
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (bunge la Iran) Mohammad Baqer Qalibaf amesema kuwa, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (SEPAH) ni mojawapo ya vikosi imarai na vyenye ufanisi zaidi vya kupambana na ugaidi duniani.
Spika Walibaf amesema hayo akijibu hatua ya Baraza la Umoja wa Ulaya ya kukiweka Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH katika orodha ya makundi ya kigaidi.
Qalibaf ameilaani hatua hiyo aliyoiita kuwa ya kisiasa na kubainisha kwamba, Ni wale tu ambao wamesimama upande wa magaidi wenyewe ndio wanaweza kukataa rekodi ya jeshi la SEPAH katika kupambana na ugaidi wa DAESH. Qalibaf aliongeza kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X: “Kuunga mkono ugaidi kutasababisha majuto kwa nchi za Ulaya.”
Wakati huo huo, Wizara ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, imelaani katika taarifa yake, kitendo cha Baraza la Umoja wa Ulaya cha kukitaja Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kama shirika la kigaidi na kusema: “Kitendo hiki cha Baraza la Umoja wa Ulaya ni jibu la chuki, la haraka, na la kukata tamaa kwa kushindwa kwao mfululizo katika kushinda azma na irada thabiti ya taifa tukufu la Kiislamu la Iran dhidi ya vitisho vyote vilivyobuniwa na kuelekezwa kutoka nje.
Katika upande mwingine, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetoa taarifa, ikiita uamuzi huo wa Umoja wa Ulaya kuwa haramu, usio na haki, na wa udanganyifu wa kutoa shutuma zisizo na msingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.