Iran imetangaza kwamba kauli za “kuchochea vita” za Donald Trump zinazidisha mvutano wa kikanda.
Amir Saeed Iravani, Balozi na Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa, amesema kwamba “kauli za Rais wa Marekani Donald Trump zinazochochea moto wa vita, zinazidisha mvutano wa kikanda, zinaongeza hatari ya makosa ya kimahesabu na zinahatarisha moja kwa moja amani na usalama wa kimataifa.”
Akiashiria vitisho vipya vya Rais wa Marekani, Iravani alisema katika barua yake kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Baraza la Usalama siku ya Jumatano, kwamba: “Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapinga na kulaani vikali kauli hizo za kuchochea vita, ambazo si za uwajibikaji, ni za kichochezi na ni kinyume kabisa na kanuni na sheria za kimataifa na Hati ya Umoja wa Mataifa.”
Mwanadiplomasia huyo mwandamizi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa: “Tishio la kutumia nguvu dhidi ya taifa huru ni ukiukaji wa wazi wa Kifungu cha 2, Sehemu ya 4, cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa ambacho kinakataza waziwazi utumiaji wa nguvu na vitishio vya kutumia nguvu dhidi ya ardhi au mamlaka ya kujitawala kisiasa ya taifa lolote.”
Ameendelea kusema: “Kwa masikitiko makubwa, kauli hizi hazina kifani, na ni sehemu ya muundo mpana uliosajiliwa wa mashinikizo, vitisho, vitendo vya kuvuruga usalama, shughuli za kijasusi za siri na mashinikizo haramu ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.”

Inaonekana kwamba kauli za vitisho za Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya Iran mnamo Januari 2026, zilizoambatana na kutumwa kundi la meli za kivita katika eneo la Asia Magharibi na tishio la moja kwa moja la kijeshi dhidi ya Iran, zimezidisha mvutano uliopo hadi kiwango hatari kwa sababu kadhaa muhimu:
Kwanza ni hatari iliyoongezeka ya makosa ya kimahesabu na majibishano ya kijeshi. Tishio la wazi la Trump na kutunisha misuli ya nguvu za kijeshi limefuatiwa na jibu la Iran la kuwa tayari kukabiliana na tishio hilo. Katika muktadha huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araqchi, ameonya kwamba vikosi vya jeshi la Jamhuri ya Kiislamu viko tayari kujibu “mara moja na kwa nguvu” shambulio lolote. Majibizano haya ya vitisho na utayarifu wa vita huunda mazingira ambayo makosa madogo ya kimahesabu au mgogoro mdogo wa mpakani unaweza kupanuka haraka na kuwa vita kamili. Katika barua yake kwa Umoja wa Mataifa, Iran imeonya waziwazi kwamba kauli hizi “zinazidisha hatari ya makosa ya kimahesabu.”
Pili ni kuharibiwa njia za kidiplomasia na kubana machaguo mezani. Makabiliano haya makali yanadhoofisha uwezekano wowote wa kujiondoa kwenye mgogoro kwa njia za kidiplomasia. Ripoti zinaonyesha kwamba, mazungumzo ya awali kati ya Washington na Tehran kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran yamekwama, na mkwamo huu umekuwa sehemu ya sababu zinazotumiwa kuhalalisha lugha ya vitisho. Hata hivyo, vitisho vya shambulio kubwa au “kuondoa madarakani utawala” wa Iran ili kufikia makubaliano yasiyokubalika, kama kusitishwa kabisa urutubishani wa urani nchini Iran na kuharibiwa akiba ya urani iliyorutubishwa, kubana uwezo wa makombora na kukomeshwa misaada ya Tehran kwa Mhimili wa Muqawama katika eneo la Magharibi mwa Asia, vinaharibu hali ya kuaminiana inayohitajika ili kuanza tena mazungumzo.
Wachambuzi wa mambo wanasema kwamba matamshi ya aina ya Trump sio tu kwamba yamebana uwezo wa rais wa Marekani wa kupata suluhisho mbadala, lakini pia yanaifanya Iran iazimie zaidi kutetea misimamo yake ya kimantiki dhidi ya madai yasiyo na mantiki ya Marekani.

Suala la tatu ni wasiwasi wa washirika wa kikanda wa hatari ya kupanuka zaidi migogoro. Matokeo mabaya zaidi ni uwezekano wa kuzuka mapigano makubwa zaidi katika eneo la Magharibi mwa Asia. Washirika wa jadi wa Marekani eneo la Asia Magharibi, ambao wenyewe wanaogopa ushindani na Iran, wamemuonya Trump faraghani kwamba shambulizi lolote la kijeshi linaweza kusababisha “mgogoro mpana zaidi.” Washirika hao wa Washington wanaogopa kwamba, Iran itajibu shambulio hilo si tu kwa kuanzisha mashambulizi dhidi ya ngome za Marekani, bali pia kwa kuanzisha vita vya kikanda. Hofu hii inaonyesha kwamba usalama katika Ghuba ya Uajemi ni dhaifu sana kiasi kwamba hata washirika wa Kiarabu wa Marekani hawataki kuingia kwenye vita vya pande zote.
Kwa ujumla, vitisho vipya vya Trump dhidi ya Iran, vilivyowekwa ndani ya mfumo wa mbinu ya ama kujisalimisha au mashambulizi ya kijeshi, sio sera iliyopangwa kwa umakini, bali ni sababu ya kuzidisha ukosefu wa utulivu. Vitisho hivyo vimeiweka kanda ya Asia Magharibi ukingoni mwa mgogoro mkubwa kwa kuunda majibizano ya vitisho vya pande zote, kufunga milango ya diplomasia na kuwatia wahfa na hofu hata washirika wa Marekani.