Dar es Salaam. Imekuwa ni jambo la kawaida duniani kote wasanii wa muziki kuwatumia wapenzi wao katika video za nyimbo zao, hata hivyo imekuwa ni mara chache kuona msanii akifanya hivyo zaidi ya mara moja.
Nchini Tanzania wasanii wa Bongofleva nao wapo katika utamaduni huo, wengi wamefanya hivyo kwa miaka mingi lakini kuna wachache ambao wamejaribu zaidi ya mara moja kama ifuatavyo.
Diamond – Wema, Zari & Hamisa
Mwimbaji huyu wa WCB Wasafi karibia warembo wote ambao wamewahi kuwa nao katika uhusiano ameshafanya nao video za nyimbo zake.
Alianza na Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu ambaye alitokea kwenye video ya wimbo, Moyo Wangu (2012) chini ya Visual Lab: Next.
Kisha akafuata Zari The Bosslady aliyeonekana kwenye video ya wimbo, Utanipenda (2015), pamoja na Iyena (2018) ambayo ilitoka wiki chache baada ya Zari kutangaza kuachana kwao.
Pia Hamisa Mobetto ambaye hawakuwi kuweka wazi uhusiano wao, naye aliigonekesha vizuri video ya wimbo, Salome (2016), ikiwa ni baada ya Hamisa kuoneka katika video ya wimbo, Mawazo (2012).
Harmonize – Wolper, Sarah & Kajala
Wakati penzi la Harmonize na Jacqueline Wolper lipo katika kilele cha mafanikio yake, walisafiri hadi Afrika Kusini kufanya video ya wimbo wake, Niambie (2017) ambayo imeshatazamwa YouTube mara milioni 29.
Baadaye Harmonize alianzisha uhusiano na mrembo kutokea Italy, Sarah mbaye walisafiri wote hadi Ngorongoro na kufanya video ya wimbo, My Boo (2019) ambao alishirikiana na Q Chief.
Haikuishia hapo, hata alipokuja kuwa na Kajala Masanja utamaduni ukaendelea kuwa ule ule. Kajala ameoneka katika video ya wimbo wa Harmonize, Nitaubeba (2022).
Shilole – Nuh Mziwanda & Uchebe
Wakati Nuh Mziwanda bado yupo katika uhusiano na Shilole alimshirikisha katika video ya wimbo wake, Msondo Ngoma (2014), hivyo katika video yake Shilole anaonekana mwanzoni hadi mwisho.
Baadaye Shilole alikuja kuzama kwenye penzi jipya na Uchebe, wimbo wa kwanza kwa Shishi kuutoa baada ya kufunga ndoa unaitwa Mchaka Mchaka (2018), katika video yake alijiachia vilivyo na mume wake huyo ambaye tayari wameachana.
Ben Pol – Ebitoke & Anerlisa
Mkali huyu wa RnB ambaye kila uhusiano wake unaokuwa kwenye vyombo vya habari lazima yawe na drama nyingi, wakati wa penzi lake Ebitoke, aliamua kumtumia kwenye video ya wimbo wake, Natuliza Boli (2018).
Mwishoni mwaka 2020, Ben Pol alichia wimbo ‘Kidani’ ambao katika video yake amejiachia na aliyekuwa mkewe kutokea Kenya, Anerlisa ambaye walikuja kuachana kwa maneno ya hapa na pale.
Jux – Vanessa, Nayika & Priscilla
Kipindi cha penzi lao Vanessa Mdee alionekana kwenye video ya wimbo wa Jux, Sisiki (2014), pia walikuja kutoa nyimbo mbili pamoja ambazo ni Juu (2016) na Sumaku (201).
Vilevile Vanessa amekuja kuokena tena kwenye video ya wimbo wa mchumba wake, Rotimi, Love Somebody (2020).
Baada ya kuachana na Vanessa, Jux aliamua kubadili mapishi ndipo akafunga safari hadi Bangkok nchini Thailand na kukutana na Nayika ambaye amejiachia naye kwenye video ya wimbo wake, Unaniweza (2020).
Haikuishia hapo, Jux akaenda Nigeria, huku anakutana na mkewe Priscilla ambaye ameonekana kwenye video zake kama Ololufe Mi (2024), Si Mimi (2025), God Design (2025), Thank You (2025), na See Body (2026).
Rayvanny na Fahyma & Paula
Hakuna ubishi kuwa Rayvanny ndiye anaongoza Bongo kwa kufanya video nyingi zaidi na mpenzi wake, ambaye ni Fahyma a.k.a Fahyvanny ambaye wamejaliwa kupata mtoto mmoja.
Wawili hao wamefanya pamoja video sita ambazo ni Kwetu (2016), Natafuta Kiki (2016), Siri (2017), Forever (2023), Habibi (2023) na Mwambieni (2023).
Na kipindi ana uhusiano na Paula, binti wa Kajala Masanja na P-Funk Majani, Rayvanny alimtumia mrembo huyo katika video ya wimbo wake, Wanaweweseka (2021) iliyosimamiwa na Director Eris Mzava.