokrasia.
Amesisitiza kuwa ushindi wa uchaguzi unapaswa kupatikana kwa njia halali na za haki ili kuimarisha imani ya wananchi katika mifumo ya kidemokrasia.
“Demokrasia ya kweli ni ulinzi wa jamii na ni wajibu wa kila mmoja kuilinda. Hatupaswi kukubali ushindi unaopatikana kwa hila.
“Tunapotafuta haki, ni lazima tuache kubaguana kwa misingi ya Uzanzibar na Utanganyika mshikamano wa kitaifa unahitajika ili kupata suluhu ya matatizo yetu,” amesema Profesa Lipumba.
Aidha, amewataka wananchi kuepuka ubaguzi wa kidini wakati wa mijadala ya haki na demokrasia, akisisitiza kuwa nguvu ya umoja wa kitaifa ndiyo msingi wa kufanikisha demokrasia ya kweli, hususan katika mfumo wa vyama vingi unaoendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali.
“Pamoja na Tanzania kuingia katika mfumo wa vyama vingi bado suala la kupata demokrasia ya kweli bado linasuasua, ili tulitibu Taifa hili tunahitaji kuwa kitu kimoja tuweze kushinda, na kupata tiba ya matatizo ya Kitaifa na kuirudisha nchi katika amani,” amesema
Akirejea uchaguzi Mkuu wa 2025, Profesa Lipumba amedai matukio ya wananchi kupigwa risasi na vyama vya upinzani kutopata matokeo yanadhihirisha ni udhaifu wa demokrasia nchini.
“Serikali inayoundwa bila ridhaa halali ya wananchi hushindwa kutatua matatizo yao na kujenga ustawi wa jamii. Lazima tujue demokrasia kama nyenzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi,” amedai.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa CUF, Mohamed Ngulangwa, amesema chama hicho kinaendelea kudai haki kwa wafuasi wake waliofariki dunia katika tukio la Januari 2001.
Amesema madai hayo wanaamini siku moja yatafikishwa mahakamani, akieleza kuwa tukio hilo liliwaacha wengine wakiwa na ulemavu wa kudumu na linapaswa kuendelea kukumbukwa kila mwaka.
Ngulangwa amesema ni umuhimu kuundwa kwa Katiba Mpya itakayoweka mifumo imara ya haki kwa wananchi wote bila ubaguzi.