f

Chanzo cha picha, Reuters

Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa ni “hatari sana” kwa Uingereza kuimarisha mahusiano yake na China, kauli aliyotoa wakati Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer, akiendelea na ziara yake rasmi mjini Beijing.

Trump alikuwa akijibu makubaliano yaliyotangazwa baada ya Sir Keir kukutana na Rais wa China, Xi Jinping, katika ziara ya siku tatu iliyolenga kufufua na kurekebisha upya uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.

Makubaliano hayo yanalenga kuongeza biashara na uwekezaji kati ya Uingereza na China.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa filamu ya maandishi kuhusu mke wake, Melania Trump, alisema: “Ni hatari sana kwao kufanya hivyo,” alipoulizwa maoni yake kuhusu Uingereza kuimarisha uhusiano wa kibiashara na China.

Kauli hiyo ilitolewa kufuatia matamshi ya Sir Keir kwamba uhusiano wa Uingereza na China uko katika “hali nzuri na imara” baada ya mkutano wake na Rais Xi katika Ukumbi Mkuu wa Watu, siku ya Alhamisi.

Waziri Mkuu huyo aliongeza kuwa mikutano aliyofanya ilikuwa “ya mafanikio makubwa” na ilifikia kiwango cha ushirikiano ambacho Uingereza ilikuwa inakitarajia.

“Tulizungumza kwa uwazi na kwa heshima, na tumepiga hatua muhimu, kwani Uingereza ina mchango mkubwa wa kutoa,” alisema Sir Keir alipohutubia Jukwaa la Biashara la Uingereza na China katika Benki ya China mjini Beijing.

Miongoni mwa matokeo ya ziara hiyo ni makubaliano ya kusafiri bila visa, kupunguzwa kwa ushuru wa whiski, pamoja na uwekezaji wa pauni bilioni 10.9 kutoka kampuni ya AstraZeneca kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya uzalishaji nchini China.

Aidha, makubaliano ya kuimarisha ushirikiano katika maeneo mengine, yakiwemo mapambano dhidi ya uhalifu uliopangwa na uhamiaji haramu, yalitangazwa.

Mwenyekiti wa Chama cha Biashara cha Uingereza nchini China, Chris Torrens, aliitaja ziara hiyo kuwa “ya mafanikio” na kusema kuwa ni jambo la msingi kwa Uingereza kuendelea kushirikiana na China, mmoja wa washirika wake wakubwa wa kibiashara.

Bw Torrens alieleza kuwa, ingawa Marekani mara nyingine huweka vikwazo au kutoza ushuru kwa mataifa yanayofanya biashara na China, bado kuna uwezekano mkubwa kwa Marekani yenyewe kuingia makubaliano ya kiuchumi na China, jambo analosema linatarajiwa kutokea mwaka huu mwezi April.

Awali wiki hii, Trump alitishia kuiwekea Canada ushuru iwapo ingetimiza makubaliano ya kiuchumi iliyoafikiana na China kufuatia ziara ya kiongozi wake, Mark Carney, mjini Beijing.

Kwa mujibu wa takwimu za Idara ya Biashara na Biashara ya Kimataifa ya Uingereza, Marekani ilikuwa mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa nchi hiyo mwaka 2025, huku China ikishika nafasi ya nne.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *