Shirika la ndege la Ethiopian Airlines limefuta safari za ndege kuelekea kaskazini mwa mkoa wa Tigray baada ya mapigano ya silaha kuzua hofu ya kuibuka mzozo mpya katika eneo hilo.

Shirika la Ndege la Ethiopia lilifuta safari za ndege kuelekea eneo la kaskazini mwa Tigray jana Alkhamisi, huku wakazi wa eneo hilo wakijaribu kutoa pesa kwenye mabenki baada ya mapigano kati ya vikosi vya majeshi ya kikanda na kitaifa kuzua hofu ya kuibuka mzozo mpya.

Vyanzo vya kidiplomasia na serikali vimeripoti kuwa mapigano yalizuka mapema wiki hii katika eneo linalogombaniwa magharibi mwa jimbo hilo.

Afisa mmoja wa Shirika la Ndege la Ethiopia ameambia Reuters kwamba “kufikia jana Alkhamisi, safari zote za ndege kuelekea jimbo hilo zilikuwa zimefutwa,” bila kutoa sababu maalumu.

Mkazi wa Mekelle, mji mkuu wa jimbo la Tigray, alisema kwamba mamia ya watu walianza kumiminika kwenye mabenki kutoa pesa zao jana Alkhamisi, lakini benki nyingi zilikuwa zikisumbuliwa na uhaba wa pesa taslimu.

Kati ya Novemba 2020 na Novemba 2022, eneo la Tigray lilishuhudia mapigano makali kati ya jeshi la Shirikisho, likiungwa mkono na vikosi vya jeshi la Eritrea, na waasi wa Tigray People’s Liberation Front (TPLF). Mgogoro huo ulisababisha vifo vya takriban watu 600,000 katika eneo hilo.

Vita vya Tigray vilimalizika kwa makubaliano ya amani mnamo Novemba 2022, lakini bado kuna hitilafu kuhusu masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na eneo lenye mgogoro magharibi mwa Tigray na ucheleweshaji wa zoezi la kuwapokonya silaha wapiganaji wa Tigray.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *