Anaeleza kwamba nchini Haiti, ambako zaidi ya nusu ya wananchi wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, msaada wa dharura wa FAO unasaidia familia kurejea haraka katika uzalishaji wa chakula; huku nchini Jamhuri ya Dominika, juhudi za kuzuia homa ya nguruwe ya Afrika zimeboresha kwa kiasi kikubwa usalama wa kibaolojia mashambani na kuondoa kabisa maambukizi ya ugonjwa huo katika mashamba yaliyoidhinishwa.
Chanjo ya Polio Ethiopia
Nchini Ethiopia, Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO limeeleza kwamba Ethiopia imefanikiwa kutekeleza mizunguko minne ya uchanjaji watoto kwa njia ya matone dhidi ya ugonjwa wa polio.
Mwaka jana 2025 Ethiopia kwa kutumia chanjo ya nOPV2 ilitekeleza uchanjaji huo kupitia mzunguko mmoja wa nchi nzima na mitatu kupitia maeneo mbalimbali ya nchi na kufanikiwa kuwafikia watoto milioni 26 katika mikoa yote. Wakati huo huo, katika kanda 22 za mikoa saba ya Amhara, Oromia, Somali, Ethiopia kusini, Harari, Dire Dawa na Afar, chanjo hiyo ilitolewa kwa pamoja na chanjo nyingine ya matone inayofahamika kama bOPV ambayo imeidhinishwa na WHO ikiwa ni mchanganyiko wa dawa mbili. Kampeni hizi za chanjo zilikuwa nguzo muhimu ya mkakati wa Ethiopia wa kuzuia maambukizi ya virusi vya polio vilivyobadilika, kuziba mapengo ya kinga, na kuimarisha ufuatiliaji.
Mchungaji anawatia alama mbuzi zake baada ya kupata chanjo ya Peste des Petits Ruminants (PPR) katika jimbo la Laghman, Afghanistan.
Afghanistan
Na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, (FAO) kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Asia (ADB) wametangaza kuwa wanatekeleza mpango wa dola milioni 100 ili kuimarisha uhakika wa chakula na lishe pamoja na kurejesha kipato kinachotokana na kilimo kwa zaidi ya watu milioni moja walio katika mazingira magumu kote nchini Afghanistan.
Taarifa ya FAO iliyotolewa leo katika makao makuu ya shirika hilo jijini Roma, Italia na katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul imeeleza kwamba katika kipindi cha miaka miwili ijayo, mradi huu utasaidia zaidi ya kaya 151,000 wakiwemo waliorejea kutoka Pakistan na Iran, jamii zinazowahifadhi, pamoja na familia zilizoathiriwa na matetemeko ya ardhi na mafuriko ya hivi karibuni. Mpango huu utasaidia kaya za vijijini kurejesha vyanzo vyao vya maisha, kulinda mifugo, na kujenga upya mifumo ya uzalishaji wa kilimo iliyovurugika.