Luteni Jenerali Subramanian ametanabaisha hayo hapa makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani alipohojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa ya kihindi wakati huu akitamatisha jukumu lake huko Juba, Sudan Kusini.
“Hata sasa tunapozungumza leo, tuko karibu zaidi na hatari yavvita vya wenyewe kwa wenyewe kuliko ilivyokuwa miaka mitano hadi sita iliyopita. Tuko katika hali ambapo makubaliano ya amani yako hatarini. Na pale kila mdau anapoelewa kwamba kuyadumisha makubaliano haya ya amani kuwa kiini cha hatua zetu zote na kuyatekeleza licha ya changamoto zote, hiyo ndiyo njia pekee ya kusonga mbele. Hata hivyo, pamoja na hayo, makubaliano ya amani leo yanakabiliwa na changamoto kwa njia zaidi ya moja.”
Miongoni mwa tishio ni habari potofu akisema kila inapochipuka wanachukua hatua.
“Tunaendelea kujifunza katika kila fursa. Popote ambapo kumekuwa na upungufu katika mwitikio wetu dhidi ya taarifa fulani potofu, tunajitahidi kujirekebisha. Kwa sasa, tuna mkakati unaofanya kazi. Kwa bahati mbaya, katika nchi ambayo haina miundombinu ya kawaida ya mawasiliano inayohitajika, taarifa potofu hutawala, kwa kuwa ni mitandao ya kijamii pekee inayofikia kila makazi.”
Wahenga husema kuwa kila jambo lina pande mbili, vivyo hivyo huko Sudan Kusini, licha ya tishio, kuna mafanikio ambayo ameshuhudia Kamanda huyu wa Kikosi cha UNMISS anayemaliza muda wake.
“Katika miaka mitatu na nusu ambayo nimekuwa shuhuda wa operesheni za UNMISS, tumeokoa watu 162,000, sio tu dhidi ya mapigano, bali pia wengi wao dhidi ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi yanayodhihirishwa na mafuriko yasiyo ya kawaida nchini humo. Hivyo kwa wastani watu kati ya elfu 30 hadi elfu 35 wanalindwa na vitisho dhidi ya mafuriko kila mwaka, na takribani elfu 15 hadi elfu 20 wanaokolewa dhidi ya mashambulizi. Na nyongeza ya hapo tunaokoa watu dhidi ya ukatili wa kingono.”
Kamanda huyo wa Kikosi amehimiza serikali ya Sudan Kusini na wadau wenye nia ya dhati ya kuleta amani katu wasitume taarifa potofu dhidi ya Umoja wa Mataifa, akifafanua kuwa Umoja wa Mataifa uko nchini humo kusaidia jamii ambayo imepitia machungu mengi tangu mapigano yazuke mwezi Desemba mwaka 2013. Hivyo huu ni wakati wa wadau kuepuka kuongeza machungu kwa kumomonyoa uaminifu wa chombo hicho bila haki.
Mkataba wa amani ulioboreshwa ulitiwa saini mwaka 2018 huko Addis Ababa Ethiopia na pamoja na mambo mengine unataka kusitishwa kwa mapigano, kuwa na madaraka ya pamoja, kuleta maridhiano ya kitaifa na kurejesha utawala wa kidemokrasia.
Msichana mchanga anachimba mashimo ili kuandaa makao kwa familia yake katika kambi ya wakimbizi huko Tawila ambapo mamia ya watu kutoka Al Fasher wametoroka kwa usalama.
2. Hali ya njaa inatishia maisha ya watoto nchini Sudan
Sudan inakabiliana na viwango vya hatari vya njaa, ambapo mamilioni ya watoto kama Noon wako katika hatari kubwa. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) liko shambani, likitoa msaada muhimu wa lishe, maji safi, na ulinzi. Hata hivyo, mahitaji ni makubwa, na msaada zaidi unahitajika haraka ili kuokoa maisha ya watoto hawa.
Familia ya Noon, msichana mwenye umri wa miaka 11, ililazimika kuikimbia nyumba yao huko Al-Fasher baada ya mabomu kushambulia mji huo. Safari ya kuhama iliwapeleka kwanza kwenye kambi ya wakimbizi ya Zamzam, kisha Tawila, huku kila hatua ikichukua kipande cha maisha yake ya utoto. Katika mazungumzo yake, anaelezea jinsi safari hiyo ilivyoanzia,
“Yalianza tulipokuwa shuleni. Mabomu yaliporushwa na risasi zikirushwa kila mahali, watu walikimbia nje, hivyo tuliungana nao. Tulitembea hadi tukafika kambi ya Zamzam. Huko, maji yalikuwa na chumvi na chakula kilikuwa ghali sana.”
Familia ya Noon ililazimika kukimbilia Tawila baada ya risasi kuanza kuwa karibu nao. Lakini hapa wanakabiliwa na uhaba wa chakula na maji safi ya kunywa. Anasimulia
“Kwa sasa tunapata milo miwili tu, kifungua kinywa na chakula cha jioni. Ukosefu wa chakula umenidhoofisha. Kila wakati naumwa na kichwa au tumbo , na mara kwa mara ninaenda hospitali. Baba yangu anafanya kazi kwa bidii ili atupatie chakula na maji hapa. Ndugu zangu wanalia, na mimi huwa nawasihi tuvumilie, baba atatuma pesa kwetu hivi karibuni.”
Mahali ambapo Noon hapo awali alicheza kwenye mitaa, sasa anakutana na njaa, miili ya watu, na risasi. Anaeleza kwa huzuni
“Maisha yangu yalikuwa mazuri hapo awali. Nilicheza na marafiki zangu na kuzungumza na jamaa zangu. Ninaifikiria nyumba yangu, kitanda changu, marafiki zangu na familia yangu.”
Hadithi ya Noon inatuonesha jinsi njaa na mzozo vinavyoathiri maisha ya watoto. UNICEF ipo mstari wa mbele kutoa msaada, lakini msaada zaidi unahitajika kwa haraka.