India. Ni habari mbaya kwa wapenzi wa muziki wa Bollywood baada ya juzi muimbaji na mwanamuziki wa India, Arijit Singh, kutangaza rasmi kuacha muziki.
Arijit, kupitia mtandao wa Instagram, aliandika: “Habari heri ya mwaka mpya kwenu nyote. Ninataka kuwashukuru nyote kwa kunipa upendo mwingi kwa miaka yote kama wasikilizaji.
Nina furaha kutangaza kuwa sitachukua tena kazi yoyote mpya kama mwimbaji wa playback. Kuanzia sasa nimeamua kuachana nayo. Imekuwa safari ya ajabu.”
SABABU ZA KUACHA
Kwenye moja ya mahojiano, Arijit Singh alifunguka kuhusu sababu zilizomfanya achukue uamuzi wa kujiondoa kwenye uimbaji wa playback.
Arijit anasema kuna sababu nyingi zilizo nyuma ya nyota huyo kuacha muziki, mojawapo ikiwa ni kupoteza ushawishi, jambo linalomfanya abadilishe mara kwa mara mipangilio ya nyimbo zake na kufurahia zaidi kuzitumbuiza moja kwa moja jukwaani.
Anaongeza kuwa amechoka kiakili na kimuziki, na sasa anahisi anahitaji kuchunguza mitindo tofauti ya muziki ili aendelee kukua na kustawi kama msanii.
Mwanamuziki huyo anasema sababu nyingine ni kuwapa nafasi waimbaji wapya, ambao wanaweza kumvutia na kumpa msukumo wa kweli, akiamini kuwa mustakabali wa muziki unaendelea kuishi.
“Nimefikia uamuzi huu kwa sababu hakukuwa na sababu moja tu, bali mambo mengi ambayo yamenifanya nifikirie kwa muda mrefu, hatimaye nimepata ujasiri wa kuchukua hatua hii,” anasema.
Moja ya sababu ni kwamba napoteza hamasa haraka, ndiyo maana mara nyingi hubadilisha mpangilio wa nyimbo zangu na kuzipa uhai mpya jukwaani. Ukweli ni kwamba nimechoka, na nahitaji kuchunguza muziki tofauti ili niweze kuendelea kukua na kustawi.
MASTAA WENZAKE
Miongoni mwa mastaa waliofanya kolabo nyingi na Arijit ni mwanamama Shreya Ghoshal aliyemshirikisha kwenye nyimbo kama Samjhawan, Tum Kya Mile, Manwa Lage, Ve Kamleya na nyinginezo zilizoacha alama kwenye muziki wa India. Inadaiwa Shreya, mwenye sauti tamu, na Arijit ni moja ya kolabo zenye nguvu nchini humo kutokana na vipaji vya sauti vya wote wawili.
Baada ya ujumbe huo, Shreya aliandika: “Ni mwanzo wa awamu mpya ya Arijit na mimi nina furaha kubwa kusikia, kusikiliza na kuishi kupitia kile kipaji hiki kinachozalisha. Siwezi kamwe kuita hii kama mwisho wa enzi.”
Aliendelea kusema, “msanii wa kiwango chake hawezi kufafanuliwa kwa njia na vipimo vya kijadi, wala kufungwa katika muktadha wa fomula iliyowekwa. Wakati wa kuruka juu zaidi, mpenzi wangu Arijit.”
Mwanamuziki Hrishikesh Ranade anasema: “Ni hazina ya kipekee kabisa, zawadi ya Mungu kwa tasnia yetu ya muziki. Hebu tuwe na uhakika kwamba tutaendelea kushuhudia muziki wa kuvutia, wenye ubora na utajiri mkubwa kutoka kwake, kama ambavyo amekuwa akitufurahisha hadi sasa. Daima nina hamu ya kusikiliza muziki mwingi zaidi.”
Gwiji wa muziki wa Bollywood, Udit Narayan, alisema: “Arijit amefanya kazi kubwa kwa muda mfupi sana. Kuanzia tuzo, kutambuliwa, umaarufu, fedha hadi kushangiliwa jukwaani, ameyaona yote katika kilele chake. Ni uamuzi wake ikiwa anataka kustaafu, lakini hataacha muziki. Ni chaguo lake, lakini kazi yake imechongwa mioyoni mwa watu na itaendelea kuwepo milele.”
SAFARI YAKE
Arijit alizaliwa West Bengal, India, na safari yake ya muziki ilianza mwaka 2005. Alianza kutambulika zaidi alipokuwa mmoja wa waimbaji kwenye wimbo wa Phir Mohabbat kutoka filamu ya Murder 2 iliyotoka mwaka 2011.
Baada ya kazi hiyo, alipata nafasi ya kuimba kama msanii pekee wimbo wa Tum Hi Ho kutoka kwenye filamu ya Aashiqui 2 iliyotoka mwaka 2013, jambo lililomfanya kuwa nyota wa kiwango cha juu.
Baadaye alitoa nyimbo kama Tum Hi Ho, Channa Mereya, Gerua, Agar Tum Saath Ho, Raabta, Kesariya, Ae Dil Hai Mushkil, Tera Yaar Hoon Main na Tujhe Kitna Chahne Lage, akibadilisha kwa urahisi kati ya nyimbo za mapenzi, ibada na zile zenye nguvu za kuamsha hisia.
Hivi karibuni, Singh ametoa wimbo wa Ghar Kab Aaoge kutoka kwenye filamu ya vita ya kihistoria, Border 2, inayoongozwa na Sunny Deol na Varun Dhawan, uliogusa hisia za mashabiki wengi.
Baadhi ya kazi kama Gerua, Jawan na Zaalima, ambazo Arijit aliingiza sauti, zilichangia kumpa umaarufu mkubwa Shah Rukh Khan, ambaye ulimwengu unamtambua kama mmoja wa waigizaji waliokuza soko la filamu la India.
Hata hivyo, kuna mashabiki wanaomchukulia Shah Rukh Khan kama ndiye anayeimba nyimbo hizo, ilhali ukweli ni kwamba yeye huigiza tu.
MAISHA BINAFSI
Nyota huyo anaweka faragha kubwa katika maisha yake binafsi. Inaelezwa ana mke na watoto watatu. Aliingia katika ndoa na rafiki yake wa utotoni, Koel Roy, Januari 2014 katika sherehe ya faragha iliyofanyika kwenye hekalu la Tripathi huko West Bengal.
Koel na Arijit walikuwa marafiki tangu utotoni, na Koel alikuwa na binti kutoka kwenye ndoa yake ya awali.
Hiyo ilikuwa ndoa ya pili kwa Arijit baada ya awali kuachana na Ruprekha Banerjee, mshiriki mwenzake katika shindano la Fame Gurukul lililofanyika mwaka 2013.
Hata hivyo, uhusiano wao haukudumu kwa muda mrefu, na baadaye wakaachana huku tofauti za hisia na msongo wa kazi zikitajwa kuwa sababu za kutengana kwao.
Baadhi ya tuzo alizobeba ni Filmfare Awards kama Wimbo Bora wa Mwaka kwa Kalank (2022) na Kesariya (2023), pamoja na tuzo ya Best Male Playback Singer.
Pia amejinyakulia tuzo nyingine kama IIFA Awards, Zee Cine Awards, Screen Awards na Stardust Awards katika kipengele cha Best Male Playback Singer.