Dar es Salaam. Kolabo katika muziki wa Bongo Fleva ni nyingi na kuna vichwa vikikutana kinachotokea ni mzuka tu. Lazima wakubalike kutokana na kuachia kazi kali.

Tangu muziki wa Bongo Fleva ubadilike na kuwa biashara kubwa tofauti na miaka ya nyuma, hata wasanii wanaotafutana kufanya kolabo wanazingatia hilo na si kuokotana tu.

Wanaangalia nani wasimame naye ili kuleta ladha na mshiko sokoni, huku pia zikiteka hisia za mashabiki ambao ndiyo wateja wao kwa kiasi kikubwa.

Hizi hapa baadhi ya kolabo ambazo zinakimbiza mitandaoni kwani zimekutanisha vichwa vikali na zaidi wanakubalika kwa mashabiki na kila wanapotoa wimbo, mapokeo yanakuwa makubwa.

Zuchu vs Dvoice

Wawili hao hivi karibuni wameachia kazi ya pamoja ‘Baridi’, na katika siku 10, umefikisha zaidi ya watazamaji Milioni moja ikiwa ‘trending’ namba mbili kwenye chati ya video zinazotazamwa katika mtandao wa YouTube.

Kwa pamoja wawili hawa kutoka lebo ya Wasafi wametoa nyimbo tano baada ya kushirikiana kwenye ngoma kama ‘Nani’, ‘Hujanizidi’, ‘Bambam’, ‘Nimezama’ na ‘Baby Mpya’.

Ni wazi kukubalika kwao kunawafanya wazidi kushirikiana na safari yao ya muziki inaweza kusababisha kolabo nyingine nyingi.

Alikiba vs Vanilla

Mmiliki wa lebo ya Kings Music, Alikiba na msanii wake Vanilla wameshatoa ngoma kali mbili, ‘Tamu Chungu’ na ‘Rafiki’ na zote zimewabamba mashabiki wao.

Ni takriban miaka minne sasa tangu Vanilla atambulishwe na Kings Music Novemba 2022.

Kama ilivyo ‘Tamu Chungu’ iliyosubiriwa kwa hamu na mashabiki na kuwashika, ‘Rafiki’ waliyomshirikisha pia Abdu Kiba ilipenya na kukubalika ikiwa ni miezi miwili tu tangu iachiwe, huku kukiwa na ufundi mwingi wa sauti na wanavyonata na biti.

Diamond Platnumz vs Rayvanny

Kwa muda mrefu sasa, Diamond Platnumz na Rayvanny wamekuwa wakiongoza katika muziki wa Bongo, na kila mmoja ameweka alama yake kimataifa.

Ushirikiano wao katika wimbo wa ‘Tetema’ ulikuwa moja ya mafanikio makubwa zaidi kwenye soko la muziki la Afrika Mashariki. Wimbo huu umeendelea kufanya vizuri kwenye majukwaa ya mtandao na video yake imefuatiliwa zaidi mitandaoni.

Ukiachana na Tetema ambao umemtambulisha zaidi Rayvanny wawili hao walifanya kolabo nyingi ikiwemo Nesanesa (2025), Nikutongoze (2023), Iyena (2018) ambazo zote ziliacha alama.

Harmonize vs Ibraah

Kolabo kati ya Harmonize na Ibraah, wote kutoka lebo ya Konde Music, imeweza kuonyesha umoja wa nguvu za vijana wa Bongo. Wimbo wao wa ‘Dharau’ ni moja ya kolabo ambazo zimekuwa na mafanikio makubwa kwenye jukwaa la muziki la Afrika Mashariki na video yake imekuwa kivutio kwa mashabiki.

Kabla ya Ibrah kutimka kwenye lebo hiyo mwaka jana walifanmya kolabo sita One Night Stand (2020), Friend Zone (2025), Tunapendeza (2023), Mdomo (2022) kutoka kwenye albamu yake ya High School na Addiction (2021).

Kati ya hizo zilizovunja rekodi ya kutazamwa kwenye mtandao wa Youtube ni mbili, ‘One Night Stand’ yenye watazamaji zaidi ya Milioni 24 na ‘Dharau’ yenye nayo 32 Milioni.

Diamond Platnumz vs Jux

Mbali ya wawili hao kuwa na majina makubwa kwenye muziki lakini ni marafiki wa muda mrefu, tofauti na matarajio ya wengi kwamba kutokana na ukaribu wao wangefanya kolabo nyingi lakini imekuwa tofauti.

Diamond na Jux wamefanya kolabo tatu ‘Ololufemi’ (2024), ‘Enjoy’ (2023) na ‘Sugua’ kutoka kwenye albamu ya mkali huyo wa R&B ya ‘The Love Album’ iliyoachiwa rasmi mwaka 2019.

Kolabo zote tatu zinaonyesha Jux ndiye aliyemshirikisha Diamond na zote zimefanya vizuri hasa kwenye mtandao wa You Tube lakini iliyofanya vizuri zaidi ni ‘Enjoy’ iliyopiga zaidi ya watazamaji Milioni 100.

Abigail Chams vs Harmonize

Kolabo kati ya Abigail Chams na Harmonize ni mfano wa mkakati wa kukuza vipaji vipya kupitia wasanii wakubwa. Wimbo wao ‘Me Too’ uliwakutanisha msanii chipukizi mwenye sauti ya kimataifa na msanii mwenye uzoefu mkubwa katika tasnia ya muziki Afrika Mashariki.

Video ya wimbo huu ilijengwa kwa mtindo wa kisasa ikionesha taswira ya kimataifa na kumsaidia kumtambulisha zaidi Abigail Chams kwa mashabiki wa Bongo na nje ya nchi.

Video ilifanya vizuri kati ya kolabo nne walizofanya pamoja na kuingia kwenye hatua za mchujo kwenye tuzo kubwa za Grammy zinazotolewa kila mwaka duniani.

Mbali na Me Too wawili hao walitoa kolabo nyingine kama ‘Lala’, ‘Leave Me Alone’ na ‘Closer’.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *