Afisa mwandamizi wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS, amejibu vitisho vilivyotolewa na waziri mkuu wa utawala wa kizayuni wa Israel kuhusu upokonyaji silaha huko Ghaza na kusisitiza kwamba, silaha za Muqawama zinahusiana na mwendelezo wa uvamizi na kukaliwa ardhi za Palestina kwa mabavu, na kwamba huo ni uamuzi wa kitaifa ambao hautaachwa hadi uvamizi utakapokomeshwa.

Suhail al-Hindi ametoa msimamo huo leo akijibu kauli za Benjamin Netanyahu, aliyetishia kwamba, silaha za Hamas katika Ukanda wa Ghaza zitakusanywa “kwa namna yoyote itakayowezekana,” na kusisitiza kuwa, silaha za Muqawama zina uhusiano wa moja kwa moja na kuendelea uvamizi unaofanywa na Wazayuni, na ni uamuzi wa kitaifa na wa pamoja wa Palestina.

Al-Hindi ameongezea kwa kusema: baadhi ya kauli za Netanyahu zimetolewa katika muelekeo wa “simulizi za upotoshaji” ili kulionyesha jeshi la Israel kama jeshi la “kimaadili na la kiutu”, dai ambalo haliendani na uhalisia.

Amesema: “Silaha ni suala la kitaifa ambalo haliwezi kutenganishwa na uhalisia wa uvamizi, na uamuzi kuhusiana na hilo ulifanywa na mirengo na wananchi wa Palestina.”

Akiashiria hali ya sasa katika Ukanda wa Ghaza, Al-Hindi amesisitiza kwamba, silaha zilizosalia, zaidi ni za ulinzi wa mtu binafsi, si za kushambulia, na ziko kwenye karibu kila nyumba kwa ajili ya kujilinda.

Afisa huyo wa Hamas amebainisha pia kwamba, Muqawama umetekeleza ahadi zake zote kwa wapatanishi na umekabidhi mwili wa mwisho wa askari wa Israel Ran Gvili.

Amekumbusha pia kwamba Hamas hadi sasa imekabidhi wanajeshi na maafisa 20 wa Israel walio hai na miili 28.

Halikadhalika, al-Hindi ameushutumu utawala wa Kizayuni kwa kukiuka makubaliano, kuendeleza mauaji, kufunga vivuko, na kutoheshimu itifaki za kibinadamu, na akasema, tangu yaliposainiwa makubaliano ya kusimamisha vita hadi sasa, Wapalestina 503 wameuliwa shahidi na zaidi ya 325 wamejeruhiwa.

Afisa huyo wa Hamas amemalizia kwa kusisitiza kwamba, kuheshimu Muqawama makubaliano hayo si ishara ya udhaifu na kwamba taifa la Palestina “halitainua bendera nyeupe” bali litaendeleza Muqawama dhidi ya “adui huyo mtenda jinai”…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *